tiko
tiko
Mapya
yanazidi kuibuliwa juu ya sakata linaloiandama Kampuni ya Reli Limited
(TRL) ya uingizaji mabehewa feki nchini, sasa ikifahamika kuwa hata
Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), haikushirikishwa kwenye
manunuzi hayo.
Kufichuka
kwa ukweli huo, ndiko sasa kunaongeza hali ya wasiwasi ndani ya TRL na
kuna uwezekano mkubwa sakata hilo litaibua mjadala katika mkutano wa 19
wa Bunge unaotarajiwa kuanza kesho mjini Dodoma.
Ukweli
huo uliwekwa wazi mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luaga Mpina, wakati wa kikao
cha kamati yake na PPRA.
Mpina alitoboa siri hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao baina ya kamati yake na PPRA.
Alisema
kamati yake iliwahoji PPRA kuhusu ushiriki wao kwenye ununuzi wa
mabehewa hayo na kubaini kuwa mamlaka hiyo haikushirikishwa.
“Tunashangaa
kwamba hata PPRA hawakushirikishwa kwenye mchakato wa ununuzi wa
mabehewa hayo. Hadi sasa ninapozungumza hawajawahi kuitwa kushuhudia
mabehewa 150 yaliyobainika kuwa ni feki,” alisema Mpina.
Mpina
ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa, alisema hali hiyo inaonyesha mambo
kufanywa kinyume cha taratibu katika mchakato mzima wa ununuzi wa
mabehewa hayo, hali aliyosema imechangia kuingiza hasara serikali kwa
kununua mabehewa feki.
Ili
kulishughulikia suala hilo sawa sawa, mbunge huyo alisema kamati yake
inatarajia kukutana na uongozi wa PPRA chini ya mkurugenzi wake, Laurent
Shirima Ijumaa wiki hii mjini Dodoma, kwa ajili ya kupata taarifa zaidi
kuhusu ununuzi wa mabehewa hayo feki.
Wakati
huo huo, kamati iliyoudwa na aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison
Mwakyembe, imewasilisha taarifa ya uchunguzi wake kwa Bodi ya
Wakurugenzi wa TRL kama walivyoagizwa na Waziri wa sasa wa Uchukuzi,
Samuel Sitta, ambaye anatarajiwa kukabidhiwa ripoti hiyo leo.
Mabehewa
hayo yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan
Engineering and Industrial Limited ya India ikishirikiana na kampuni
moja nchini inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja jina kwa sasa
linasitiriwa. Mfanyabiashara huyo amekuwa akijihusisha na biashara
nyingi za kulaghai mashirika ya umma na kujipatia ukwasi wa kupindukia.
Waziri
Sitta ambaye alichukua hatua ya kusimamisha uingizaji wa mabehewa
mengine 124 yaliyosalia hadi hapo atakapopata taarifa ya uchunguzi ya
mabehewa ya awali ambayo yamebainika kuwa feki, amekwisha kuweka wazi
kwamba hatakuwa na simile kwa yeyote atakayehusika na kadhia hiyo hata
kama ana madaraka makubwa kiasi gani.
Mabehewa hayo yaligundulika kuwa mabovu baada ya kufanyiwa majaribio baadhi yalianguka kwa kukosa ‘stability’ yakiwa relini.
Habari
za ndani ya TRL zinasema kuwa, mabehewa hayo yaliyopokelewa na Dk.
Mwakyembe Julai 24, mwaka jana, hayakupitiwa na jopo la mafundi wa TRL
ili kuthibitisha ubora wake.
Ingawa
Dk. Mwakyembe amekuwa akijiweka mbali na sakata hilo na kueleza kuwa
alijua tatizo mapema ndiyo maana akaagiza kamati ichunguze, hataweka
wazi ilikuwaje kwenda kuyapokea kwa mbwembwe wakati hakuwa na ripoti
kamili ya ubora wake na ufuataji wa sheria ya manunuzi katika kutoa
kandarasi hiyo kwa kampuni ya India kwa kushirikiana na mfanyabiashara
huyo.
Dk.
Mwakyembe aliyapokea mabehewa hayo kwa bashasha, huku akieleza kuwa
ununuzi wake ni utekelezaji wa mpango wa serikali wa ‘Matokeo Makubwa
Sasa (BRN)”, ambao umelenga kuhakikisha reli inahimili usafirishaji wa
abiria na mizigo nchini.
Menejimenti ya TRL imetajwa kwa nyakati mbalimbali na vyanzo vyetu ndani ya TRL kuwa na mikono katika kashfa hiyo.
tiko
tiko

Post a Comment