tiko
tiko
NA EVANS MAGEGE
SASA kuna kila dalili kuwa
mwangwi wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyotikisa mkutano wa 16
na 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utaendelea kusikika
kwa namna ya kuihanikiza Serikali kuwajibika zaidi.
Dalili hizi zimeonyeshwa
waziwazi na baadhi ya wabunge hususani waliokuwa vinara wa kupambana na
kashfa hiyo ambao hawajaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Rais
Jakaya Kikwete dhidi ya watendaji wa Serikali na viongozi wa kisiasa
walioguswa na ripoti ya uchunguzi wa kashfa hiyo.
Mmoja wa wabunge walio katika
mkakati huo ambao kimsingi unalenga kumng’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
ni David Kafulila wa Kigoma Kusini.
Kafulila katika mahojiano yake
na MTANZANIA Jumamosi alisema hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete
kushughulikia maazimio nane ya Bunge haziridhishi na kuongeza kuwa kabla
ya kuketi kwa mkutano wa 18 wa Bunge anapaswa kuwa amemfukuza kazi
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Alisema Waziri Muhongo ni
muhusika muhimu katika kashfa hiyo, kwa sababu alidiriki kusimama
bungeni na kulidanganya taifa kuwa fedha zilizokuwa zimehifadhiwa katika
Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwa za umma hadi uchunguzi wa vyombo vya
dola ulipothibitisha pasipo shaka kuwa ni za umma.
“Hatufanyi haya kwa lengo la
kumkomoa mtu, hapana kabisa. Sisi tuna dhamira ya dhati ya kutetea
maslahi ya taifa kwa hiyo hatuko tayari kumuona Rais akiendelea kumuacha
kiporo Waziri Muhongo.
“Rais anaonekana kusuasua
kuchukua uamuzi dhidi ya Waziri Muhongo, sasa kama itatokea akashindwa
kutengua uteuzi wake hadi Bunge lijalo tutawasilisha hoja binafsi ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu tukiwa na kusudio la kumng’oa kwenye
wadhifa wake, hiyo ndiyo njia pekee ya kumwondoa Waziri Muhongo,”
alisema Kafulila.
Alipoulizwa iwapo mkakati huo
wa kumng’oa Waziri Mkuu Pinda unaungwa mkono pia na wabunge wa CCM,
alisema hawezi kuzungumzia msimamo wa wanasiasa wengine hata hivyo,
ujasiri waliouonyesha baadhi ya wabunge wa chama hicho wakati wa mjadala
uliopitisha maazimio ya Bunge unaondoa shaka ya kupata uungwaji mkono
wa kutosha.
Mbali na Kafulila, Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge wa Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alipoulizwa
msimamo wake kuhusu jambo hilo, akiandika kwa maandishi kupitia barua
pepe alisema anaamini Serikali itatekeleza maazimio yote ya Bunge.
Ingawa tayari Katibu Mkuu
Kiongozi, Ombeni Sefue amekwishamsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kupisha uchunguzi dhidi yake kwa
kashfa ya Escrow, bado yapo mashinikizo yanayotaka hatua zaidi
zichukuliwa kwa mujibu wa maazimio nane ya Bunge.
Mbali na Katibu Mkuu Sefue,
Jaji Mkuu Othaman Chande bado yuko kimya kuhusu majaji wa Mahakama Kuu
walioguswa katika kashfa hiyo.
Awali viongozi wanaounda Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa nyakati tofauti walikaririwa na
vyombo vya habari wakitoa matamshi yenye mwelekeo wa kulishinikiza Bunge
kuiwajibisha Serikali iwapo Rais Kikwete hatatekeleza maazimio yote
nane ya Bunge.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa,
Profesa Ibrahim Lipumba, ndiye aliyekaririwa kwanza akieleza kuwa endapo
Rais Kikwete atashindwa kumwajibisha Prof. Muhongo, wabunge walio ndani
ya Ukawa watawasilisha hoja na kushawishi wengine kupiga kura ya
kutokuwa na imani na Waziri Mkuu sambamba na kuitisha maandamano nchi
nzima.
Wakati shinikizo hili likizidi
kushika kasi, Rais Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mwaka
aliendelea kusisitiza msimamo wake wa kumuweka kiporo Prof. Muhongo kwa
maelezo kuwa uchunguzi dhidi yake haujakamilika.
MTANZANIA
tiko
tiko
Post a Comment