tiko
tiko
Walimu Jiji la Mbeya, wakiwa wamezuiwa na FFU ili wasiendelee kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya.
WALIMU wa shule za Msingi na Sekondari
katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wapatao 113, juzi waliandamana
kuelekea ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji hilo kwa ajili ya kudai haki zao
mbalimbali.
Maandamano hayo ya amani, yalianzia
katika ofisi kuu ya Jengo la CWT Mkoa wa Mbeya majira ya saa 5;27
asubuhi, kabla hayajazuiwa na kikosi cha askari wa kutuliza ghasia
mkoani hapa saa 5;33 mpaka saa 5;39 na kuwaomba warejee ofisini kwao
kutokana na hali ya vurugu iliyokuwa imelizingira Jiji hilo jana.
“Tunawaomba mrudi ofisini kwenu na sisi
tutaenda kumleta Mkurugenzi wa Jiji, kwasababu hata mkijaribu kwenda
muda huu hamtaweza kuonana naye, ulinzi umeimarishwa sana kutokana na
mgomo wa wafanyabiashara wa soko la Soweto ambao wamegoma na wanataka
kuandamana” alisikika mmoja wa askari mwenye nyota tatu, akiwasihi
walimu hao.
Wakizungumza na waandishi wa habari,
walimu hao walisema kuwa, walifikia uamuzi wa kwenda kumuona mwajiri wao
kutokana na madai mbalimbali yakiwemo malimbikizo ya mishahara yao
tangu mwaka 2007.
“Mwalimu unaingia darasani ukiwa na
mawazo ya fedha zako huku ukiangalia dawati la mwanafunzi limechoka.
Serikali inajisikia raha kuona mwalimu anaenda na biashara ya ubuyu
shuleni! Mimi nadai zaidi ya Milioni Nne tangu mwaka 2007 sijalipwa na
fedha tunaambiwa zimekuja zinafanya kazi zingine”alisema Mwalimu Stella
Robson.
Mwalimu Lucas Mahenge, ambaye ni mlemavu
wa macho, alisema kuwa yeye madai yake ni suala la kupandishwa madaraja
bila kupandishwa mshahara, hali ambayo alisema inamkatisha tamaa na
serikali isifikie mahala ikawafikirisha walimu kuanza kuwafundisha
watoto kuwa 2+2=22.
“Serikali kama imeshindwa kutulipa madai
yetu, ituambie ili tuweze kumwomba mfanyabiashara, Rwegemalil” alisema
Mwalimu Gunza Mwasomola.
Katibu wa Chama cha walimu Jiji la
Mbeya, Mwalimu Felix Mnyanyi, alisema kuwa kwa kushirikiana na viongozi
wenzake, wamefuatilia kwa muda mrefu madai hayo na kufanya uhakiki
lakini utekelezaji wake umekuwa siyo wa kuridhisha.
“Walimu wamefika hapa wakiwa na madai
zaidi ya matatu, ambayo ni malimbikizo ya mishahara tangu mwaka 2007,
ambapo ni wilaya pekee nchini walimu hawajalipwa, madai ya fedha za
likizo, kupanda na kushushwa madaraja baada ya kujiendeleza kitaaluma na
walimu wastaafu kutolipwa” alisema Mwalimu Mnyanyi.
Alisema kuwa baada ya kuzuiwa na
kuwaelewa askari polisi kuwa wasifike katika ofisi ya mwajiri wao ambaye
ni Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, kutokana na hali ilivyokuwa ya utata wa
usalama wao na watu wengine, walirejea ofisini hapo na kuendelea
kumsubiri mwajiri huyo chini ya ulinzi wa polisi, hali ambayo mpaka
majira ya saa saba mchana, walimu waliendelea kuwepo katika ofisi yao na
Mkurugenzi hakuweza kufika kwa wakati huo mpaka tunaenda mitamboni.
Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Mussa
Zungiza, alikiri kuwepo madai ya walimu katika ofisi yake na kwamba
madeni hayo hayatawezwa kumalizwa kwa siku moja kutokana na walimu
kutofautiana muda wa kuanza likizo na kumaliza.
Alwaambia walimu kuwa atashughulikia madai yao kwa kushirikiana na uongozi wao wa CWT.
tiko
tiko
Post a Comment