Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

HUYU NDIO TANZANIA ONE (T.O) ALIYEONGOZA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE KWA KUFANYA VIZURI TANZANIA NZIMA

tiko tiko
Mwanafunzi aliyeongoza kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha nne kitaifa mwaka jana, Nyakaho Marungu akipongezwa na mama yake Celestina Maro, nyumbani kwao Kitunda Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kutangaza matokeo ya mtihani huo. 
Ufaulu katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne umeongezeka kwa asilimia 10, chini kidogo ya viwango vya Matokeo Makubwa Sasa (BRN), lakini shule za Serikali za vipaji maalumu, kongwe na za seminari zimeendelea kuporomoka.

Nyakaho Marungu (16)
Katika matokeo hayo, Shule ya Sekondari ya Kaizirege ya mkoani Kagera, iliyoanzishwa mwaka 2010, ndiyo imekuwa kinara ikiwa ni mwendelezo wa mafanikio baada ya mwaka jana kushika nafasi hiyo lakini kwa upande wa shule zenye watahiniwa chini ya 40. Shule iliyoshika mkia ni Manolo iliyopo Tanga, mkoa ambao umetoa shule tano miongoni mwa shule zilizoshika nafasi 10 za mwisho.
Matokeo hayo ni ya kwanza tangu kuanza kutumika kwa mfumo mpya wa upangaji wa Wastani kwa Kutumia Pointi (GPA) ambao unaonyesha shule zote 10 za kwanza ni za binafsi.
Akitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde alisema waliofaulu mtihani huo ni wanafunzi 196,805 sawa na asilimia 68.33 ya watahiniwa 288,247 waliofanya mtihani huo, ikilinganishwa na 235,227, sawa na asilimia 58.25 ya waliofaulu mwaka 2013.
Dk Msonde alisema wavulana waliofaulu ni 106,960 sawa na asilimia 69.85 na wasichana ni 89,845 sawa na asilimia 66.61.
Kwa mujibu wa maelekezo ya BRN, ufaulu wa upande wa sekta ya elimu, ambayo ilipangiwa malengo tisa, ulipaswa uwe asilimia 70.
Hata hivyo, pamoja na kuwa chini kidogo ( asilimia 1.7) kufikia wastani wa ufaulu kitaifa, Msonde alisema: “Tumejitahidi kwani ni asilimia kama moja na ushee ilibaki, walimu walifanya kazi nzuri na nina imani tutaifikia.”
Alisema watahiniwa 297,365 waliandikishwa kufanya mtihani huo wakiwamo wasichana 139,400 sawa na asilimia 46.88 na wavulana 157965 sawa na asilimia 53.12. Watahiniwa wa shule walikuwa 244,902 ikilinganishwa na watahiniwa 367,163 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka 2013.
“Idadi ya watahiniwa wa shule walioandikishwa kufanya mtihani huo ilipungua kwa asilimia 33.3 ikilinganishwa na watahiniwa walioandikishwa mwaka 2013.”
“Mwaka 2012 kati ya watahiniwa 386,355 waliofanya mtihani wa kidato cha pili, watahiniwa 136,243 walirudia kidato cha pili na watahiniwa 250,112 waliendelea na kidato cha tatu ambao ndiyo waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2014,” alisema na kuongeza:
“Kati ya watahiniwa 297,365 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne 2014, watahiniwa 288,247 sawa na asilimia 96.93 walifanya mtihani na watahiniwa 9,118 sawa na asilimia 3.07 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali.”
Alisema watahiniwa wa shule, kati ya watahiniwa 244,902 waliosajiliwa watahiniwa 244,410 sawa na asilimia 98.17 walifanya mtihani ambao wasichana walikuwa ni 110,603 sawa na asilimia 98.13 na wavulana ni 129,807 sawa na asilimia 98.19. Watahiniwa 4,492 sawa na asilimia 1.83 hawakufanya mtihani.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, alisema kati ya watahiniwa 52,463 waliosajiliwa, 47,837 ambao ni sawa na asilimia 91.18, walifanya mtihani na ambao hawakufanya ni 4,626 sawa na asilimia 8.82.
Ufaulu wa masomo
Dk Msonde alisema ufaulu wa watahiniwa wa shule katika masomo ya msingi umepanda kati ya asilimia 1.28 na 11.22 ikilinganishwa na mwaka 2013.
“Ufaulu wa juu kabisa ni ule wa somo la Kiswahili na asilimia 69.66 ya watahiniwa wote wa shule waliofanya somo hili wamefaulu na ufaulu wa chini kabisa ni ule wa somo la hisabati ambalo asilimia 19.58 ya watahiniwa wote waliofanya somo hili wamefaulu.”
“Ufaulu katika masomo ya sayansi yaani fizikia, kemia na baiolojia umeendelea kuimarika kidogo kwa kulingana na ufaulu wa masomo hayo mwaka 2013,” alisema.
Katika matokeo hayo, ufaulu wa kila somo na asilimia katika mabano ni Kiswahili (69.66), kemia (56.73), Kiingereza (55.10), baiolojia (48.30), fizikia (46.71), jiografia (37.96), uraia (37.70), historia (37.41), biashara (34.29), uhasibu (42.20) na hisabati (19.58).
Matokeo yaliyozuiwa, kufutwa
Dk Msonde alisema baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 184 waliobainika kufanya udanganyifu. Kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu, 128 ni wa kujitegemea na 56 ni watahiniwa wa shule.
Alisema kati ya watahiniwa hao, 128 wanatoka vituo viwili vya Kisesa mkoani Mwanza na Ubago visiwani Zanzibar, huku wengine 56 wakitoka shule mbalimbali.
“Tumeagiza mamlaka husika kuwachukulia hatua za kinidhamu waliohusika katika vituo hivyo vya Kisesa na Ubago kwani udanganyifu uliofanyika ni karatasi moja ya kujibia mtihani imeandikwa na watu watatu tofauti jambo ambalo linaonyesha hakukuwa na umakini,” alisema.
Shule kongwe na za vipaji hoi
Shule za vipaji kama Ilboru, Mzumbe, Msalato, Kilakala, Tabora Boys, Kibaha na Tabora Girls na Shule kongwe zinazomilikiwa na Serikali kama Pugu, Zanaki, Bwiru Boys, Minaki, Azania na Jangwani, kwa mara nyingine zimeshindwa kufua dafu kwa shule za binafsi.
Katika orodha ya shule 10 bora shule binafsi zilizotamba katika matokeo hayo ni Kaizirege (Kagera), Mwanza Alliance (Mwanza), Marian Boys (Pwani), St. Francis Girls (Mbeya), Abbey (Mtwara), Feza Girls (Dar es Salaam), Canossa (Dar es Salaam), Bethel Sabs Girls (Iringa), Marian Girls (Pwani) na Feza Boys (Dar es Salaam).
Shule 10 za mwisho ni Manolo (Tanga), Chokocho (Pemba), Kwaluguru (Tanga), Relini (Dar es Salaam), Mashindei (Tanga), Njelekela Islamic Seminari (Kigoma), Vudee (Kilimanjaro), Mnazi (Tanga), Ruhembe (Morogoro) na Magoma (Tanga).
Watahiniwa 10 bora kitaifa
Dk Msonde aliwataja wanafunzi 10 bora kitaifa kuwa ni Nyakaho Marungu (Baobab), Elton Jacob (Feza Boys), Samwel Adam (Marian Boys), Fainess Mwakisimba (St. Francis Girls), Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys), Angel Mcharo (St. Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St. Francis Girls) na Mahmoud Bakili (Feza Boys).
Wasichana 10 bora kitaifa
Katika matokeo hayo mwanafunzi bora kwa wasichana ni Nyakaho Marungu (Baobab), aliyefuatiwa na Fainess Mwakisisimba (St. Francis Girls), Angel Mcharo (St. Francis Girls), Atuganile Jimmy (Canossa), Jenifa Mcharo (St. Francis Girls), Levina Ndamugoba (Msalato), Veronica Wambura (Canossa), Sifaely Mtaita (St Maris Mazinde Juu), Catherine Ritte (St. Francis Girls) na Anastazia Kabelinde (Kaizerege).
Wavulana 10 bora
Dk Msonde alimtangaza kinara kwa wavulana kuwa ni Elton Jacob (Feza Boys) akifuatiwa na Samwel Adam (Marian Boys), Mugisha Lukambuzi (Bendel Memorial), Paul Jijimya (Marian Boys), Mahmoud Bakili (Feza Boys), Amani Andrea (Moshi Technical), Mahmoud Msangi, Elias Kalembo, Haji Gonga na Kelvin Sessan wote kutoka Feza Boys.

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII

tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top