tiko
tiko
MAELEZO
BINAFSI YA MHE. ZITTO ZUBEIR KABWE, MB KUHUSU UANACHAMA WAKE KATIKA
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) NA HATMA YAKE KAMA MBUNGE
KATIKA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA.
1)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa fursa uliyonipa kutoa maelezo
yangu binafsi katika Bunge lako Tukufu leo. Ninatoa maelezo haya kwa
mujibu wa Kifungu cha 50 (1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la
Aprili, 2013 kinachosema kwamba,
“Mbunge
yeyote anaweza, kwa idhini ya Spika, kutoa maelezo binafsi Bungeni
yanayolenga kufafanua kuhusu jambo lolote linalomhusu na lililoifikia
jamii”
2)
Mheshimiwa Spika, Nilijiunga na Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza
Mwaka 2015 nikiwa na lengo kuu la kupaza sauti ya vijana kwenye masuala
yanayohusu nchi yetu na kutetea maslahi ya Watanzania hususani Wananchi
wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Mkoa wa Kigoma, na Watanzania kwa
ujumla. Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Wananchi wa Kigoma
Kaskazini walinichagua tena Mwaka 2010 kupitia tiketi ya CHADEMA.
3)
Mheshimiwa Spika, kupitia fursa ya ubunge niliyopewa na wananchi wa
Kigoma Kaskazini kwa udhamini wa CHADEMA, nimejifunza mengi hapa Bungeni
na nje ya Bunge hili. Nimeijua nchi yangu, nimejua siasa na
nimejulikana ndani na nje ya Tanzania. Muhimu zaidi ni kwamba nimepata
fursa adhimu ya kutoa mchango wangu katika kutunga sheria na sera
mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Aidha, nilipata fursa ya
kipekee kama Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati zako mbili ya kuisimamia,
kuishauri na kuiajibisha serikali.
4)
Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru sana wanachama wa CHADEMA kwa dhamana
mbalimbali walizonipa ndani ya CHADEMA. Ninawashukuru viongozi wangu na
hasa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Freeman Mbowe kwa kunilea na kuniamini
kufanya naye kazi kwa kipindi chote tangu nilipokuwa mwanafunzi Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, katika chama na hapa Bungeni. Kama ambavyo
nimesema mara nyingi, CHADEMA imenilea na kunikuza tangu nikiwa na umri
wa miaka 16 na tangu kipindi hicho nimejifunza mengi.
5)
Mheshimiwa Spika, Nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa
Kigoma Kaskazini kwa mapenzi yao na imani waliyonipa na kuniwezesha
kukalia KITI hiki ninachokalia ndani ya Bunge lako Tukufu. Nashukuru
kwamba juzi nilipata fursa ya kipekee ya kuwashukuru kwa imani
waliyonipa kuwatumikia kwa vipindi viwili mfululizo. Mola atawalipa
wananchi wa Kigoma Kaskazini kwa imani kubwa walioionyesha kwangu na
kuniwezesha kulitumikia Taifa langu kwa namna nilivyolitumikia.
6)
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa pamekuwa na msuguano wa kiuongozi
kati yangu na viongozi wangu ndani ya CHADEMA uliosababishwa na tofauti
za kimtazamo juu ya tafsiri pana ya demokrasia ndani ya chama chetu.
Hatimaye tofauti hizi zilipelekea mwezi Novemba 2013 Kamati Kuu ya
CHADEMA kunivua nafasi zangu zote za uongozi nilizokuwa nazo.
Sikuridhika na maamuzi hayo na hivyo nikaonyesha kusudio la kukata rufaa
katika Baraza Kuu la chama chetu kama taratibu za kikatiba za chama
chetu zinavyotaka. Bahati mbaya ofisi ya Katibu Mkuu haikunipa fursa
hiyo, na huo ndio ukawa msingi wa mimi kufungua kesi mahakamani kuweka
pingamizi la Kikao cha Kamati Kuu kujadili hatima ya uanachama wangu
hadi pale ofisi ya Katibu Mkuu itakaponipa fursa ya kukata rufaa katika
vikao vya chama. Yaliyotokea baada ya hapo ni historia, lakini hatimaye
Mahakama Kuu imetoa hukumu yake tarehe 10 Machi 2015. Katika hukumu hii,
nimeshindwa kwa sababu za kiufundi kwa maelezo kwamba pingamizi letu
liliwasilishwa kimakosa.
Pamoja
na kwamba hatukuridhika na mwenendo wa jinsi kesi hii ilivyoamuliwa
pamoja na maudhui ya hukumu yenyewe, ninaheshimu maamuzi ya mahakama na
sina mpango wa kukata rufaa.
7)
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kawaida na kwa mujibu wa katiba ya
chama chetu, ilitarajiwa kwamba baada ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Kamati
Kuu ingekaa na kunipa rasmi mashtaka yangu yanayohusu uanachama wangu,
mimi kuitwa kujieleza na hatimaye Kamati Kuu kutoa uamuzi wake. Hata
hivyo, mara baada ya hukumu ya Mahakama Kuu dunia nzima ilitangaziwa na
Mwanasheria wetu Mkuu, kwa niaba ya chama, kwamba mimi nimeshafukuzwa na
sio mwanachama tena wa CHADEMA. Baada ya hapo viongozi wangu wametoa
matamko mbalimbali yote yakionyesha kwamba sitakiwi tena katika chama
hiki, pamoja na kwamba hadi ninapoongea hapa leo sijawahi kukabidhiwa
barua yeyote inayonitaarifu kufukuzwa kwangu katika chama.
8)
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ni wazi kwamba
uanachama wangu wa kisiasa ndani ya CHADEMA umeshaondolewa. Ninaweza
kuendelea kupigania uanachama wangu kisheria na kwa kweli nina sababu na
misingi yote kubaki na uanachama wangu kisheria. Lakini mimi ni
mwanasiasa. Sikuja hapa bungeni kwa sababu ya kushinda kesi mahakamani.
Nilichaguliwa na wananchi wa Kigoma Kaskazini na ninatambua kwamba
huwezi kuwa mbunge bila udhamini wa chama cha siasa. Huu ndio utaratibu
wa kisheria tuliojiwekea. Kwa mujibu wa viongozi wangu katika chama ni
kwamba udhamini wa chama changu umekwishaondolewa.
9)
Mheshimiwa Spika, kutokana na maelezo ya hapo juu, ninaomba kukutaarifu
wewe na Bunge lako tukufu kwamba sina mpango wa kuendelea kupigania
uanachama wangu wa CHADEMA katika viunga vya mahakama. Kwa hiyo
ninatangaza rasmi leo kwamba taratibu za kikatiba zitakapokamilika tu
nitaachia uanachama wa CHADEMA, chama nilichokipenda sana kwa sababu ya
kuendelea kukua kwa tofauti za kiitikadi, kimtazamo na hata kibinafsi
kati yangu na viongozi katika chama changu. Nimeona kuwa kuendelea
kupigania uanachama kisheria ni kutatiza na kukwaza harakati za
mabadiliko hapa nchini katika wakati ambapo mfumo wa kisiasa unatambua
uwepo wa vyama vingi vya siasa. Kwa kuwa taratibu hizo sijui
zitakamilika lini, natumia fursa hii kuwaaga wabunge wenzangu.
10)
Mheshimiwa Spika, vyama vya siasa ni jukwaa muhimu katika ujenzi wa
demokrasia lakini havipaswi kamwe kuwa juu ya wananchi. Kwa hiyo ni
maoni yangu kwamba wakati sasa umefika wa kukomesha udola na ufalme wa
vyama vya siasa hapa nchini. Mfumo wa siasa ambao unavipa vyama vya
siasa mamlaka ya kisheria ya kukanyaga mamlaka ya wananchi haupaswi
kuendelea katika Karne ya 21 na katika nchi ambayo inaendeshwa kwa
misingi ya demokrasia ya kuheshimu wananchi. Mimi ninaondoka bungeni sio
kwa sababu wananchi wangu wa Kigoma Kaskazini walionichagua wametaka
niondoke. Siondoki kwa sababu nimeshindwa kufanya kazi zangu za ubunge.
Na kwa kweli siondoki kwa sababu wanachama wenzangu katika CHADEMA
wametaka niondoke. Ninaondoka kwa sababu mfumo wetu wa kisheria unavipa
vyama vya siasa mamlaka juu ya wananchi na wapiga kura. Ni matumaini
yangu kwamba Bunge lako tukufu halitaruhusu mfumo huu unaoruhusu vyama
vya siasa kupora mamlaka ya wananchi uendelee. Ni Bunge lako pekee lenye
uwezo wa kukomesha mfumo ambao unatukuza Parties’ Power, badala ya
People’s Power.
11)
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali kwamba vyama vya siasa ni
jukwaa. Bahati nzuri nchi yetu inafuata mfumo wa vyama vingi vya siasa
na sasa tuna vyama 22. Kwa hivyo, wananchi wanaoniunga mkono
wasisikitike kwa maamuzi yangu ya leo. Bado ninayo fursa ya kuwatumikia
kupitia jukwaa lingine ambalo nitaamua katika siku chache zijazo, na
inshala Mungu akitujalia nitarudi tena hapa Bungeni katika Bunge la 11
kwa nguvu za wananchi.
12)
Mheshimiwa Spika, kwa miaka kumi niliyotumikia hapa Bungeni, si yote
niliyoyafanya yalikuwa sahihi, yapo ambayo niliyakosea kama mwanadamu
katika kufanya kazi zangu, kwa namna yeyote ile naomba radhi Watanzania
wote kwa yote ambayo sikuyafanya kwa usahihi. Mimi ni binadamu, kiumbe
dhaifu, sijakamilika. Ni Mola peke yake aliyekamilika.
13)
Mheshimiwa Spika, siwezi kuanza maisha yangu mapya kisiasa bila ya
kulishukuru Bunge lako Tukufu. Kwanza, Bunge la Tisa chini ya Mzee
Samwel Sitta, mzee wa kasi na viwango! Bado ninakumbuka vizuri jinsi
hoja ya Buzwagi ilivyotikisa Bunge lake na hatimaye kupelekea nchi yetu
kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa sekta ya madini
(Sera mpya ya Madini na Sheria mpya ya Madini ) na hivyo kukuza mapato
ya sekta ya madini kutoka Tshs. 32 bilioni kwa mwaka mpaka Tshs. 450
bilioni kwa mwaka.
14)
Mheshimiwa Spika, ninajivunia kuwa sehemu ya Bunge la Kumi chini yako,
Mama shupavu Anna Semamba Makinda. Katika Bunge hili nimekuzwa,
nimejifunza, nimepambana, nimefurahi na nimelia ndani ya Bunge hili. Kwa
pamoja tumepigania maslahi ya wananchi wetu kwa juhudi na maarifa na
hivyo kuleta mabadiliko kadhaa. Ni katika kipindi hiki ambapo wabunge
tumekuwa na sauti. Bunge la Tisa lilijijenga likawa ‘Bunge lenye Meno’
katika kupambana na ufisadi. Bunge la Kumi limejenga ‘Bunge lenye Nguvu’
katika mfumo wa Bajeti ya nchi yetu. Kupitia Bunge hili tumeweka
misingi ya kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika nchi yetu. Na
katika siku za hivi karibuni Bunge la Kumi litakumbukwa kwa Hoja Maalumu
ya Tegeta Escrow iliyopelekea mfumo wetu wa maadili ya Viongozi kupitia
Baraza la Maadili kuanza kufanya kazi kwa namna ambayo haijawahi
kushuhudiwa katika miaka iliyopita.
15)
Mheshimiwa Spika, wajumbe wa PAC ( ambao nimeishi nao kama familia )
tumekuwa nguzo kubwa ya kujenga uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge na
wananchi. Napenda kuwashukuru kwa dhati kabisa kwa kuniunga mkono na kwa
kunipa ushirikiano kama Mwenyekiti wao. Changamoto na malezi mliyonipa
kwa miaka yote hii yamejenga Mtanzania mmoja mwenye nia ya dhati ya
kuitumikia nchi yake, muda wowote, wakati wowote na kwa namna yeyote ile
bila woga wala upendeleo. Nawashukuru kwa kujitoa kwenu kwa nchi yetu
na dhamira isiyo na mawaa ya kujenga Taifa imara zaidi. Pamoja na kwamba
ninaondoka Bungeni leo, ninaahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa
Kigoma Kaskazini na Taifa langu katika kusimamia ukweli, kutetea
demokrasia ya kweli na kupigania maendeleo ya kweli kwa mwananchi wa
kawaida bila ubaguzi wowote.
16)
Mheshimiwa Spika, Kwa viongozi na wanachama wa CHADEMA, najivunia kwa
fursa mliyonipa kuwa sehemu ya Baraza hili la Taifa ambalo leo
ninalihutubia kwa mara ya mwisho kama mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Inawezekana tusiweze kuelewana katika masuala ya uongozi, misingi na
itikadi, lakini ninaamini tunapaswa kuelewana na kukubaliana katika
dhamira kubwa ya kuijenga nchi yetu kuwa Taifa linalojitegemea na lisilo
na aina yeyote ya ubaguzi. Taifa lenye uchumi shirikishi wenye
kuzalisha ajira na kuondoa umasikini, ujinga na maradhi, yaani Taifa la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na ni matumaini yangu kuwa tutakuwa
bega kwa bega katika harakati hizi katika siku zijazo. Yaliyopita si
ndwele tugange yajayo. Nafasi hii ya kihistoria tuliyopewa haihitaji
siasa za ubinafsi na unafsi! Uzalendo wetu utapimwa kwa uwezo wetu wa
kuweka tofauti zetu binafsi pembeni kwa lengo lililo kubwa zaidi yetu.
17)
Mheshimiwa Spika, Ninawashukuru tena na tena wana Kigoma na wananchi
wote wa Tanzania ambao kwa ridhaa yao nimekaa katika viti hivi kwa miaka
takribani kumi. Ninawahakikishia kuwa changamoto nilizokumbana nazo na
ambazo zimenilazimisha leo niondoke bungeni zimechochea zaidi dhamira,
nia na sababu yangu ya kuwatumikia kwa nguvu zaidi kuliko wakati
mwingine wowote ule. Huu ni mwanzo mpya.
Mheshimiwa Spika,
Asanteni sana na Kwa herini!
tiko
tiko
Post a Comment