tiko
tiko
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza
na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge, mjini Dodoma jana.
Picha na Anthony Siame.
Licha
ya Serikali kusisitiza kuwa uandikishaji wa wapigakura nchi nzima kwa
mfumo wa BVR utakamilika Aprili 28 na Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30,
mwaka huu kama ilivyopangwa, hesabu zilizopigwa na Mwananchi zinakataa
kuwianisha siku zilizosalia na idadi ya mashine za BVR zilizopo na
zinazotarajiwa kuwasili. Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimebaki siku 36
kabla ya Kura ya Maoni kufanyika, huku kukiwapo wasiwasi miongoni mwa
wadau kuhusu uwezekano wa kufanikisha matukio hayo bila manung’uniko.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwaeleza
waandishi wa habari jana kuwa uandikishaji nchi nzima utaanza siku sita
kuanzia leo na kusisitiza kuwa Kura ya Maoni kuridhia au kukaa Katiba
Inayopendekezwa itafanyika Aprili 30, mwaka huu kama ilivyopangwa.
Wasiwasi wa kutofanyika kwa kura hiyo
katika tarehe iliyopangwa unatokana na uandikishaji wa wapigakura kwa
BVR unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ulioanza Februari
23, mwaka huu kutokamilika hata katika mkoa mmoja wa Njombe, wenye
wapigakura 392,634 kati ya milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini
kote.
Hesabu zinavyokataa
Kulingana na takwimu za NEC, BVR moja
inaandikisha kati ya wapigakura 80 hadi 100 kwa siku endapo hakuna
tatizo lolote, hivyo kwa kadirio la chini, iwapo BVR 7,750 zilizoagizwa
na NEC zitawasili nchini kwa mafungu, zitahitajika siku 38 kuandikisha
wapigakura milioni 24 wanaokusudiwa kama kazi hiyo itaanza leo.
Hata hivyo, katika uandikishaji wa
majaribio na baadaye katika Mkoa wa Njombe mashine hizo zimeripotiwa
kukabiliwa na changamoto mbalimbali ama za kukwama, weledi mdogo wa
watumiaji na hali ya hewa, hivyo kufanya idadi iliyokusudiwa
kutokamilika.
Mwandishi wa Mwananchi, Kizzito Noya
aliyekuwa Makambako, Njombe wakati wa uandikishaji hivi karibuni amesema
kwa wastani alishuhudia mashine moja ya BVR ikiandikisha wapigakura 60
kwa siku, idadi hiyo ikilinganishwa na watu 24,000,000 wanaokusudiwa
kuandikishwa kwa BVR 7,750 nchi nzima, shughuli hiyo itachukua siku 52,
wakati siku zilizosalia hadi Kura ya Maoni ni 36.
Jambo jingine linalofanya hesabu hizo
kukataa ni kitendo cha mashine hizo 7,750 za BVR zilizokusudiwa,
kutokuwapo zote nchini hadi sasa, licha ya NEC kusema mara kwa mara
kwamba zitawasili wakati wowote.
Jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva alisema hata awamu ya kwanza ya mashine 3,100 za BVR bado ziko njiani.
Iwapo mashine hizo pekee zitafika na
kutumika kuandikisha wapigakura hao milioni 24 zitahitajika siku 97
kukamilisha shughuli hiyo.
Mchakato huo ulianza kusuasua tangu
wakati majaribio yaliyotumia BVR 250 katika majimbo ya Kilombero,
Morogoro; Kawe, Dar es Salaam na Milele mkoani Katavi na baadaye katika
Mji wa Makambako na mkoa mzima wa Njombe.
Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi
umebaini kuwa mashine hizo 250 zimekuwa hazitumiki zote kwa kuwa baadhi
zinatumika kutoa mafunzo kwa waandikishaji watakaofanya kazi hiyo nchi
nzima.
tiko
tiko
Post a Comment