tiko
tiko
Lakini hebu mpe huo ukubwa uone. Hapo
ndipo utakapotambua uhalisia wake, kwa sababu utajua jinsi gani alivyo
na utu, jeuri, tamaa, mzinzi, busara, fisadi na kila jambo. Kifupi,
madaraka yanayoambatana na mamlaka ya kuamua hukupa picha halisi ya mtu.
Na kwa namna ambayo hukutegemea, mtu
ambaye ulimuona mwingi wa busara, unaweza kujikuta ukishangazwa na
ukatili wake, kama ambavyo mtu uliyeamini ni wa ovyo, anavyoweza
kukushangaza kwa maamuzi na matendo yake yenye hekima na weledi
uliotukuka.
Mimi ni miongoni mwa watu, nadhani
wengi, walioshangazwa sana na uteuzi wa Paul Makonda, kuwa Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wakati Rais Kikwete
alipofanya uteuzi wake, unaodhaniwa kuwa wa mwisho wa wakuu wa wilaya.
Nilishangazwa kwa sababu kubwa mbili.
Kwanza ni udogo wake kwa umri, ambao una tofauti kubwa na majukumu
mazito anayokwenda kukabiliana nayo. Maana haipendezi mtoto mdogo
akapewa jambo lililostahili mtu mzima, asije akaleta mambo ya disko
wakati watu wanahitaji hekima.
Jambo la pili lililonifanya nishangazwe
na JK kumpa dhamana kubwa kama ile, ni kile ambacho binafsi hukiamini
kuwa Makonda hana busara. Kwa jinsi ambavyo amekuwa akitoa maneno
kumhusu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa hayaonyeshi kama ni kijana
aliyekulia kwenye utamaduni wa kuheshimu wakubwa, kwani licha ya mbunge
huyo wa Monduli kumzidi sana umri, pia kwa wadhifa wake, anastahili
heshima, hasa kutoka kwa chipukizi wa chama chake, akiwemo Makonda.
Lakini kitu kimoja tu alichokifanya,
kimenifanya nione afadhali ya akina Makonda kumi wangepewa Ukuu wa Mikoa
wangekuwa na msaada kwa watu, kuliko waheshimiwa wengi wanaoishi kwa
kudhani wako peponi na kusahau kabisa maisha halisi ya Watanzania.
Mwanzoni mwa wiki hii, Makonda alitoa
agizo (kazi ipo katika utekelezaji wake) kwamba polisi wanapaswa kuwekwa
katika hospitali mbili za Palestina iliyopo Sinza na Mwananyamala, zote
katika Wilaya ya Kinondoni, ili kutoa unafuu kwa wananchi kupata Hati
ya Matibabu (PF3).
Nadhani suala hili limechelewa mno na
kwa kiasi kikubwa, linachangia sana kuwepo kwa vifo ambavyo vingeweza
kuzuilika. Mtu amepigwa kisu na vibaka nje ya hospitali, ameporwa kila
kitu na damu nyingi zinamtoka, lakini sheria zinataka kabla ya kutibiwa,
lazima kwanza apate fomu ya matibabu kutoka polisi!
Kama ni lazima kwa matakwa haya ya
sheria kutimizwa, kwa nini kusiwe na utaratibu wa kuwaweka polisi katika
hospitali zote ili kuwanusuru watu wanaoshambuliwa na wezi, majambazi
au wanaopata ajali?
Chukulia mfano wa mtu aliyeshambuliwa na
vibaka, amepigwa, ameporwa na hana kitu, anatokea msamaria, badala ya
kukimbizwa hospitalini, anapelekwa kwanza polisi, ambako nako kuna
urasimu wa kupitiliza.
Mtu anayevuja damu anaweza kukaa kituo
cha polisi zaidi hata ya nusu saa pasipo kuhudumiwa na anapoanza
kuulizwa maswali, saa nzima inaweza kupita kabla ya kupewa PF3 na
kuondoka. Kwa majeruhi, saa moja ni muda mrefu sana wa kuvuja damu.
Kwa hiyo wakati ninatoa pongezi za dhati
kwa Makonda kwa agizo lake lenye akili, ninawataka watu wazima wengi
walioshika nafasi za umma kuwa na wepesi wa utambuzi kama huu, wa
kuelewa nini hasa watu wanahitaji na kwa wakati gani.Nimuombe Rais
Kikwete kulipokea suala hili kwa umakini mkubwa na asimamie utekelezaji
wake kwa faida ya Watanzania wenye kero nyingi.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment