tiko
tiko
Mjumbe
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za mitaa (LAAC) za Mitaa,
Kangi Lugola akizungumza wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika
Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mjumbe mwenzake, Omari Nundu.
Licha
ya Bunge kuazimia kuwa wenyeviti wa kamati zake waliotajwa kuhusika
kwenye kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow wavuliwe nyadhifa zao, hali
imekuwa tofauti katika vikao vya kamati hizo vilivyoanza jana baada ya
baadhi yao kuongoza vikao hivyo. Jana, Kamati Kuu ya CCM imeamua
viongozi hao, Andrew Chenge, William Ngeleja Na Profesa Anna Tibaijuka
wafikishwe Kamati ya Maadili ya chama.
Awali,
walitakiwa kuachia ngazi na kamati zao katika mabano ni Ngeleja
(Katiba, Sheria na Utawala), Chenge (Bajeti) na Victor Mwambalaswa
(Nishati na Madini).
Kikao
cha 16 na 17 cha Bunge kiliazimia kuwa kamati husika za kudumu za Bunge
zichukue hatua za haraka na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa 18 wa
Bunge unaoanza Januari 27, kuwavua nyadhifa zao wenyeviti tajwa wa
kamati husika.
Hata hivyo, jana, Ngeleja alisema anaendelea na madaraka yake, kwa kuwa hatua iliyopo sasa ni ya uchunguzi.
“Mimi
naendelea na kazi zangu kama mwenyekiti wa kamati, najua uchunguzi wa
suala hili bado unaendelea, baada ya hapo ikithibitika ndipo Bunge
litachukua uamuzi nami sitakuwa na budi kutekeleza,” alisema Ngeleja.
Aliongeza: “Ingawa ninajua kuna shinikizo kwa baadhi ya watu kwa sababu wanazozijua wao hawapendi kutuona katika nafasi hizi.”
Kwa
upande wake, Chenge alisema: “Sikuwahi kutangaza kujiondoa katika
nafasi hii ya uenyekiti. Nimeshangaa taarifa zilizotolewa katika baadhi
ya vyombo vya habari.”
Alisema
tuhuma zinazomkabili hazimuumizi kichwa kwa sababu hazina ukweli,
“Dhamira hainiumi kwa sababu siwezi kushiriki kuiba fedha za wananchi.
Mimi ni kama tumbili hata hapa nitaruka.”
Makamu
mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Festus Limbu alisema suala la Chenge
linasubiri uamuzi utakaotolewa na Spika wa Bunge, Anne Makinda. “Kamati
imeamua kwa busara Chenge akae pembeni na makamu mwenyekiti aongoze
vikao huku ikisubiri hatua atakazozichukua Spika (Makinda)...lakini siyo
taarifa kwamba Chenge kajiuzulu, siyo kweli.”
“Unajua
suala hili unaweza kusema bado ni bichi, Chenge ni mwenyekiti mteule wa
Spika, lakini wenyeviti wengine wanachaguliwa na wajumbe wa kamati zao,
labda Spika hajaona wa kumteua au anataka kuiachia kamati ifanye
uchaguzi, hili litategemea na yeye,” alisema Limbu ambaye ni Mbunge wa
Magu (CCM)
Kuhusu
wafadhili wa maendeleo ambao kamati hiyo ilikutana nao jana alisema
wametoa asilimia 50 ya Dola 558 milioni ambazo wahisani hao waliahidi.
Kikao
cha Kamati ya Nishati na Madini kiliongozwa na Makamu mwenyekiti wake,
Jerome Bwanausi ambaye alilithibitishia gazeti hili kwamba hawakufanya
uchaguzi wowote.
Alipotafutwa kwa simu Mwabalaswa na kutakiwa kuzungumzia hatima yake, alijibu kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwenye simu.
Mkurugenzi
wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Suala halipo
kikanuni, bali ni maagizo yaliyotolewa na Bunge kwa hiyo mwenye nafasi
nzuri ya kulizungumzia ni Spika.”
Hata
hivyo, habari zilizopatikana jana usiku ndani ya Kamati Kuu ya CCM
zilieleza kuwa, Ngeleja, Chenge pamoja na Profesa Tibaijuka suala lao
imeachiwa Kamati ya Maadili ya CCM chini ya mwenyekiti wake, Philip
Mangula.
LAAC yalishukia jiji
Katika
hatua nyingine, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),
imeitaka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo itoe taarifa za
kueleweka kuhusu uuzaji wa hisa zake na mikataba kwa Kampuni ya Simon
Group. Uamuzi huo umekuja baada ya Mkurugenzi wa jiji hilo, Wilson Kabwe
na Meya, Dk Didas Masaburi kujichanganya wakati wakijibu maswali ya
uuzaji wa hisa hizo kwa kampuni hiyo ambayo inamiliki Shirika la Usafiri
Dar es Salaam (UDA).
Mwenyekiti
wa LAAC, Rajab Mbarouk Mohammed alitoa maazimio hayo baada ya kuibuka
mvutano kati ya wajumbe wa kamati hiyo na Dk Masaburi na Kabwe kuhusu
uuzwaji wa hisa hizo ambazo ni asilimia 21.
Mvutano
uliibuka baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola kueleza kuwa mmiliki
wa Simons Group, Robert Kisena alitaka kununua hisa hizo, lakini jiji
lilikataa.
Kwa
upande wake, Kabwe alikiri kuwa walikataa zisinunuliwe kwa sababu
alikuwa na shaka kama Simon Group ingeweza kulipa fedha zote kama
unavyoeleza mkataba. Hisa hizo zinauzwa kwa Sh5 bilioni.
Kitendo
cha wajumbe wa kamati hiyo kulichachamalia zaidi suala hilo ambalo
liliwagawa katika Bunge la Bajeti kinatafsiriwa kuwa ni kutaka kulipa
kisasi baada ya Dk Masaburi wakati akitoa ufafanuzi kuhusu UDA, Mei
mwaka jana katika kikao cha Bajeti, kutumia lugha ya kuudhi kwa wabunge.
Pia,
kamati ilihoji kwa nini Jiji la Dar es Salaam lisivunjwe na kuwa na
kitengo kidogo kutokana na kutokuwa na majukumu ya moja kwa moja kwa
wananchi.
Hoja
hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige kwamba kuna
haja ya kuvunjwa kwa jiji hilo na badala yake kubakiwe watu wachache
(meya, mkurugenzi na katibu muhtasi) ambao watashungulika na masuala
mtambuka.
Alisema
pia kuna haja ya kuangalia upya, sheria ambayo inaipa mamlaka
halmashauri ya jiji kukusanya ushuru wa maegesho ili kazi hiyo ifanywe
na manispaa za jiji hilo na kisha kutoa gawiwo kwa jiji.
Katika
ziara ya LAAC iliyofanya katika manispaa za jiji hilo hivi karibuni,
ilipokea malalamiko ya kutopewa fedha za maegesho kutoka jiji, jambo
linalozikwamisha kufanya shughuli za maendeleo. Manispaa zote tatu,
Ilala, Kinondoni na Temeke zinatakiwa kugawana asilimia 75 ya mapato ya
maegesho na asilimia 25 inabaki jiji.
Akijibu
hoja ya ushuru, Dk Masaburi alisema madai hayo huenda yakawa na ukweli
na kuwa tatizo lililopo ni mkataba uliokuwa umeingiwa na wakala, Nation
Park Solution (NPS).
Awali,
Mbarouk aliupa uongozi wa jiji siku 19 kuanzia leo kuhakikisha
inapeleka ripoti ya tathmini ya mali kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kutokana na kushindwa kuikamilisha kwa miaka
mitatu tangu kutolewa kwa agizo hilo.
PAC yataka uchunguzi NBC
Nayo
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imemwagiza
Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru kuteua mkaguzi binafsi kwa ajili ya
kufanya uchunguzi wa sababu za kushuka kwa mtaji wa Benki ya NBC ambayo
inadaiwa Sh22.5 bilioni na Kampuni ya Absa Group Limited ya Afrika
Kusini.
Mwenyekiti
wa PAC, Zitto Kabwe alitaja maeneo yaliyosababisha mtaji kushuka kuwa
ni mikopo iliyotolewa kwenye sekta ya usafirishaji, utekelezaji wa sera
za Benki mama ya ABCA na mfumo wa uhasibu uliotambua mapato hewa. Iwapo
Serikali itashindwa kulipa deni hilo hadi Machi mwaka huu, itapoteza
asilimia 30 ya hisa zake katika NBC na hivyo benki hiyo kuwa chini ya
Kampuni ya Absa ambayo ina asilimia 55 ya hisa za NBC.
Awali,
kampuni hiyo ilikuwa na hisa asilimia 70 za benki hiyo lakini ikauza
asilimia 15 ya hisa zake kwa Shirika la Fedha la Kimataifa.
Serikali
ilikopa kiasi hicho cha fedha ili kutekeleza agizo la Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) ambayo mwaka 2012 iliiagiza NBC kuongeza mtaji wa
biashara wenye thamani ya Sh75 bilioni, baada ya ule wa awali kushuka
kwa asilimia 12.
Baada
ya NBC kubinafsishwa mwaka 1997, Serikali ilibaki na asilimia 30 ya
hisa na Kampuni ya Absa kuchukua asilimia 70, mtaji wa NBC ulishuka kati
ya mwaka 2010 hadi 2012 baada ya benki hiyo kutoa mikopo ya magari wa
Sh55 bilioni.
Baada
ya mtaji wa NBC kushuka kwa asilimia 12, Benki Kuu Tanzania (BoT),
iliagiza wanahisa wote watatu kuongeza mtaji. Kwa kuwa Serikali haikuwa
na fedha za kuongeza katika mtaji, ilikopa Sh22.5 bilioni kwa Absa na
kuzitoa kama mtaji kwa makubaliano ya kurejesha deni hilo ndani ya miaka
miwili. Kuhusu taasisi ya mikopo ya Pride, Msajili wa Hazina alisema
baada ya ukaguzi wa CAG walibaini kuwa taasisi hiyo iliondolewa kimakosa
katika orodha ya taasisi za umma.
Alisema
kutokana na hali hiyo kuna hasara ambayo serikali imeipata na
kusisitiza kuwa watapokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa taasisi hiyo
uliofanywa na CAG na wataiwasilisha katika vikao vya Bunge vinavyoanza
Januari 27.
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Beatrice Moses.
tiko
tiko
Post a Comment