tiko
tiko
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeelezea wasiwasi wake kuwa kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa huenda isifanyike mwezi ujao
kutokana na kusuasua kwa uandikishwaji wapiga kura katika daftari la kudumu lawapigakura mkoani Njombe.
Akizungumza
na waandishi wa habari, jana mjini Njombe, Mwenyekiti wa Nec, Jaji
Damian Lubuva, alisema kuwa upigaji wa kura hiyo huenda usifanyike
Aprili 30, mwaka huu na badala yake utasogezwa mbele kupisha kukamilisha
kazi ya uandikishaji wananchi katika daftari la kudumu la wapigakura
kwa kutumia mfumo wa kielekroniki (BVR).
Wakati
Mwenyekiti huyo akisema hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema
serikali imekwishaipatia Nec, asilimia 70 ya fedha zote za BVR
zinazohitajika na kwamba kinachotakiwa sasa ni kuandikisha wapigakura,
kazi ambayo itafanyika kwa ufanisi pindi vifaa vyote 8000
vitakapowasili.
Jaji
Lubuva alisema kuwa daftari hilo ni moja kati ya hatua za kufikia kura
hiyo ya maoni ya Katiba mpya na kuwa kura haitafanyika kama uboreshaji
wa daftari hilo halitakamilika nchi nzima.
“Vitu
hivi vinakwenda kwa kufuatana kikikamilika kimoja kinafuata kingine,
hatutapiga kura ya maoni kama hautakamilika uboreshaji wa daftari la
kudumu la wapigakura kwa mfumo wa BVR mkoani hapa,” alisema Jaji Lubuva.
Mwenyekiti
huyo alisema licha ya msimamo wa serikali kuwa kura ya maoni ifanyike
Aprili 30, mwaka huu, lakini kwa mwenendo wa uandikishaji wapigakura
italazimika kusogezwa mbele.
“Ndugu
waandishi mwendo wa daftari la kudumu na nyinyi mnauona, hivyo tutatoa
siku ya kupigia kura ya maoni kulingana na tutakavyoona mwelekeo wa
uandikishaji, lakini siwezi kusema sasa kuwa imeahirishwa mpaka lini,” alisisitiza.
Alisema uandikishwaji wananchi mkoani Njombe utaendelea hadi Aprili 15, mwaka huu.
Kauli hiyo ni tofauti na iliyotolewa na Nec wakati uandikishaji unaendelea kuwa mkoani humo, utakamilika Aprili 12, mwaka huu.
Jaji
Lubuva alisema BVR kits 7,750 zipo njiani na baada ya kuwasili
zitatumika nchi nzima na ratiba itawekwa wazi na kwamba kwa mkoa wa
Njombe zinatumika 250.
Pinda
wakati akizindua uandikishwaji wa daftari la kudumu la mpigakura,
Februari 23, mwaka huu, katika halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani
Njombe, alisema vitambulisho vinavyoandikishwa vitatumika katika kupiga
kura ya maoni ya katiba hiyo.
Mara
kwa mara Rais Jakaya Kikwete alikaririwa na vyombo vya habari akisema
kuwa kura ya maoni kwa Katiba inayopendekezwa itafanyika Aprili 30,
mwaka huu.
Tangu
kuanza uandikishaji wa majaribio katika majimbo matatu ya Kawe,
Kilombero na Mlele, Desemba mwaka jana, na Februari 23, mwaka huu,
mkoani Njombe, kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya mashine
kushindwa kufanya kazi kwa muda wote, kutosoma vidole vyenye ngozi
ngumu na uchache wa vifaa.
Baada
ya uandikishaji wa majaribio, Nec ilitangaza kuanza na mikoa mitatu ya
Mtwara, Njombe na Ruvuma, lakini hadi sasa uandikishaji unafanyika kwa
Njombe pekee na hadi sasa haujakamilika.
Jaji
Lubuva amekuwa akiwaeleza waandishi wa habari kuwa BVR kits 7,750 zipo
njiani na zitawasili wakati wowote kwa kuwa serikali imetoa asilimia 50
ya fedha.
Wadau
wa uchaguzi ambao ni vyama 22 vya siasa, vilivyokutana na Nec Februari
12, mwaka huu, waliitaka kuweka wazi ratiba ya uandikishaji, mzabuni wa
vifaa, kiasi cha fedha kinachotakiwa na wapiga kura wanaokadiriwa
kuandikishwa kila kata.
Licha
ya maswali ya wadau hao, majibu ya Nec yamekuwa ni kuwa wanaamini
uandikishaji utamalizika kabla ya Aprili 30, mwaka huu, ili daftari hilo
litumike katika kura hiyo na uchaguzi mkuu.
Hali
iko hivyo, huku zikiwa zimebaki siku 26, ukitoa siku za Jumapili na
sikukuu , ambazo uandikishaji haufanyiki, kufika siku ya kura ya maoni
kama ilivyotangazwa na serikali.
Hali ilivyo Njombe
Machi
22, mwaka huu, wakati uandikishaji ulipokamilika katika mji wa Njombe,
baadhi ya wananchi hawakuandikishwa kutokana na nyongeza ya siku moja
kutotosheleza kutokana na uchache wa vifaa.
Mkazi
wa Njombe, Freddy Kifasi, ameomba kuongezwa kwa muda zaidi kwa kuwa
alifika kituoni siku ya mwisho lakini hakufanikiwa kutokana na utaratibu
uliopo kumtaka kuandikisha jina siku ya Jumapili na kwenda kuandikishwa
Jumatatu, utaratibu ambao alidai hakuufahamu.
Msimamizi
wa uchaguzi katika mji huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa mji wa Njombe,
Venance Msungu, alisema hakuna nyongeza ya muda na kuwataka wananchi
kuwa na subra hadi nec itakapotangaza nyongeza ya muda.
Pinda: Serikali imejipanga
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, amesema serikali imejipanga kuhakikisha uboreshaji
wa daftari la wapigakura kwa mfumo BVR, unafanikiwa hivyo kila kata
itapelekewa seti mbili au tatu ya vifaa hivyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana,
alisema hadi mwezi ujao, uandikishaji utakuwa umeanza nchi nzima.
Hata hivyo, Pinda hakueleza ni lini vifaa hivyo vitawasili nchini kwa kuwa wanaosimamia jambo hilo ni Nec yenyewe.
“Uandikishaji
kule Njombe umekwenda vizuri na tumejifunza kwamba maeneo ya mijini BVR
ziwe nyingi tofauti na vijijini kwa sababu presha haikuwa kubwa
vijijini kama mjini. Kwa sasa tunaona kila Kata tukiandikisha kwa siku
saba na tukawa tumepeleka BVR mbili au tatu, zoezi litakwenda vizuri,” alisema.
Kuhusu
kamati za kampeni kuhusu Katiba inayopendekezwa ambazo zinapaswa kuanza
kazi Aprili Mosi, Pinda alisema jambo hilo linashughulikiwa na Nec,
lakini serikali imejipanga kuhakikisha kura ya maoni inafanyika Aprili
30, kama ilivyopangwa.
tiko
tiko

Post a Comment