tiko
tiko
Siku chache baada ya Serikali kusema itazifutia usajili shule zitakazokaidi agizo la kuweka viwango maalumu na tofauti vya ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine, wadau wa elimu wamezungumza na kusema agizo hilo linalenga kuua ubora wa taaluma nchini.
Akizungumza
na mwandishi, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa
Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Benjamin Mkoya alisema
viwango vinavyowekwa na shule binafsi vinakubaliwa na wazazi na kuwa
kinyume chake shule hizo zitakufa kutokana na uwezekano wa kufifia ubora
wa kitaaluma.
“Viwango
vinavyoweka huwa vinakubaliwa na wazazi, na lengo la kufanya hivyo ni
kutaka shule zifanye vizuri hivyo kuweza kujiendesha, kwani mbali na
kutoa huduma, tunafanya biashara,” alisema Mkoya.
Alisema
suala la baadhi ya shule kupanga viwango vya ufaulu limekuwa
likifanyika muda mrefu na kuridhiwa na wizara husika ya elimu Julai
2013, baada ya agizo la kuifungia shule ya sekondari ya Mwilavya, Kasulu
mkoani Kigoma iliyopandisha viwango vya ufaulu hadi kufikia asilimia 45
kutokana na matakwa ya wazazi.
Mkoya
alisema suala hilo lilifika wizarani na uongozi wa TAMONGSCO kukutana
na Naibu Waziri (wakati huo akiwa ni Philipo Mulugo) ambaye alisema kama
wazazi wameridhia viwango hivyo, shule zinatakiwa kuendelea kufuata
viwango hivyo.
“Tulikutana
na uongozi wa wizara, na hapa hatumuangalii mtu aliyekuwepo ofisini
bali taasisi,” na tulizungumza hilo, na hapo walisema kama wazazi
wanaridhia viwango hivyo basi hakuna sababu ya kugombana na wapiga kura
ambao wanataka viwango vya juu,” alisema na kuongeza kuwa kwa mwaka
huu pekee wameshafanya vikao na viongozi wa Wizara ya Elimu mara mbili
kwa lengo la kuboresha sera ya elimu na suala zima la Matokeo Makubwa
Sasa (BRB).
Aidha,
Mkoya alisema Serikali imekuwa ikitoa maagizo mbalimbali yanaonekana
kulenga kudhoofisha shule zisizo za serikali, na kutolea mfano wa agizo
lililotangulia lililotolewa na TAMISEMI likizitaka shule hizo
kutosajili wanafunzi mpaka hapo shule za serikali zitakapojaa.
“Serikali
inatakiwa kutoona shule hizi kama ni ebola na kuzipiga vita, badala
yake wazione kama partner (mshirika) katika kuboresha elimu hasa katika
kufikia BRN."
Mkoya
alisema wakati umefika sasa, sekta ya elimu kuwa na taasisi huru ambayo
itasimamia elimu hapa nchini hivyo kuondoa mgongano wa kimaslahi kutoka
kwa serikali ambayo ni wamiliki wa shule na pia ndio wanaosimamia
elimu.
“Tunataka mamlaka huru kama ilivyo SUMATRA, Wizara ndio yenye shule na ndio inayosimamia elimu, hapa hapatakuwa na usawa,”alisema.
Naye
Mkurugenzi wa Huduma ya Elimu kwa Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii
(CSSC) ambayo ni Bodi ya muungano wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania (TEC) na Jumuiya ya Kikristo (CCT), Petro Pamba alisema shule
zao hazitakwepa mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu kwani unaandaa
wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
Alisema
taasisi yake yenye shule za sekondari 368 nchi zima imekuwa ikiendesha
shule kwa mifumo miwili ambayo ni shule za seminari ambayo zinalenga
kuwaandaa watumishi wa kanisa na ile ya kutoa huduma ya elimu kwa jamii.
Alisema
mfumo wa kupanga viwango vya ufaulu umekuwa ukitumika muda mrefu na
kujulikana na wizara na kwa sasa hawawezi kuukwepa kwani umekuwa
ukiwaandaa vizuri wanafunzi na uwajibikaji kwa walimu.
“Mfumo
wa kuweka viwango vya ufaulu unawafanya walimu pia wajitathmini,
ukiwaacha walimu huru basi nao wanabweteka, hivyo sisi tutaendelea na
mfumo huo kwani umekuwa ukifanyika muda mrefu na mamlaka za elimu
zinaelewa,” alisema.
Alisema
viwango vilivyopo sasa ni kati ya asilimia 40 hadi 49 na kuwa zaidi ya
asilimia 50 kwa shule za seminari ambazo zinaandaa watumishi wa kanisa.
“Huko
kwenye seminari mchujo wetu ni mkali sana kwa sababu ndio tunaowaandaa
watumishi ambao watakuwa wakihudumia jamii hivyo kutakiwa wawe vizuri
kichwani,” alisema.
Hata
hivyo, Pamba alisema taasisi yao inakamilisha mfumo mbadala wa
kuwasaidia wanafunzi wanaoelewa taratibu kwa kuwaandalia mafunzo maalumu
ili waweze kufanya vizuri mitihani ya mwisho na kuwa wale wenye alama
za chini watalazimika kurudia darasa.
Alisema
pamoja na Wizara kutaka shule kufuata Sera ya Elimu inayotaka viwango
vya ufaulu kuwa ni asilimia 30, alisema sera hiyo inaelekeza kwa
wanafunzi wanapotakiwa kuvuka kutoka kidato cha pili kwenda cha tatu na
si katika madarasa mengine.
Alisema
pia kiwango hicho cha ufaulu ni cha chini ukilinganisha na mfumo mpya
wa upangaji wa alama za ufaulu unaofanywa na Baraza la Mitihani Tanzania
(NECTA) ambayo ufaulu ni kati ya alama 40 hadi 49 (C), huku alama 30
hadi 39 ni ufaulu hafifu ambao unatoa daraja D.
Alisema
kutokana na alama hizo kupitwa na wakati, CSSC, imepeleka pendekezo
wizarani kutaka kubadilishwa kwa viwango vya ufaulu hadi kufikia alama
40 kwa kidato cha pili kwenda cha tatu.
Alipoulizwa Katibu wa Elimu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mohammed Jongo alisema: ”Wizara ndio wasajili wa shule hapa nchini hivyo tutatekeleza agizo lao.”
Kwa
nyakati tofauti wakijibu maswali bungeni, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake Anne Kilango Malecela
walisema serikali itazifutia usajili shule zote za serikali au binafsi,
zitakazobainika kukaidi agizo la kuacha kuweka viwango maalumu na
tofauti za ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine.
Waraka
wa Elimu Namba 6 wa mwaka 2011, umetoa maelekezo kuhusu wastani wa
ufaulu katika mtihani wa kidato cha pili ambapo kiwango cha alama ya
ufaulu ni asilimia 30 tu na si vinginevyo kwa shule za serikali na
binafsi.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment