Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

JAJI MKUU AANGUA KICHEKO BAADA YA KUSIKA SWALI LA TEGETA ESCROW

tiko tiko
Jaji Mkuu, Othman Chande
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande jana aliangua kicheko baada ya kuulizwa ni lini atatoa tamko la majaji wanaotuhumiwa katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mwishoni mwa mwaka jana, Bunge liliazimia kwa kuitaka polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi kwa wote waliotajwa katika taarifa maalumu ya kamati yake ya Mashirika ya Umma (PAC), kuhusika na vitendo vyote vya kijinai, kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.
Januari 15, Jaji Chande alikaririwa akisema atalishughulikia mwenye suala linalohusu majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Eudes Ruhangisa na Aloysius Mujulizi, waliotajwa kupata mgawo wa fedha kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa IPTL, James Rugemalila.
Hata hivyo, alipoulizwa jana aliangua kicheko na kubasamu mwishoni na kisha akasema: “Jamani siwezi kulizungumzia hilo, leo jamani ninazungumzia maadhimisho ya Siku ya Sheria na Maonyesho ya Wiki ya Sheria.”
Jaji Chande alisema Mahakama haifanyi uamuzi wa kesi kwa kuangalia hali ya mtu, lakini akasema ucheleweshwaji wa kesi mbalimbali zikiwamo za ufisadi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na dawa ya kulevya unasababishwa na uchunguzi pamoja na mashahidi kutofika mahakamani kwa wakati pindi wanapohitajika.
Katika kukabiliana na hali hiyo alisema: “Mahakama imejipanga kikamilifu kuhakikisha kesi hizo zinasikilizwa mfululizo mwaka huu ili kuondokana na tatizo la mrundikano wa mashauri ya kesi za muda mrefu.”
Akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Sheria, alisema yatafanyika kuanzia kesho hadi Februari 3 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema maonyesho hayo yanalenga kutoa elimu na huduma za kisheria kwa wananchi na mgeni rasmi anatarajia kuwa Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.
Jaji Chande alisema, katika wiki hiyo itatolewa elimu kuhusu ufunguaji na uendeshaji mashauri hasa yale yenye ugumu ya mirathi, utatuzi wa mgogoro kwa njia ya suluhu mwafaka na tozo za Mahakama kulipwa kwa njia ya benki. Pia, kutakuwapo na matembezi maalumu ya kuadhimisha wiki hiyo yatakayoongozwa na Mzee Mwinyi na wiki hiyo itahitimishwa na Rais Jakaya Kikwete.
tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top