tiko
tiko
MWANAMKE mmoja
aliyetambuliwa kwa jina la Doreen John Mlemba, mwenyeji wa Same mkoani
Kilimanjaro, mwishoni mwa mwaka uliopita alikamatwa kwa kuhusishwa na
shehena ya madawa ya kulevya aina ya Heroin, yenye thamani ya shilingi
bilioni 2.5.
Madawa hayo yalikutwa kwenye nyumba moja
iliyopo eneo la Ununio, Tegeta jijini Dar es Salaam, ambayo ni mali ya
Mbunge wa CCM (Jina linahifadhiwa) wa jimbo moja la mikoa ya Kanda ya
Ziwa, Uwazi limefukunyua.
Taarifa toka vyanzo mbalimbali makini,
zinasema majirani wa nyumba hiyo walikuwa na mashaka na kinachofanyika
ndani ya nyumba hiyo, kwani licha ya ukubwa na kukamilika kwa ujenzi
wake, lakini haikuwa ikikaliwa na mtu na mara chache, watu walionekana
wakiingia na kutoka bila kujulikana walichokuwa wakikifanya.
Kutokana na hali hiyo ya wasiwasi,
wasamaria wema walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambalo liliifanyia
kazi habari hiyo na kufika kwenye nyumba hiyo na kujaribu kugonga lakini
bila mafanikio yoyote.
“Baada ya kugonga, ndipo polisi hao
walipoamua kuvunja mlango na kufanya upekuzi katika sehemu zote ndani ya
nyumba hiyo, ambapo walifanikiwa kulikuta sanduku ambalo baada ya
kufunguliwa, zikagundulika kilo 35 za madawa ya kulevya aina ya Heroin,”
kilisema chanzo chetu kilichoshuhudia zoezi hilo.
Kamanda wa Kikosi Cha Kupambana na
Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, SACP Godfrey Nzowa alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa baada ya kukamata shehena hiyo,
vijana wake walijikuta katika wakati mgumu wa kumjua mmiliki wa nyumba
hiyo.
Baada ya kutafuta nyaraka mbalimbali,
hatimaye waligundua kuwa nyumba hiyo inamilikiwa na mbunge huyo wa
zamani ambaye alitafutwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa, ambapo alikiri
kuimiliki, lakini akidai kwa muda huo, alikuwa ameipangisha kwa watu
aliowataja, bila kujua shughuli iliyokuwa ikifanyika ndani yake.
Inadaiwa kuwa baada ya kupata
ushirikiano huo kutoka kwa mbunge huyo, askari waliingia mtaani kuwasaka
wapangaji hao, ambapo Septemba 15, mwaka jana, saa saba mchana,
walifanikiwa kumkamata Doreen, akiwa shambani kwake, eneo la Ruaha
Mbuyuni mkoani Iringa alikokuwa akivuna vitunguu, bamia na bilinganya.
“Tulifanya uchunguzi na tayari watu
watano wameshakamatwa akiwemo Doreen, nyumba hiyo waliifanya kama ghala
la kuhifadhia madawa na mtu mmoja bado tunaendelea kumsaka, baadhi ya
waliokamatwa tulikuwa tukiwasaka kwa muda mrefu,” alisema Kamanda Nzowa.
Aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano
wao na kuwaomba waendelee hivyo na kwamba donge nono litatolewa kwa
watakaofanya hivyo huku majina yao yakihifadhiwa.Gazeti hili lilimfikia
Mbunge huyo mmiliki wa nyumba kwa njia ya simu, lakini alikataa
kulizungumzia suala hilo, akidai liko chini ya polisi.
“Naomba suala hili umuulize Kamanda
Nzowa, mimi siwezi kulizungumzia kwa vile lipo chini ya uchunguzi wao,
pamoja na kwamba nawatambua hao wapangaji lakini siwezi kusema lolote,”
alisema.
tiko
tiko
Post a Comment