Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

UKOSEFU WA VYOO SHULENI ILEMELA HATARI KWA AFYA ZA WANAFUNZI NA WALIMU

tiko tiko
Mheshimiwa Highness Kiwia kupitia Chama cha Demokrasia na  Maendeleo.
Ilemela ni moja kati ya majimbo saba yanayounda Mkoa wa Mwanza ambalo linaongozwa na Mheshimiwa Highness Kiwia kupitia Chama cha Demokrasia na  Maendeleo (CHADEMA).
Wiki iliyopita, Uwazi lilitembelea Kata za Nyakato, Mecco, Buzuruga, Nyasaka, Ilemela, Kahama, Kiseke, Sangabuye, Kayenze, Bugongwa, Shibuda, Pasiansi, Kawekamo, Kitangiri, Kirumba, Nyamanoro, Ibungiro, Busweru na Nyamhongolo na kufanya mahojiano na wananchi walioeleza kero mbalimbali wanazokabiliana nazo katika maisha yao ya kila siku.
MATATIZO YA WANANCHI
Miongoni mwa matatizo yaliyobainika katika ziara hiyo ni ukosefu wa vyoo, ofisi za walimu na upungufu wa madawati katika shule nyingi za msingi za jimbo hilo. Charles Yohana ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Buzuruga ambayo imegawanywa na kuwa shule tatu ambazo ni Buzuruga A, Buzuruga B na Buzuruga C, alikuwa na haya ya kusema:
“Shule zetu hizi zina wanafunzi wengi sana lakini kuna matatizo ya vyoo na vyumba vya ofisi kwa walimu kwani hapa tunatumia madarasa kama ofisi na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili wanatumia darasa moja.
“Tatizo lingine ni ukosefu wa matundu ya vyoo ambayo hayatoshelezi ukilinganisha na idadi ya wanafunzi tulionao kwenye shule hizi kwani matundu yaliyopo yamechoka halafu ni machache, kwa kweli mazingira ni magumu kiafya kwa wanafunzi na hata sisi walimu tunaiomba serikali itusikie na iweze kutatua tatizo hili.
“Tatizo lingine lililopo katika shule za msingi ni utoro wa wanafunzi na kupata mimba jambo ambalo linasababisha kushindwa kuendelea na masomo kutokana na jamii kutokuwa na mwamko wa kusimamia watoto wao na pia hali hiyo inasababisha kupata matokeo mabovu.”
Swed Omary ni mkazi wa Kata ya Mecco iliyopo kwenye jimbo hilo ambaye aliibua kero inayowasumbua ya kutokuwa na sehemu maalum ya kutupia takataka, jambo linalosababisha takataka kusambaa maeneo mbalimbali na kuziba mitaro inayopitisha maji wakati wa mvua, pia kunakuwa na unyevunyevu mwingi ambao unaweza kusababisha magonjwa ya milipuko katika eneo hilo.
“Watu wanatupa takataka kila sehemu kwa sababu hakuna eneo la kutupa takataka jambo linalofanya kuwa na mlundikano wa uchafu unaoziba mitaro, hii ni hatari kwa afya zetu tunaweza kupata magojwa ya mlipuko, tunamuomba mbunge atutafutie eneo la dampo ili kuepukana na madhara ambayo yataweza kujitokeza.”
Charles Matiku, yeye aliibua kero nyingine ambayo ni ukosefu wa kituo cha afya katika eneo la Mecco na ukosefu wa soko unaosababishwa na baadhi ya vigogo wanaoishi katika eneo ambalo lilitengwa kwa ajili ya soko.
“Kwa kweli hapa soko ni kero kubwa sana kwani kuna eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya soko lakini kuna watu ambao wanazuia eneo hilo watu wasifanyie biashara kama ilivyopangwa kwa madai kuwa ni njia yao ya kupitisha magari kwenda nyumbani kwao.
Peter Katoto yeye alitoa kero ambayo inawasumbua katika Kata ya Buswelu ambayo ndipo zilipo ofisi za wilaya hiyo kuwa wanasumbuliwa na tatizo la ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu wa kituo cha polisi, ukosefu wa madawa na gari la kubebea wagonjwa katika kituo cha afya kilichopo kwenye eneo hilo, kutokuwa na soko linalokidhi mahitaji wa wananchi.
“Kero nyingine tunatozwa fedha nyingi wakati wa kuandikisha watoto kuanza shule ya awali kwani kila mtoto anatakiwa kulipiwa shilingi elfu 25 hadi 30, serikali iangalie hali yetu na tunamuomba mbunge wetu tuliyemchagua atatue hizi kero zetu ili tuwe na imani naye katika uchaguzi ujao.
Tatizo lingine lililoelezwa na wananchi ni malalamiko kuwa polisi wanatumia nafasi yao kuwatesa wananchi kwa kuwapiga bila makosa na kuwapora mali zao hasa nyakati za usiku.
Pia imebainika kuwa walimu wengi wa shule za msingi na sekondari hawaingii darasani kufundisha na badala yake wanafanya kazi ya kuendesha bodaboda, jambo linalosababisha wanafunzi wafeli kwenye mitihani yao.
MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kusikia kero za wananchi, Uwazi lilianza jitihada za kumtafuta mbunge ambapo mwandishi wetu alifika ofisini kwake na kumkosa kwa maelezo kwamba alikuwa Dodoma kwa shughuli za kibunge. Uwazi halikuishia hapo, lilijaribu kumpigia simu yake ya mkononi ambapo awali ilikuwa ikiita bila kupokelewa kwa siku kadhaa.
Hata alipotumiwa ujumbe, hakujibu chochote na mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni, juhudi za kumpata zilikuwa zimegonga mwamba. Uwazi linaendelea kumtafuta Mheshimiwa Kiwia ili atoe majibu ya kero zinazowakabili wananchi wa jimbo lake.

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII

tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top