tiko
tiko
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu.
Matukio
ya kuvamia, kupora silaha na kuua askari katika vituo vya polisi
yameelezwa na Jeshi la Polisi kuwa huenda wahalifu wanafundishwa na
makundi ya kigaidi yanayofanya uhalifu katika baadhi ya nchi za Afrika
kama vile kundi la Boko Haram.
Mkuu
wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, akizungumza katika mahojiano
maalum jana jijini Dar es Salaam, alisema kila siku jeshi hilo limekuwa
likijitahidi kupambana na mauaji, wizi na ujambazi, lakini bado matukio
hayo yanaendelea kutokea nchini.
IGP
Mangu alisema kinachofanywa hivi sasa na Jeshi la Polisi ni kubadilisha
mbinu za kiulinzi na kuachana na za kizamani kwa sababu jeshi hilo
halikuwahi kufikiria kama kuna siku vituo vya polisi vitavamiwa kama
inavyotokea sasa na hivyo imekuwa ni changamoto kubwa na mpya kwa jeshi
hilo.
“Uhalifu
ni kama upepo ukitokea kwa jirani hapo hakuna namna ya kuzuia huo upepo
usijekutupuliza na sisi, cha msingi baada kupulizwa mnashtuka namna
gani mtapambana nao kama mtaweza kubadilika mbinu au mtaendelea kubakia
katika utendaji kazi wenu na mambo ya zamani,” alisema.
Alisema
suala la kwamba majambazi wamekuwa na nguvu kuzidi jeshi hilo na ndiyo
maana matukio haya yanatokea siyo la kweli, kwa sababu dunia sasa
inabadilika na matukio ya kupora silaha na kuua askari yamekuwa
yakitokea hata katika nchi jirani kama Kenya.
“Haya
matukio yanatokea hata kwa jirani zetu kama Kenya, askari
wananyang’anywa silaha, kundi kama la Boko Haram wanavamia vituo vya
polisi na kupora silaha, kwa hiyo lazima tutambue kuwa Tanzania siyo
kisiwa, hao wahalifu waliopo huko inawezekana wakawa wanafundisha na
hawa kwetu kufanya uhalifu hapa nchini,” alisema.
Alisema
jambo la msingi ni kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi
kuwafichua wahalifu ili hatua zichukuliwe dhidi yao na Tanzania iendelee
kuwa nchi ya amani.
Katika
kipindi cha kuanzia Januari mwaka huu kumetokea matukio mfululizo ya
uvamizi wa vituo vya polisi ambavyo vinaporwa silaha, kuua na kujeruhi
askari, hali ambayo imeleta hofu kwa wananchi kuhusu hatma ya usalama
wao hasa katika kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu.
Tukio
kubwa lililotikisa ni lile lililotokea mwezi uliopita baada ya watu 10,
wanadhaniwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za jadi na za moto
walipokiteka kituo cha polisi Ikwiriri kilichopo tarafa ya Ikwiriri,
wilayani Rufiji, mkoani Pwani na kuwaua askari wawili, kupora silaha
saba na kisha kulipua bomu kituoni hapo.
Kamanda
wa polisi Mkoa wa Pwani, Urich Matei, aliwataja askari waliouawa katika
tukio hilo kuwa ni PC Judith Timoth na Koplo Edgar Mlinga.
Alisema
katika tukio hilo majambazi hao ambao hadi sasa hawajakamatwa wala
silaha walizopora hazijapatikana, baada ya kukivamia kituo hicho
walifanikiwa kuiba silaha aina ya SMG (Sub Machine Gun) mbili, SAR
mbili, Shortgun moja na bunduki mbili za kulipulia mabomu ya machozi.
Siku
chache baada ya tukio hilo, watu wengine wanaosadikiwa kuwa majambazi
waliwavamia askari polisi wawili waliokuwa doria Mjini Tanga na kuwapora
bunduki mbili aina ya SMG kisha kumjeruhi kwa kumchona kisu mmoja wao.
UVAMIZI MGETA
Tukio
lingine ni la mkoani Morogoro, Wilaya ya Kilombero, ambako watu
wanaodhaniwa kuwa majambazi walivamia kituo kidogo cha polisi Mgeta na
kupora SMG moja na magazine moja yenye risasi 30.
Katika
tukio hilo, wavamizi hao walipora vitu mbalimbali ambavyo ni vielelezo
vya ushahidi kwenye kesi inayomkabili mtuhumiwa Emmanuel Shewele (21).
UVAMIZI MKAMBA
Matukio
mengine yalitokea Juni 11, mwaka jana baada ya watu wasiojulikana
walipokivamia kituo kidogo cha polisi Mkamba mkoani Pwani na kusababisha
kifo cha askari mmoja na mgambo.
Askari
aliyefariki ni mwenye namba D 9889 koplo Joseph Ngonyani ambaye alifia
katika hospitali ya wilaya ya Mkuranga wakati akitibiwa kutokana na
kumkatakata na mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
Katika
tukio hilo, askari mgambo Venance Francis naye alifariki wakati
akitibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) huku askari
Mariamu Mkamba aliyejeruhiwa akipatiwa matibabu na kupona.
Majambazi
hayo katika tukio hilo walipora silaha aina ya Shortugun tatu, Sub
Mashine Gun (SMG) mbili na magazine 30 kila moja ambazo zilikuwa kwenye
ghala la muda zikisubili kupelekwa kwenye kituo kikubwa penye ghala kuu
la silaha.
UVAMIZI USHIROMBO
Tukio
jingine la kuvamiwa kituo cha polisi lilitokea Septemba mwaka jana
katika kituo kikuu cha polisi wilayani Bukombe mkoani Geita ambako
askari wawili waliuawa na kujeruhi wengine watatu. na bunduki 10
kuporwa.
Mbali
na kupora SMG 10, pia inadaiwa walifanikiwa kupora risasi ambazo idadi
yake haikutambulika mara moja pamoja na mabomu ya kutupa kwa mkono na
kutokomea kusikojulikana.
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Geita, Joseph Konyo aliwataja askari waliouawa kuwa
ni WP 7106 Uria Mwandiga na G. 2615 PC Dustani Kimati na waliojeruhiwa
askari namba E.5831 CPL David Ngupama Mwalugelwa aliyejeruhiwa kichwa na
usoni huku akiumizwa mdomo na meno mawili kungooka pamoja na Mohamed
Hassan Kilomo amabye alijeruhiwa kifuani na mguu wa kulia kwa risasi.
tiko
tiko
Post a Comment