tiko
tiko
KIONGOZI wa vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), waliokuwa wakiishinikiza Serikali kuwapatia ajira, George Mgoba, amelazwa katika Hospitali ya Amana, jijini Dar es Salaam, baada ya kutekwa nyara na kisha kuteswa na watu wasiojulikana.
Mgoba
ni miongoni mwa vijana waliowawakilisha wenzao zaidi ya 300 kukutana na
viongozi wa juu wa Serikali hivi karibuni, akiwemo Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, kuzungumzia kilio chao na kupinga
upendeleo wa ajira ndani ya Jeshi.
Tukio
hilo ambalo kwa kiasi kikubwa linafanana na kile alichofanyiwa
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka au Mhariri
Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda,
lilimfika Mgoba Jumatatu wiki hii saa 11:00 jioni.
Mgoba,
ambaye analindwa na vijana wenzake waliomaliza mafunzo ya JKT katika
wodi namba saba aliyolazwa, anadai kufanyiwa vitendo vya kinyama ikiwa
pamoja na kuchomwa sindano ambayo haijulikani aina ya dawa iliyokuwa
nayo.
Mpekuzi
lilifika katika Hospitali ya Amana ambako pamoja na mambo mengine,
lilifanikiwa kuzungumza na Msemaji wa vijana hao, Omary Bakari, ambaye
alisema alipokea simu saa nne siku ya Jumatatu hiyo hiyo ikimtaarifu
kuwa Mwenyekiti wao, Mgoba, amelazwa katika Hospitali ya Tumbi, iliyoko
Kibaha, mkoani Pwani.
Alisema simu hiyo aliyopigiwa na mtu aliyejitambulisha kama askari polisi pia ilimtaarifu kuwa mwenzao huyo alikuwa mahututi.
Baada
ya kupata taarifa hizo, Bakari alisema alichukua jukumu la kutoa
taarifa kwa baadhi ya vijana wenzao ambao walikutana katika Hospitali ya
Tumbi usiku huo huo.
Alisema akiwa Tumbi alipata nafasi ya kuzungumza na mgonjwa ili kufahamu kilichompata hadi kufikia hatua hiyo.
Bakari
alisema mgonjwa, huku akizungumza kwa shida, alieleza kilichomkuta
ambapo alidai kuwa siku hiyo ya Jumatatu saa 11:00 jioni, akiwa nyumbani
kwake maeneo ya Mabibo Loyola, alipigiwa simu na watu waliojitambulisha
kuwa ni vijana wenzake wa JKT.
Alisema
vijana hao walimtaka waonane eneo la Mabibo Mwisho ili wazungumze
kuhusu mipango ya maandamano ya kudai ajira yaliyokuwa yamepangwa
kufanyika tena keshokutwa, baada ya yale ya awali ya kuelekea Ikulu
kumuona Rais Jakaya Kikwete kugonga mwamba.
“Nusu
saa baada ya kupigiwa simu alifika eneo walilopanga na kukutana na watu
hao ambao walikuwa ni wanawake wawili na mwanaume mmoja, waliokuwa na
gari aina ya Noah,” alisema.
Akinukuu
maelezo ya mgonjwa, Bakari alisema baada ya kusalimiana kwa kupeana
mikono na wanawake hao, mmoja wao alimwambia ajitoe kitu katika sikio na
mara baada ya kufanya kitendo hicho alihisi mwili kupata ganzi na hivyo
kupoteza fahamu papo hapo.
Alisema
baada ya kuhakikisha amezimia inavyoonekana watu hao walimfunga kamba
mikononi na miguuni na kisha kitambaa usoni na kwenda naye
kusikojulikana.
“Baada
ya muda mchache kupita Mgoba alipata fahamu na kujikuta akiwa amefungwa
kamba pamoja na kitambaa usoni na hakujua anakopelekwa, ila alisema
wakati huo alihisi wanaingia kwenye bonde ambako walimshusha,” alisema.
Alisema walipomshusha walianza kwa kumpiga, huku wakimtaka ataje ni nani aliyemtuma kuandamana kati ya Ukawa au Lowassa?
“Aliposhindwa
kusema aliyemtuma ndipo walipombana sehemu za siri, vidole na mbavu na
kisha kumpiga mateke na baada ya kumuona ameishiwa nguvu wakamvua nguo
na kumlazimisha afanye tendo la ndoa na mmoja wa wanawake hao,” alisema.
Alisema
walipoona ameshindwa kufanya tendo hilo wakamnyoa nywele na kisha
kuanza kutafuta mshipa uliopo pembeni ya paji la uso, lakini walishindwa
kuupata na hivyo kuamua kumchoma sindano mkononi.
“Walihakikisha
hana nguvu, ndipo walisikika wakisema wamemaliza kazi, hivyo
wakamchukua na kumtupa msitu wa Mailimoja wilaya ya Kibaha Mkoa wa
Pwani.
“Akiwa
msituni alijisikia kupata fahamu, ambapo alianza kutambaa kuelekea
barabarani ambako msamaria mwema mmoja alimuona na kisha kumpeleka Kituo
cha Polisi cha Mailimoja, Kibaha,” alisema.
Alisema
Polisi wa Kibaha ndio waliochukua jukumu la kumpeleka katika Hospitali
ya Tumbi saa nne usiku, kabla ya kufanya uamuzi mwingine wa kuwasiliana
na ndugu pamoja na jamaa zake.
Kwa
mujibu wa Bakari, polisi hao baada ya kufanya mazungumzo na ndugu wa
Mgoba kwa minajili ya kumhamisha hospitali ili apatiwe matibabu zaidi,
badala yake walimpeleka katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central)
kilichopo jijini Dar es Salaam.
“Cha kushangaza huko Central walimuweka rumande na baadaye walimtaka atoe maelezo pasipo kujali hali aliyokuwa nayo,” alisema.
Alisema baadaye polisi hao walimruhusu Mgoba kuondoka na kumpatia Sh 2,000, ingawa wakati huo alikuwa akijisikia vibaya.
Inaelezwa
kuwa baada ya kuruhusiwa hakufika mbali, alidondoka na alizinduka akiwa
amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Mwandishi
wa habari hizi alishuhudia magari ya polisi (defender) matatu na basi
moja la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) yakiwa yameegeshwa katika
viunga vya hospitali hiyo.
Kitendo
hicho kililalamikiwa na vijana hao kupitia kwa Katibu wake, Linus
Steven, ambaye alisema kinatia shaka na kuonesha ubabe wakati awali
walionekana kukwepa kumhudumia mwenzao.
Alilishutumu Jeshi la Polisi kutaka kutumia tukio hilo kama la kihalifu au kuna jambo la kuvunja amani.
Mwandishi
alizungumza na mke wa Mgoba ambaye hata hivyo alikataa kutaja jina
lake, ambapo alithibitisha kuwa siku ya tukio alikuwa pamoja na mume
wake nyumbani na kwamba ilipofika saa 11:00 alimuaga anakwenda kwa
rafiki zake.
Alipotafutwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, kuzungumzia tukio hilo,
alikiri askari wake kumpokea Mgoba na kisha kumpeleka katika Hospitali
ya Tumbi baada ya kumuona kuwa yupo katika hali mbaya.
Kamanda
Matei alisema alipofikishwa katika hospitali ya Tumbi madaktari
walithibitisha kuwa hana matatizo yoyote, na hivyo kuruhusiwa.
“Polisi
wangu walimsaidia kutafuta ndugu zake na miongoni mwa waliofika ni
mmoja aliyejitambulisha kama askari polisi na mwingine Usalama wa Taifa,
aliyejitambulisha polisi alidai kuwa ni shemeji wa Mgoba, lakini yule
aliyedai usalama wa Taifa alisema ni ndugu yake kwa hiyo sisi tuliishia
hapo, hayo mengine siyafahamu, waulizwe polisi wa Dar es Salaam,” alisema Kamanda Matei.
Kwa
upande wake, Kamada wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova, alisema ofisi yake ipo katika hatua za awali za upelelezi, ingawa
kuna taarifa za kukanganya kuhusu kijana huyo.
Pamoja na hilo, Kova aliahidi kutoa taarifa kamili kuanzia leo baada ya kukamilisha upelelezi.
Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Amana, Meshack Shimwela, alisema hawezi
kuzungumzia taarifa zozote za Mgoba mpaka hapo atakapopata taarifa
kutoka kwa yeye mwenyewe au ndugu zake.
Daktari
mmoja wa hospitali ya Amana aliyezungumza na mwandishi kwa sharti la
kutotajwa jina alisema mgonjwa huyo anaweza kuhamishiwa katika Hospitali
ya Muhimbili kwa kuwa hospitali hiyo haina baadhi ya vipimo ambavyo
vinaweza kubaini kitu kilichotokea kwenye damu yake baada ya kulalamika
maumivu sehemu za siri na kudaiwa kuchomwa sindano.
Kwa
mujibu wa daktari huyo, Polisi walitaka kuchukua jukumu la kumhamishia
Muhimbili baada kumaliza dripu, lakini kumekuwa na mvutano mkubwa kati
yao na ndugu zake.
Mpaka
kufikia jana jioni, daktari huyo alisema kuwa hali ya mgonjwa huyo
ilikuwa inaimarika, huku pia wakiwa wanasubiri kumpeleka Hospitali ya
Muhimbili.
Tukio
la kutekwa kwa kijana huyo limejenga hisia kwamba huenda kuna mpango
unaandaliwa wa kummaliza nguvu kwa staili ile ile kama iliyotumika kwa
Dk. Ulimboka.
Dk
Ulimboka ambaye alikuwa akiongoza wenzake kudai haki za madaktari,
alitekwa na kufanyiwa vitendo vya kinyama Juni 27, 2012, wakati Kibanda
alifanyiwa vitendo vinavyofanana na hivyo Machi 5, 2013.
Mgoba ndiye kiongozi wa vijana zaidi ya 3,000 ambao wanaishinikiza serikali kuwapatia ajira wale wote waliopatiwa mafunzo JKT.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment