tiko
tiko
Rais alifanya mabadiliko kwenye baraza hilo baada ya mawaziri wawili kuanguka kutokana na kashfa ya uchotwaji takriban Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Ikiwa imesalia miezi isiyozidi sita kabla ya Baraza la Mawaziri kuvunjwa na akitakiwa kujaza nafasi mbili zilizoachwa wazi na Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Wizara ya Nishati na Madini na Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rais Kikwete alifanya mabadiliko 13, yakihusisha mawaziri wanane na manaibu watano.
Miongoni mwa mabadiliko hayo manane ya mawaziri, ni uhamisho wa Dk Mwakyembe kutoka Uchukuzi kwenda Afrika Mashariki huku Samuel Sitta, ambaye aliwahi kumwelezea mbunge huyo wa Kyela kuwa ni mmoja wa “marafiki wa kweli”, akihama kutoka Wizara ya Afrika Mashariki kwenda Uchukuzi.
Watu wengi walioongea na mtandao huu, walisema hakukuwa na haja ya kumhamisha Dk Mwakyembe kutokana na kazi nzuri ambayo ameshaifanya kwenye wizara hiyo, ambayo ina tatizo kubwa la usafiri wa reli, kuyumba kwa Shirika la Ndege (ATCL) na utendaji mbovu kwenye bandari, mambo ambayo Dk Mwakyembe alionekana kuyashughulikia kwa nguvu zote.
Sitta, mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki, alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, pia aliwahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC).
“Tulikuwa tunaziona jitihada za Dk Mwakyembe,” alisema mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Frank Tily. “Na kuhamishwa kwake kunamaanisha kuwa mambo yote yaliyokuwa yanaendelea yatatakiwa kuanza upya. Nashindwa kuelewa ni kwa nini waziri huyu amebadilishwa… ingekuwa bora zaidi kama angeachwa.”
Dk Frank Tily alisema kuwa kutokana na haja ya kuongeza mawaziri ili kuziba nafasi mbili zilizoachwa wazi, hakukuwa na haja ya kuwabadilisha wale waliofanya vizuri katika wizara zao.
Aliongeza kuwa nafasi ya uwaziri isiwe inajazwa bila ya sababu za msingi, bali ifanywe tu endapo kuna haja kweli ya kufanya mabadiliko na akasisitiza kuwa “wizara ya uchukuzi haikuwa na sababu za kubadilishiwa waziri.”
Naye mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, Samwel Chacha alisema kuwa, mabadiliko hayo yatakuwa na athari japo zinaweza zisionekane kwa muda mfupi.
“Mwakyembe alikuwa na mipango ambayo ilianza kuonekana na kudhihirisha uzalendo katika Wizara ya Uchukuzi. Kama angeachwa aendelee nayo, kungekuwa na mabadiliko ambayo yangetutambulisha Watanzania kwa kuwa na vitu vyetu kwa manufaa ya nchi nzima,” alisema Chacha.
Ofisa Mikopo wa Benki ya NMB, Tito Mwanjala alisema mabadiliko yaliyofanywa, yamekosa mwonekano mpya kutokana na wabunge wengi kukosa sifa zinazotumika kuwapata mawaziri hao.
“Baada ya Bunge kupitisha maazimio, Rais hakuwa na jinsi zaidi ya kutekeleza. Sura zimeendelea kuwa zile zile kutokana na kukosekana kwa watu wenye sifa kwa sababu waziri lazima awe mbunge ambaye anatoka chama tawala. Nadhani Rais atakuwa ametumia muda mwingi kuwapata mawaziri wapya aliowaingiza katika baraza lake,” alisema Mwanjala.
Aliongeza kuwa, mabadiliko yaliyofanyika katika Wizara za Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Uchukuzi, yanaweza yakawa na athari za kiutendaji kwani “viatu vya Mwakyembe vinaweza visimwenee Sitta” kutokana na muda mfupi uliobaki kwa waziri huyo kuonyesha tofauti iliyofanywa kwa muda mrefu na mtangulizi wake.
Hata hivyo, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaji Musa Salum alikuwa na maoni tofauti kwa kueleza kuwa, mabadiliko hayo ni sahihi na kwamba anaamini kutakuwa na ufanisi katika wizara zote kutokana na wateule wake kuwa watendaji wazuri.
“Mabadiliko ya Waziri Mwakyembe na Sitta yatakuwa na faida kwa wizara zote mbili kwa kuwa hawa wote wanafanya kazi kwa kujituma. Kila mmoja ataanzia pale alipoishia mwenzake na kufikia malengo yanayotarajiwa,” alisema Alhaji Salum.
Alifafanua kuwa hata mawaziri wengine nao watakuwa na mchango mkubwa kutokana na jitihada walizozionyesha walikotoka na kumtolea mfano George Simbachawene kuwa alijituma vya kutosha alipokuwa naibu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi.
tiko
tiko
Post a Comment