tiko
tiko
BONDIA
nyota wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka aliyehukumiwa kifungo
cha miaka mitatu jela pamoja na faini ya shilingi milioni moja, hapo
Februari 2 mwaka huu mjini Morogoro, amebadilishiwa adhabu hiyo na
badala yake atatumikia kifungo cha nje.
Cheka alihukumiwa kwa kosa la kumpiga na kumsababishia maumivu makali,
meneja wa baa yake ya Vijana Social Hall iliyopo mjini Morogoro, aitwaye
Bahati Kibanda, hapo Julai 2 mwaka jana katika eneo la Sabasaba.
Bondia
Francis Cheka akiongea na wanahabari baada ya kumchakaza Thomas Mashali
tarehe 1 Mei, 2013 katika ukumbi wa PTA jijini Dar Es Salaam. (Picha na
Maktaba).
Cheka anayeshikilia mkanda wa WBF alipandishwa Kizimbani katika Mahakama
ya Hakimu Mkazi mkoa wa Morogoro, kwa shitaka hilo lililosomeka kuwa ni
la shambulio la kudhuru mwili na kujeruhi.
Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya mkoa wa Morogoro Said Msuya,
aliyesikiliza shauri hilo, alikubaliana na ushahidi uliotolewa na upande
wa mashtaka na kuthibitisha shitaka hilo.
Pamoja na Cheka kupewa nafasi ya kujitetea, bondia huyo hakutoa maelezo
yoyote na kuiachia mahakama hiyo kutoa adhabu inayostahili kwa bondia
huyo aliyejizolea sifa kemkem katika ngumi za kulipwa nchini.
Hata hivyo, taarifa kutoka Morogoro zinasema kuwa Cheka ameachiwa kutoka
katika gereza la Manispaa ya Morogoro, mchana wa leo na kwamba sasa
atatumikia kifungo cha nje, sambamba na kumlipa fidia ya shilingi
milioni moja meneja wake huyo wa zamani.
Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, Cheka atatakiwa kuripoti katika
gereza la Manispaa ya Morogoro kila wiki, hatakiwi kutoka nje ya
Manispaa ya mkoa bila kibali maalum cha Gereza na kwamba kwa muda wote
huo, atatakiwa kutofanya kosa lolote la jinai, vinginevyo adhabu yake
itarejeshwa au kuongezwa.
Kocha wake wa muda mrefu, Abdalah Komando akiwa na wanafamilia ya bondia
huyo mjini Morogoro, wamethibitisha kuachiwa kwa mpiganaji huyo, baada
ya kukaa gerezani kwa muda wa siku 44.
Habari kutoka mji kasoro bahari zinasema kuwa kulikuwa na shamra shamra
kubwa nyumbani kwa bondia huyo, mtaa wa Kilimahewa kwani ndugu, jamaa na
marafiki walifurika kwa wingi kumpa pole na pongezi bondia huyo asiye
na mpinzani kwa sasa nchini.
Mwandishi wa mtandao huu ambaye alifika nyumbani kwa bondia huyo na
kukutana naye wakati akitoka kuoga, alisema baada ya kusalimiana naye
kama rafiki, kocha wake alimuomba kumuacha mwanandondi huyo ili apate
mapumziko kwa siku nzima ya leo.
Kocha wake huyo, Komando, alisema Cheka bado akili yake haijakaa sawa,
hivyo ni vyema kama ataachwa kwa leo ili apumzike, lakini
akawahakikishia wanahabari kuwa watapata fursa ya kuzungumza naye mambo
mbalimbali kesho.
tiko
tiko
Post a Comment