tiko
tiko
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa maelekezo kwa
Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) kufanya uchunguzi wa Sh milioni
699 zinazodaiwa kutolewa na Wizara ya Nishati na Madini kwenda Shirika
la Umeme Tanzania (TANESCO) ambazo zinaonekana kuyeyuka katika mazingira
yasiyoeleweka.
Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam wakati wa Hesabu za TANESCO.
Kabwe
alisema katika ripoti ya ukaguzi wa hesabu wa shirika hilo inaonekana
wizara imetoa Sh milioni 699 kwenda Tanesco, lakini shirika hilo
limeeleza kuwa halijawahi kupokea fedha hizo, jambo ambalo linaleta
utata na kuhoji ni wapi fedha hizo zimekwenda.
“Kamati
inamtaka CAG afanye ukaguzi maalum, kwa kushirikiana na Tanesco na
Wizara na kisha ilete taarifa ni wapi fedha hizo zimekwenda,” alisema.
Awali
akitoa maelezo kuhusu fedha hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Dk
Mighanda Manyihi alisema Tanesco haijawahi kupokea fedha hizo na
kumuomba Mwenyekiti wa PAC na kamati kufanya kila linalowezekana ili
fedha hizo zipatikane kwani zitakuwa msaada kwa shirika.
“Mwenyekiti,
hizo fedha hata siye tunazihitaji sana kuna miradi mingi sana ambayo
imekwama, kama fedha hizo zikipatikana zitatufaa sana,” alisema.
Naye
Kaimu Ofisa Mkuu wa Fedha, Anetha Chengula akitolea ufafanuzi suala
hilo mbele ya Kamati alisema Tanesco haijawahi kupewa fedha hizo na
kwamba walishafuatilia hadi wizarani kwa wahasibu wa wizara na kushindwa
kutoa vielelezo kuthibitisha kutoa fedha hizo.
Katika
hatua nyingine, Kamati hiyo imeagiza Bodi ya Tanesco kuhakikisha
ifikapo Aprili 30, mwaka huu nafasi zote za ngazi ya Menejimenti kuwa
zimejazwa na hakuna tena suala la kukaimu kwani bodi ina mamlaka
kisheria kufanya hivyo.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Anetha Chengula ambaye alijitambulisha kama Kaimu
Ofisa Mkuu wa Fedha ambapo Mwenyekiti alihoji Bodi na Menejimenti kwa
nini ofisa huyo anaendelea kukaimu wakati Bodi ina mamlaka ya kuteua na
kupanga menejimenti kwa mujibu wa Sheria.
Kamati
ikitoa uamuzi kuhusu suala hilo, iliagiza Bodi kujaza nafasi zote
zilizo wazi katika menejimenti ifikapo Aprili 30 na itakapokamilisha
ipeleke taarifa kwa Katibu wa Bunge, pamoja na kuitaka bodi mpya kupitia
mikataba yote na kisha kupeleka taarifa kwa Katibu wa Bunge badala ya
kusubiri kuitwa tena katika kamati.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment