tiko
tiko
LICHA ya Mamlaka
ya Chakula, Dawa na Vipodozi (TFDA) kufuta usajili na kupiga marufuku
uuzaji wa dawa duni, zenye madhara na zisizofaa kwa matumizi ya
binadamu, dawa hizo zimegundulika kuuzwa holela na baadhi ya wamiliki wa
maduka ya dawa katika kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani Mwanza.
Hayo yameelezwa
jana na wakazi wa Kisesa wilayani hapa, wakati wa semina ya siku moja
iliyojadili visababishi vya ulemavu katika jamii, ambapo walisema
madhara ya ulemavu yanatokana na watu kutumia dawa zilizopita muda wake.
Semina hiyo
ilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 50 kutoka katika makundi ya walemavu
wa kutoona, viungo, kutosikia, uono hafifu, ngozi na watendaji wa vijiji
na vitongoji, iliyoandaliwa na asasi ya watu wenye ulemavu ya SANJO na
kufadhiliwa na Shirika la the Foundation for Civil Society.
Dawa
zilizofutiwa usajili na TFDA ni dawa ya kutibu fungus ( ya vidonge na
kapsuli) aina ya Ketoconazole, dawa za kutibu mafua na kikohozi za maji,
vidonge na kapsuli zenye kiambato hai aina ya phenylpropanol amine na
dawa ya kuua bakteria ya sindano, aina ya Chloramphenicol Sodium
Succinate.
Zingine ni dawa
ya kuua bakteria ya maji na kapsuli aina ya cloxacillin, malaria ya
vidonge yenye mchanganyiko wa Sulphadoxine na Pyrimethamine(SP) na dawa
aina ya Amikacin, Levofloxacin.
Watoa huduma pia
waliagizwa kusimamia mabadiliko ya matumizi ya dawa aina ya SP ili
ziweze kutumika kwa wajawazito tu na dawa aina ya kanamycin, amikacin na
Levofloxacin zitumike kwa wagonjwa wa kifua kikuu tu kwenye hospitali,
vituo vya afya na zahanati.
Akizungumza
katika semina hiyo, mkazi wa Kisesa, Romanus Kalista alisema licha ya
Serikali kupitia TFDA kubaini kuwepo kwa dawa duni kwa watumiaji na
kufuta usajili wake kwa matumizi ya binadamu, anaona hali hiyo
imewachanganya wananchi kutokana na ukweli wananchi wengi kabla ya
kufutiwa usajili, walikuwa wakizitumia.
“Hata hivyo dawa
hizo zilizopigwa marufuku bado zinatumika hapa Kisesa na TFDA bado
haijatoa elimu ya kutosha kwa wananchi, na kibaya ni kwamba dawa hizi
bado zinauzwa kwenye maduka ya dawa,” alisema. Agnes Mathias ambaye ni
mkazi wa Kisesa na ambaye alikiri kuwa aliwahi kufanya kazi ya kuuza
dawa katika duka la dawa, aliitaka Serikali itoe elimu zaidi kwa umma.
“Bado dawa
zilizopigwa marufuku zinauzwa huku kwetu, mimi nilikuwa muuzaji najua
mbinu zinazotumika kuuza dawa, wauzaji wanauza kwa kufungua mlango
kidogo, ningeomba serikali ingetuma wataalam waje kufanya ukaguzi
vinginevyo madhara yatakuwa makubwa”, alionya.
Akizungumza kwa
njia ya simu kutoka mkoani Iringa, Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa,
Moses Mbamba alisema wamiliki wa dawa wanaouza dawa hizo zilizofutiwa
usajili, wanajali zaidi kutafuta pesa kwa gharama ya maisha ya watu
kuliko kujali uhai wa binadamu. Alisema ofisi yake itafanya ukaguzi wa
haraka katika eneo hilo.
“Kesho
nitamuagiza msaidizi wangu aende huko mara moja kufanya ukaguzi na
watakaobainika tutawafikisha mahakamani mara moja, hatutakubali wao
kuendelea kuuza dawa zilizofutiwa usajili,” aliahidi.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment