tiko
tiko
JESHI
la Polisi linawashikilia na kuwahoji watu 15 kwa tuhuma za kutaka
kumtorosha kutoka Hospitali ya TMJ Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima
lililopo jijini, Dar es Salaam, Joseph Gwajima aliyelazwa hapo tangu
usiku wa kuamkia juzi.
Gwajima
amelazwa ikielezwa hali yake ilibadilika wakati akihojiwa na makachero
wa Polisi waliokuwa wanamhoji baada ya kujisalimisha baada ya kutakiwa
kufanya hivyo kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama
Kardinali Polycarp Pengo.
Kukamatwa
kwa watu hao, wakiwemo wachungaji sita, mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) na mwanafunzi wa udaktari katika Chuo Kikuu cha
Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU), Dar es Salaam
kumethibitishwa na taarifa ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova.
Katika
taarifa yake, amesema watu hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kula njama
pamoja na kujaribu kumtorosha Askofu Gwajima ambaye amelazwa katika
Hospitali ya TMJ kwa matibabu.
Alisema saa tisa na nusu usiku wa kuamkia jana, watu 15 walifika hospitalini hapo kwa lengo la kumuona mgonjwa huyo.
“Askari
ambao wapo katika lindo hilo waliwatilia mashaka watu hao hivyo
waliwakatalia kuingia. Na hapo walijaribu kutumia nguvu, lakini
walikamatwa,” alisema.
Kova
alisema baada ya kuwapekua, watu hao walikutwa na begi lenye bastola
aina ya BERRETA yenye namba CAT5802 ikiwa na risasi tatu, risasi 17 za
Short gun na vitabu viwili vya hundi.
Alisema
begi hilo pia lilikuwa na hati ya kusafiria yenye jina la Gwajima
Joseph Mathias yenye namba AB 544809, kitabu cha hundi cha Benki ya
Equity, nyaraka mbalimbali za kampuni ya PUMA, chaja ya Simu na Tablets,
suti mbili na nguo za ndani.
Aliwataja
waliokamatwa ni Chitama Mwakibambo (32), fundi seremala mkazi wa Gongo
la Mboto, Mchungaji Edwin Audex (24) mkazi wa Kawe Maringo, Adam
Mwaselele (29), mhandisi na mkazi wa Kawe Maringo, Frederick Fusi (25)
mkazi wa Mbezi Beach.
Wengine
mwanafunzi wa chuo cha IMTU, Frank Minja (24) mkazi wa Mbezi Beach,
Emmanuel Ngwela (28) mkazi wa Keko juu ambaye ni mlinzi shirikishi,
Geofrey William (30), Mhadhiri UDSM mkazi wa Survey Chuo Kikuu,
Mchungaji Mathew Nyangusi (62) mkazi wa Mtoni Kijichi, mchungaji
Boniface Nyakyoma (30) mkazi wa Kitunda.
Pia
wametajwa Geofrey Andrew (31), dereva mkazi wa Kimara Baruti, Mchungaji
David Mgongolo (24) mkazi wa Ubungo Makoka, Mfanyabiashara George Msava
(45) mkazi wa Ilala Boma, Mchungaji Nicholaus Patrick (60) mkazi wa
Mbagala Mission, George Kiwia (37) ambaye ni dalali wa magari na mkazi
wa Tandale Uzuri na mchungaji Yekonia Bihagaze (39) mkazi wa Kimara Stop
Over.
Kova
alisema upelelezi wa shauri hilo unaendelea kwa madhumuni ya kubaini
sababu za njama hizo sambamba na kujua mbinu zote zilizotumika kutaka
kufanikisha jaribio la kumtorosha Askofu Gwajima.
Pengo asamehe
Wakati hayo yakiendelea, jana Pengo aliwatangazia waumini wake kumsamehe Gwajima na pia kuwataka waumini wake pia wamsamehe.
Akizungumza
katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph ambako iliendeshwa misa ya
Jumapili ya Matawi, alitoa msamaha kwa Gwajima na kusema kuwa hana chuki
na mtu yeyote.
Aidha, Pengo alisema hawezi kuingilia hatua ya Polisi kumhoji kiongozi huyo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima.
Gwajima: Niombeeni
Aidha,
katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Gwajima amewaomba waumini wake
wamuombee kwa Mungu apone haraka ili aweze kuendelea na kazi aliyotumwa
na Mungu ya kuhubiri Injili.
Taarifa
iliyotolewa na kusomwa kanisani kwake imedai kuwa kiongozi huyo
anaendelea vizuri na afya yake imeanza kuimarika. Alisema waumini wake
wamuombee kwa Mungu apone haraka ili kuendelea na kazi aliyotumwa na
Mungu ya kuhubiri injili.
Kiongozi
huyo bado amelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali
ya TMJ iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam na anaendelea kupatiwa
matibabu ya karibu na madaktari kutokana na hali yake kubadilika mara
kwa mara.
Hata
hivyo, kwa taarifa iliyotolewa na daktari anayemtibu askofu Gwajima,
Fortunatus Mazigo, alisema hali ya mgonjwa inaendelea vizuri japokuwa
alikataa kusema ni nini tatizo linalomsumbua hadi akamilishe kukusanya
taarifa ya vipimo vyote ambavyo vingine bado majibu yake hayajapatikana
na huenda kila kitu kikawa hadharani leo.
tiko
tiko
Post a Comment