tiko
tiko
Dar/Tanga. Ni
dhahiri kwamba sasa hali si shwari nchini kutokana na mfululizo wa
matukio ya uhalifu ikiwamo kuvamiwa vituo vya polisi, kuuawa kwa polisi
na jingine kubwa la juzi la mapigano baina ya polisi wakisaidiwa na
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) dhidi ya makundi yanayodhaniwa kuwa
ni ya ama ujambazi au kigaidi.
Matukio hayo
yanayoliweka Taifa katika wasiwasi zaidi hasa wakati huu wa kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, yamekuwa gumzo kila kona ya nchi kutokana na
utata wake.
Katika mfululizo
wa matukio hayo, juzi risasi zilirindima mkoani Tanga kwa zaidi ya saa
48 wakati Polisi na askari wa JWTZ waliposhirikiana kupambana na
wahalifu hao.
Katika mapambano hayo, askari mmoja wa JWTZ alipoteza maisha na wapiganaji wengine zaidi ya sita kujeruhiwa.
Jana, askari hao
waliendelea na operesheni ya kuwasaka watuhumiwa na hadi tunakwenda
mitamboni hakukuwa na taarifa zozote za kukamatwa kwao.
Mbali na
kutokamatwa watu hao ambao hawajajulikana ni wahalifu wa aina gani, pia
silaha zilizokuwa zinasakwa hazikukutwa kwenye Mapango ya Amboni kama
ilivyokuwa ikihisiwa, zaidi ya pikipiki moja mbovu na baiskeli tatu.
Habari zilizopatikana jana zimedokeza kuwa vikosi vilivyopo katika
operesheni hiyo vimebadili mbinu za kuwasaka majambazi hao.
Vilevile, wakazi
wa kitongoji cha Karasha Amboni ambao walihama kukimbia mapigano, hadi
jana walikuwa hawajarejea majumbani mwao.
Kwa upande wa
majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo, wanaendelea na
matibabu huku madaktari na wauguzi wakitakiwa kutoa taarifa za kila
anayefikishwa hapo akiwa majeruhi.
“Tumepewa
maelekezo kwamba kila raia anayefikishwa hapa akiwa na majeraha tutoe
taarifa haraka kwa uongozi kwani kuna uwezekano wa kuletwa waliofanya
mashambulizi kwenye mapango,” alisema mmoja wa wauguzi kwa sharti la
kutotajwa jina.
Wakazi wa Kijiji
cha Kiomoni kilicho jirani na mapango ya Amboni, walisema baadhi ya
vyombo vya habari vimekuwa vikipotosha taarifa juu ya eneo yalikofanyika
mapambano, kwamba ni mapango ambayo hutembelewa na watalii na wageni
wengine, wakati si kweli.
“Katika eneo la
Amboni kuna jumla ya mapango 13 yaliyogunduliwa lakini yanayotumika ni
mawili, kwa hiyo kunakoendeshwa mapambano ni pango la mbali kabisa na
sehemu inayotembelewa na wageni,” alisema Hussein ambaye hufanya kazi ya
kupiga picha katika eneo hilo.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Tanga, Frasser Kashai alisema jeshi hilo lisingeweza
kuzungumza na vyombo vya habari jana kwa sababu hakukuwa na mtu yeyote
aliyekamatwa na operesheni ilikuwa inaendelea. “Sisi sote tuko huku
kwenye operesheni na Kamishna (Paul Chagonja wa Operesheni na Mafunzo)
hataweza kuzungumza na waandishi wa habari leo (jana) kwa sababu taarifa
ni zilezile za jana (juzi),” alisema Kamanda Kashai.
Kaimu Kamanda wa
Makosa ya Jinai nchini, DCI Diwani Athumani alisema matukio ya uhalifu
yanayotokea nchini ni mapya na yanayochochewa na ukuaji wa teknolojia ya
habari na mawasiliano.
“Haya ni mambo
mapya kwa hapa nchini, lakini ninachoweza kusema ni kuwa, hawa ni
wahalifu na ni wachache kiasi kwamba nina uhakika Jeshi la Polisi lina
uwezo wa kuwadhibiti,” alisema.
Akizungumzia
hali hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mathias Chikawe alisema
polisi wanafahamu kuwa kuna hali ya hatari na wameshaongeza ulinzi
katika maeneo yote.
“Sisi
tunafahamu, ndiyo maana askari wetu tumeshawaambia kuwa sasa hakuna
kuning’iniza silaha begani… sasa silaha iwe mkononi wakati wowote kwa
mapambano,” alisema Waziri Chikawe na kuongeza kuwa juhudi zaidi
zinaendelea kufanyika ili kulinda usalama wa raia na kuifanya Tanzania
ibaki kuwa kisiwa cha amani.
“Umakini
unaendelea, tunahimiza doria na ninakuhakikishia tunapambana nao,”
alisema Waziri Chikawe huku akisisitiza kuwa ni uhalifu wa kawaida.
Wakati Chikawe
akisema hayo, kumekuwapo na taarifa katika vyombo vya habari na
wachambuzi wa masuala ya kiusalama zikihusisha uhalifu huo na matukio ya
kigaidi yenye lengo la ama kulipiza kisasi cha polisi kupambana na
uhalifu au kuteka silaha za kufanyia uhalifu.
Jana, Kamishna
wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alikaririwa akisema mapigano
hayo yalifanyika katika msako wa majambazi walioiba silaha kwenye kituo
cha polisi mkoani Tanga.
Mwili wa askari
wa JWTZ, Said Kajembe aliyefariki dunia katika Hospitali ya Bombo baada
ya kujeruhiwa katika mapambano hayo uliagwa jana katika kikosi cha JWTZ
Pande na baadaye kusafirishwa kwenda kijijini kwake, Kwashemshi, Korogwe
kwa mazishi.
Kaimu DCI Diwani
alisema uvamizi huo wakati mwingine husababishwa na wahalifu kutaka
kulipiza kisasi kwa polisi hali ambayo alisema inatishia usalama wa nchi
kwa ujumla. “Wapo watu wamewekeza kwenye uhalifu, sasa wanapoona polisi
wamefanya kazi yao wanaamua kuwaharibia kwa kulipiza kisasi. Kwa
kawaida, mhalifu hapendi polisi lakini hawa hawaangalii mbali kuwa
vitendo vyao vinaweza kusababisha majanga zaidi ya haya,” alisema.
Aliwataka
Watanzania kuwa na sauti moja ili kukomesha vitendo vya uhalifu
vinavyoendelea nchini ili kuirudisha Tanzania yenye amani.
“Tuwe na sauti
moja, wimbo mmoja kama Watanzania, waandishi wa habari ni wadau wakubwa
na viongozi wa dini pia watusaidie katika hili. Tunaapa kufanya kazi
usiku na mchana kupambana na hili.”
Juni mwaka jana,
majambazi wanaokisiwa kuwa sita, wakiwa na pikipiki tatu, walivamia
Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya
Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na kupora bunduki tano na risasi
60.
Polisi aliyeuawa
ni Konstebo Joseph Ngonyani na majeruhi Venance Francis na Mariamu
Mkamba ambao walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya Mkuranga kwa
matibabu.
Septemba mwaka
jana, majambazi yalivamia Kituo Kikuu cha Polisi Ushirombo, Wilaya ya
Bukombe mkoani Geita na kuua polisi wawili na kujeruhi wengine wawili na
kupora bunduki 10 ambazo hata hivyo zilipatikana zote.
Walioawa ni
G.2615 PC Dastan Kimati na WP 7106 PC Uria Mwandiga na waliojeruhiwa ni
E.5831 CPL David na H627 PC Mohamed. Majambazi hao walivamia kituoni
hapo kwa kurusha bomu la mkono.
Januari 15, watu
15 wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za kivita na mabomu ya
kurushwa kwa mkono walivamia Kituo cha Polisi Ikwiriri, Rufiji mkoani
Pwani na kuua polisi wawili na kupora silaha tano za SMG na mbili za
kufyatulia mabomu ya machozi zilizokuwapo kituo hapo na kutokomea
kusikojulikana. Katika tukio hilo, polisi wawili Koplo Edga na WP Judith
waliuawa.
Februari 3,
Kituo cha Polisi cha Mngeta, Wilaya ya Kilombero kilivamiwa na majambazi
ambao waliiba bunduki aina ya SMG yenye risasi 30.
Mbali na matukio
ya uvamizi wa vituo vya polisi, kumekuwa na matukio mengine ya uhalifu
mkubwa yanayoashiria kuwa hali nchini si shwari, likiwamo la Aprili
mwaka jana la majambazi kuvamia Benki ya Barclays, Tawi la Kinondoni,
Dar es Salaam na kupora kiasi kikubwa cha fedha.
Katika kipindi
hichohicho, majambazi saba wakiwa na silaha waliivamia Benki ya I&M
na kupora fedha zinazokadiriwa kuwa ni zaidi ya Sh150 milioni na
kutoweka.
Novemba 2013,
majambazi wanane walipora zaidi ya Sh900 milioni katika Tawi la Benki ya
Habib, Kariakoo, Dar es Salaam. Sh700 milioni na Dola za Marekani
181,885 (Sh285, 444,000).
Mji wa Geita kutekwa kwa dakika 15
Itakumbukwa kuwa
Juni mwaka jana, majambazi yaliuteka mji wa Geita kwa takribani dakika
15 na kupora fedha kwenye kampuni ya Blue Coast Inv. na kwa wakala wa
usambazaji wa bia wilayani hapo. Kadhalika, majambazi hao walimuua kwa
risasi, wakala wa huduma za fedha kwa njia ya simu.
Pia, kumekuwapo
na matukio kadhaa ya utekaji mabasi. Januari 20, zaidi ya watu 40
waliteka mabasi sita ya abiria yanayofanya safari kati ya Jiji la Arusha
na Nairobi, Kenya.
Katibu Mkuu wa
Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis
Mataka aliwataka wananchi kutekeleza majukumu yao badala ya kuwaachia
polisi.
“Vyombo vya
kisheria na polisi havina watu wa kutosha. Wananchi wanatakiwa kuilinda
amani iliyopo. Hili si jukumu la polisi peke yao. Kama tungekuwa na moyo
wa kutoa taarifa ya mienendo ya shaka, ingekuwa rahisi kutatua matatizo
kwa haraka. Ni muhimu kurudisha ari ya kushirikiana na vyombo vya
usalama.”
Mchungaji John
Mbata wa Kanisa la Njia ya Yesu, Mbagala alisema hashangazwi na matukio
hayo kwani ni dalili ya siku za mwisho... “zamani vituo vya polisi
viliogopewa hata kwa kupita tu, leo ndivyo vinavamiwa, hii ni hatari.”
Alisema hayo yote ni matokeo ya kumuacha Mungu, hivyo Taifa halina budi kuomba ili uchaguzi ujao uwe na amani.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment