Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

Wilaya ya Bagamoyo taabani kielimu

tiko tiko

Ufaulu kwa wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari ni changamoto ambayo haijapatiwa majibu licha ya kwamba sababu kama ukosefu wa vyoo, upungufu wa walimu, madawati, umbali wa shule na mahali mwanafunzi anapoishi zimetajwa.


Mashirika mbalimbali yamekuwa yakifanya utafiti kujua ni kwanini wanafunzi hawafaulu kwa kiwango kinachotakiwa hasa kwa shule za msingi moja ya asasi hizo ni Naramatisho Pastoralists Society Organisation (Napaso) la Chalinze mkoani Pwani lililotafiti kata tano za wilaya ya Bagamoyo.

Mwenyekiti wa bodi ya shirika hilo Makaline Kashma anasema shirika hilo lilianza mwaka 2003 likiwa na lengo la kuongeza ubora, ufanisi na mabadiliko ya maisha ya wafugaji na wakulima katika wilaya ya Bagamoyo.

Anasema wanaamini kuwa ifikapo 2025 shirika hilo linakusudia kuwawezesha kikamilifu wafugaji na wakulima  kupambana na umaskini.


Josefu Joshua ni Ofisa Program wa Napaso, anasema Wilaya ya Bagamoyo ina asilimia kubwa ya wafugaji na wakulima na sehemu lakini maendeleo na matokeo ya elimu ya shule za msingi kwa mwaka 2013 na 2014 hayakuwa ya kuridhisha hivyo wameona ni vyema kupeleka nguvu nyingi kwenye elimu ambayo ni uti wa mgongo.

Anaitaja miezi sita iliyopita kuwa ni shirika limeendesha mradi wa uwajibikaji jamii wenye lengo la kuinua ushawishi wa vijana wanawake na makundi mengine ya kijamii kushiriki kikamilifu katika michakato ya kufanya maamuzi kwa ajili ya utoaji bora wa huduma za kijamii kwenye sekta ya elimu ifikapo mwaka 2016.

“Karibu shule zote za maeneo tunayofanyia kazi matokeo hayaridhishi na hii ikatupeleka kuona umuhimu wa kuanza mradi wa elimu kwenye kata nne na kithibitisho pekee ni utafiti ambao tumeufanya kwenye shule 15”, anasema mratibu wa Napaso Grace Scorey.

Anazungumzia hali ya ufaulu katika shule hizo akisema ni asilimia 47 ambao ni chini ya wastani wa taifa wa asilimia 57 na katika shule ya Kisanga wastani wa ufaulu ni asilimia sita, Tawalanda saba Kisambi 17 na Malivundo wastani wa ufaulu ni asilimia 18.

Katika utafiti huo walibaini changamoto mbalimbali zinazosababisha kufaulu miongoni mwa mwanafunzi kushuka katika shule kadhaa kama Ubena Ranchi, Hondogo, Chamakweza, Mbala, Kisambi, Mgogodo,Muungano  Mandera na Malivundo.

Scorey anabainisha changamoto hizo kuwa ni uhaba wa vitabu ambapo hauwiani na mwanafunzi . Kwa wastani wa shule zote ni wanafunzi wanne kwa kitabu kimoja na kuwa kwa shule ya Mgogodo hali mbaya kwani wanafunzi 13 hutumia kitabu kimoja.

Anasema jumla ya wanafunzi 298 katika shule 14 hawajui kusoma, kuhesabu wala kuandika na kuwa katika shule ya Muungano  wanaongoza kwa kutojua kusoma, kuhesabu na kuandika na huku mahudhurio kwa shule zote 15 ukiwa ni wastani wa asilimia 83.

Mratibu Scorey anafahamisha kuwa kwa upande wa uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi  shule sita ziko juu kwa wastani wa taifa lakini kwa upande Kisambi mwalimu ni mmoja na anafundisha watoto 120 kwa siku.

“Changamoto za ufaulu ni nyingi katika utafiti wetu ni shule saba tu ndizo zina uwiano mzuri wa madarasa lakini shule nyingi darasa moja linatumiwa na wanafunzi 120,” anasema na kutaja Muungano.

Kwa upande wa vyoo anazungumzia changamoto ya shule kukosa huduma hiyo ambapo katika shule 15 ni tatu ndizo zilizofikia malengo ya taifa ya tundu moja kwa wanafunzi 25.

“Kuna shule nyingine kama ile ya Makole ambayo ina wanafunzi 257 wanaotumia tundu moja pekee hivyo wanafunzi wanasubiriana kwa muda mrefu na wengine hutoroka kwa ajili ya kwenda kujisaidia maporini na wakati mwingine hawarudi tena shule”, anasema.

Licha ya matokea ya kumaliza mtihani wa darasa la saba mwaka jana kuonyesha ufaulu umeongezeka kwa asilimia 6.38 zaidi ya nusu ya shule hizo za jamii za wafugaji mkoani Pwani ziko katika kundi la wastani wa chini wa ufaulu.

Kwa mujibu wa viwango vya ufaulu wa mitihani uliowekwa kwenye tovuti ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwenye kundi la matokea makubwa sasa, shule 8,256 kati ya 15,867 zinaonyesha kuwa na ufaulu wa chini wa kuanzia alama 104.99 hadi 46 kati ya alama 250.

Pamoja na kuboresha elimu dhima ya Napaso ni kupambana na umaskini katika wilaya ya Bagamoyo kwa kuinua kiwango cha maisha ya wafugaji na wakulima kwa ushirikiano na  wadau wengine na kazi zake zinafanywa kwa ufadhili wa shirika la kimataif ala Action Aid.

Awali Ofisa Program wa Napaso, Joshua anasema programu kuu za asasi hiyo ni uhakika wa chakula, kipato, maji, usafi wa mazingira na afya ya msingi  na kisomo cha watu wazima, uhifadhi wa mazingira na upatikanaji na utumiaji endelevu wa rasilimali.
tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top