tiko
tiko
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
WAZIRI
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameitaka Bodi mpya ya
Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuliongoza shirika hilo kwa ufanisi na
kuhakikisha kuwa mteja mpya anapoomba umeme anafungiwa ndani ya wiki
moja.
Pia
waziri huyo ameitaka bodi hiyo kuhakikisha kuwa shirika hilo
linajitegemea na hivyo kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini.
Akizindua
bodi hiyo mwishoni mwa wiki, Profesa Muhongo alielezea kukerwa na suala
la wananchi kufungiwa umeme ndani ya siku 30 mara wanapopeleka maombi
hayo Tanesco na hivyo kuiagiza bodi hiyo kulishughulikia suala hilo ili
siku hizo zipungue.
“Bodi
simamieni maombi ya kufungiwa umeme ambayo sasa yanaelezwa
kushughulikiwa ndani ya siku 30, hii lazima ibadilike, Watanzania lazima
wapewe umeme ndani ya wiki, zaidi ya hapo haikubaliki. “EWURA (Mamlaka
ya Udhibiti wa Nishati na Maji) waelezwe kuhusu suala hili ili kuona
namna ya kupunguza hizi siku, sababu wao wanahusika katika suala la
upangaji wa siku husika,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Akizungumzia
haja ya Tanesco kujitegemea kifedha, alisema kwa kipindi kirefu,
serikali imekuwa inatoa fedha nyingi kuisaidia kutekeleza miradi katika
maeneo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Hivyo
alitaka bodi hiyo kuonesha jinsi itakavyolibadilisha Shirika ili
misaada kutoka serikalini ipungue na ifike mahala shirika hilo
lijitegemee.
Kuhusu
madeni ambayo Tanesco inadai kutoka kwa Taasisi za Umma, binafsi na
watu binafsi, Waziri Muhongo aliiagiza Bodi hiyo kulisimamia suala hilo
na kuja na mkakati utakaoliwezesha shirika hilo kukusanya madeni hayo.
Alisema
lengo la Serikali ni kuona shirika hilo linakusanya madeni kutoka kwa
wadeni wake wakubwa na wadogo ili Shirika hilo nalo liweze kulipa madeni
linalodaiwa na wadau wake.
Aidha,
Profesa Muhongo ameiagiza bodi hiyo mpya kuhakikisha kuwa shirika hilo
linashirikiana na sekta binafsi katika miradi yake ya uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji umeme ili kufanikisha lengo la serikali la
kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.
Alieleza
kuwa, kulingana na sera zilizopo, uendelezaji wa sekta ya umeme,
unahitaji ushirikishwaji wa sekta binafsi kwa kuwa uwekezaji katika
sekta hiyo unahitaji kiasi kikubwa cha fedha za kigeni, kiwango ambacho
kinahitaji ushirikiano na sekta hizo.
Alisema
Tanesco inapaswa kuonesha nia thabiti ya kuunga mkono juhudi za
serikali za kukamilisha majadiliano na wawekezaji na waendelezaji wa
miradi bila kuwakatisha tamaa.
Awali,
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Stephen Masele aliieleza bodi hiyo
kwamba serikali ina imani kuwa uzoefu na weledi wa Mwenyekiti na wajumbe
wa bodi hiyo utasaidia katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya
nishati ili sekta hiyo muhimu ichangie katika kuipeleka nchi kwenye
uchumi wa kati.
Naibu
waziri huyo aliwaasa wajumbe hao kuhakikisha kuwa taaluma walizonazo
wanazitumia katika kuliboresha shirika hilo. Naye Mwenyekiti wa Bodi
hiyo Dk Mighanda Manyahi alisema majukumu waliyokabidhiwa ya kuisimamia
Tanesco ni makubwa, lakini kwa kutumia taaluma zao watahakikisha
wanayatimiza ili kuhakikisha nchi inakuwa na umeme wa uhakika kwa kuwa
nchi ina rasilimali za kutosha zinazowezesha kutimiza malengo hayo.
Mwenyekiti
huyo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco anaongoza wajumbe nane ambao ni
Kissa Vivian Kilindu, Juma Mkobya, Dk Haji Semboja, Shaaban Kayungilo,
Dk Mutesigwa Maingu, Boniface Muhegi, Felix Kibodya na Dk Nyamajeje
Weggoro.
tiko
tiko
Post a Comment