tiko
tiko
Zikiwa
zimebaki siku tatu kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuanza mjini
Dodoma, sasa hakuna shaka kwamba Rais Jakaya Kikwete atafanya mabadiliko
katika Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia leo na kabla ya
Jumapili (saa 48) kutokana na kukabiliwa na safari ya nje.
Rais
anatarajiwa kufanya mabadiliko hayo baada ya kumwondoa Anna Tibaijuka,
ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow
baada ya kuingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye akaunti yake.
Mwingine
ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye
anatuhumiwa kutoshughulikia kwa makini sakata hilo na kusababisha
Serikali kupoteza fedha hivyo kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa kumvua
uwaziri utakaomlazimu Rais kufanya mabadiliko madogo kwenye baraza lake,
ikiwa ni miezi isiyozidi mitano kabla ya kuvunja Bunge kupisha Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Rais Kikwete anaweza kutangaza mabadiliko hayo wakati wowote kuanzia leo.
“Rais
anaondoka Jumapili kwenda Davos (Uswisi kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la
Kiuchumi la Dunia (WEF)), hivyo kwa jinsi yoyote ile ni lazima atangaze
baraza kesho (leo) au Jumamosi,” alisema mpashaji habari wetu.
“Hawezi
kutangaza baraza jipya akiwa nje ya nchi, hivyo ni lazima atangaze
kesho (leo) au ikishindikana Jumamosi ili Jumapili afanye shughuli
nyingine na kuondoka.”
Hata
hivyo, mabadiliko ya mwisho ya Baraza la Mawaziri yalitangazwa na
Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye pia anaweza kupewa kazi hiyo.
Baada
ya kujadili sakata la uchotwaji wa fedha hizo kwa takriban siku nne,
Novemba 28, mwaka jana Bunge lilifikia maazimio manane, likiwamo la
kutaka wote waliohusika kwenye kashfa hiyo wachukuliwe hatua na mamlaka
husika, akiwamo Profesa Muhongo ambaye Rais Kikwete alisema Novemba 22,
2014 kuwa amemuweka kiporo hadi baada ya “siku mbili au tatu” kusubiri
matokeo ya uchunguzi.
Hata
hivyo, shinikizo liliongezeka baada ya Kamati Kuu ya CCM, iliyokutana
Zanzibar chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete, kuitaka Serikali iwe
imetekeleza kwa vitendo maazimio yote ya Bunge kuhusu sakata hilo kabla
ya kikao cha Bunge kitakachoanza Jumanne ijayo na kutaka wahusika
walioko kwenye dhamana za uteuzi wachukuliwe hatua stahili na mamlaka
zao kuwawajibisha mara moja.
Pia,
Kamati ya Maadili ya CCM iliyokutana Dar es Salaam mapema wiki hii,
iliwajadili wanachama waliohusika kwenye kashfa hiyo na kupeleka taarifa
yake kwenye Kamati Kuu ya chama hicho kwa hatua zaidi.
Wakati
CCM ikisema hayo, wabunge wamekuwa wakimkumbusha kiongozi huyo wa
Serikali kuchukua hatua kabla ya kikao cha Bunge. Wabunge wawili wa
mkoani Arusha, Godbless Lema na Joshua Nassari wote kupitia Chadema,
wamediriki kusema kuwa watamwondoa Profesa Muhongo kwa mabavu kwenye
ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria iwapo Rais hatakuwa
amemuondoa.
Pia,
nchi wahisani zilieleza mapema mwezi huu kuwa pamoja na kuruhusu kiasi
cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, bado zinasubiri tamko la
Serikali kuhusu sakata hilo, ikiwa ni pamoja na hatua ilizochukua kuzuia
kashfa kama hiyo isitokee tena, ili Tanzania inufaike kwa misaada hiyo
ya fedha zinazotokana na walipakodi wa nchi zao.
Wapinzani
wanamlaumu Rais Kikwete kwa kuchelea kumwondoa Profesa Muhongo baada ya
kuahidi mwezi mmoja uliopita kuwa angelifanyia uamuzi suala lake katika
muda wa siku mbili au tatu tangu Desemba 22 mwaka jana.
Kuna
habari kwamba kuchelewa kutangazwa kwa mabadiliko hayo pengine
kunatokana na Rais Kikwete kusubiri ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya
Operesheni Tokomeza, ambayo habari zinasema inaweza kuwasafisha baadhi
ya mawaziri na hivyo kumpa mwanya wa kuwarejesha, hasa kutokana na muda
wa uhai wa baraza hilo kuwa mfupi, hivyo angehitaji watu ambao
ameshafanya nao kazi.
Kabla
ya kutangaza hatua alizochukua kwa mujibu wa maazimio ya Bunge, Rais
Kikwete alikatisha ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyekuwa Arabuni,
kitendo kilichotafsiriwa kuwa alitaka ushauri kuhusu mawaziri
waliohusika na hatua za kuchukua, lakini akatangaza kumvua uwaziri
Profesa Tibaijuka pekee.
Awali,
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipendekeza kuwa Waziri
Pinda naye awajibishwe kutokana na kushindwa kushughulikia suala hilo
akiwa mtendaji mkuu wa Serikali.
Aidha,
habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa Rais Kikwete pia
alitaka kutumia fursa hiyo kuwaondoa mawaziri wote waliotangaza nia ya
kugombea urais kutokana na kusakamwa kuwa wanatumia nafasi zao vibaya,
huku wakivunja taratibu za CCM.
Hata
hivyo, kutokana na ukweli kuwa Pinda ni miongoni mwa waliotangaza nia,
itakuwa vigumu kwake kumuondoa mtendaji huyo mkuu kwa kuwa itamaanisha
kuvunja Serikali.
Katika
sakata la Tegeta Escrow, zaidi ya Sh306 bilioni zilichotwa kwenye
akaunti hiyo iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ilifunguliwa
kwa pamoja na Tanesco na kampuni ya IPTL, ambayo iliingia mkataba wa
kuliuzia umeme shirika hilo la umma, baada ya pande hizo mbili kuingia
kwenye mgogoro wa viwango vya tozo na hivyo kufungua kesi mahakamani.
Kesi
hiyo iliisha kwa jaji kuamua kuwa pande hizo mbili zikokotoe upya
viwango vya tozo hiyo, lakini fedha zote zilizokuwamo kwenye akaunti
hiyo zikaondolewa mwishoni mwa mwaka jana na kulipwa kwa Kampuni ya Pan
African Power Solutions (PAP), ambayo ilinunua hisa zote za umiliki wa
IPTL.
Wakati
malipo hayo yanafanyika, kulikuwa na pingamizi la Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) ambayo ilitaka kodi ambayo Tanesco ilitakiwa ilipe,
ikatwe kwanza kabla ya IPTL kulipwa fedha zake, huku ikihoji kodi
nyingine katika ununuzi wa hisa za kampuni nyingine iliyomiliki kwa muda
hisa za IPTL ya Piperlink ulioonekana kutawaliwa na udanganyifu.
Tayari
Jaji Frederick Werema, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
ameshajiuzulu wadhifa huo, wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Wenyeviti
watatu wa kamati za Bunge, William Ngeleja, Andrew Chenge na Victor
Mwambalaswa, wamejiuzulu nyadhifa zao, ikiwa ni sehemu ya maazimio ya
Bunge. Pia kuna mlolongo wa viongozi wa umma, vigogo wa zamani wa
Serikali na watumishi wa umma walioingiziwa fedha na mmiliki wa zamani
wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila ambazo zinahusishwa na kashfa hiyo
au kutotangaza masilahi binafsi katika vikao vilivyohusu sakata hilo.
Chenge,
aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni Mbunge wa
Bariadi, aliingiziwa Sh1.6 bilioni, Ngeleja, waziri wa zamani wa Nishati
na Madini na Mbunge wa Sengerema aliingiziwa Sh40.4 milioni, wakati
Mwambalaswa ameondolewa kutokana na kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Nishati
na Madini wakati huohuo akiwa mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco
iliyotuhumiwa kushindwa kushughulikia vizuri sakata hilo.
Wakati
hayo yakiendelea, Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) imeshawafikisha mahakamani maofisa sita waandamizi wa TRA,
Tanesco na BoT kwa tuhuma za kuhusika kwa njia moja au nyingine kwenye
kashfa hiyo.
Kauli ya wasomi
Aliyekuwa
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St Augustine, Dk Charles Kitima alisema:
“Nchi lazima iundwe na Serikali imara na itakayoendeleza mikakati yake
ya maendeleo. Tunakwenda katika uchaguzi hivyo nchi inahitaji Serikali
yenye viongozi madhubuti.”
Huku
akitolea mfano Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba na Kura ya Maoni
kupitisha Katiba Mpya, Dk Kitima alisema mambo hayo yanahitaji viongozi
makini wa kuyasimamia.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema: “Nadhani mabadiliko
yanaweza kuwa makubwa kutokana na matukio yaliyopo mwaka huu. Yanaweza
kuwa ni mabadiliko ya kuhakikisha kuwa Serikali iliyopo madarakani
inaendelea kuwapo. Mabadiliko ya kuisaidia CCM kushinda.”
Aliungana
na Dk Kitima, kusisitiza kuwa sakata la escrow, Uchaguzi Mkuu na Kura
ya Maoni ni kati ya mambo yanayoweza kuchangia kufanyika kwa mabadiliko
makubwa.
Chanzo:mwananchi
tiko
tiko
Post a Comment