Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

SHINYANGA MJINI HUDUMA MBOVU ZA KIJAMII BADO NI TATIZO

tiko tiko
Na Conges Mramba Shinyanga
Shinyanga Mjini ni moja kati ya wilaya nane zinazounda Mkoa wa Shinyanga. Shinyanga Mjini imepakana na Mkoa wa Mwanza upande wa Kaskazini, Mashariki kuna Wilaya ya Kishapu na Magharibi kuna Wilaya ya Kahama. Pia ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Stephen Masele kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mheshimiwa Stephen Masele.
Wiki iliyopita, Uwazi lilifunga safari mpaka kwenye jimbo hilo na kuzungumza na wananchi wa kata mbalimbali zikiwemo  Chamaguha, Ibinzamata, Kambarage, Kitangili, Kolandoto na nyinginezo ambapo walieleza matatizo mbalimbali yanayowakabili.
MATATIZO YA WANANCHI
Katika ziara hiyo, Uwazi lilibaini matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi wa jimbo hilo, kubwa ikiwa ni uduni wa huduma za kijamii zikiwemo huduma za afya, uhaba wa maji safi na salama, uhaba wa madarasa na vifaa vya kujifunzia, ukosefu wa madawa katika hospitali, miundombinu mibovu na upungufu wa walimu na maabara kwenye shule za sekondari.
“Huduma za afya katika hospitali yetu ni za mashaka na usipokuwa makini unaweza kufa, unaenda hospitalini unapimwa tu halafu unaambiwa dawa ukanunue madukani, hata kama una bima ya afya haisaidii chochote,” alisema Rozina Maduhu, mkazi wa Shinyanga Mjini.
“Shuleni kwa kweli tunasoma kwa tabu sana, hakuna madawati ya kutosha, walimu hasa wa masomo ya sayansi hakuna yaani ni shida kwelikweli, ndiyo maana tunafeli,” alisema Anastazia Kamwela mwanafunzi wa shule moja ya sekondari jimboni humo.
“Yaani huku kwetu barabara nzuri ni hii inayoenda Mwanza tu, ukiingia huko ndanindani hali ni mbaya sana hasa mvua zikinyesha, tunaomba mbunge wetu atimize ahadi alizotoa wakati akiomba kura,” alisema Bright Mgeja, dereva wa bodaboda.
Tatizo lingine ambalo Uwazi lililibaini ni ukosefu wa ajira hasa kwa vijana. Fulgence Mafuru, mkazi wa Kolandoto alisema: “Kero yetu sisi vijana ni ukosefu wa ajira. Tunajua ajira hakuna serikalini lakini tunapotaka kujiajiri, tunakwamishwa na miundombinu mibovu ya barabara na ukosefu wa mitaji.
Baada ya kusikia kero hizo, Uwazi lilimtafuta mheshimiwa Masele ambapo mwandishi wetu alifika mpaka ofisini kwake na kumkosa huku namba zake zote alizoorodhesha kwenye mtandao wa Bunge la Jamhuri ya Muungano zikiwa hazipatikani hewani. Juhudi za kumtafuta zinaendelea ili ajibu kero za wananchi wake.
-GPL
tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top