tiko
tiko
Kiongozi
wa mila tarafa ya Ngorongoro, Augustino Pakai Olonyokei akizungumza na
Meneja uendeshaji wa mtandao wa habari wamodewjiblog, Zainul Mzige
aliyefika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia miradi mbalimbali
inayoendeshwa kusaidia jamii ya wafugaji wa kimasai hivi karibuni.
Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
KIONGOZI wa
mila tarafa ya Ngorongoro Augustino Pakai Olonyokei ameitaka serikali
kusimamisha uwekezaji katika Mamlaka ya Ngorongoro ili kupunguza
shinikizo la raslimali katika eneo hilo.
Alisema kuendelea kuwekeza katika mahoteli,makambi ya watalii,
miundombinu katika hali ilivyo sasa ni kuzidisha migogoro iliyopo kati
ya wakazi wa eneo hilo na mamlaka ambayo tayari ipo.
Olonyokei alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa
habari hizi ambaye alifika eneo hilo kwa ajili ya kuangalia miradi
mbalimbali inayoendeshwa kusaidia jamii ya wafugaji wa kimasai.
Alisema hali ya sasa ni ngumu na inayosikitisha hasa kutokana na sheria
iliyoanzisha mamlaka ya Ngorongoro kuwanyang’anya umiliki wa eneo ambalo
wao wamelilinda miaka yote ndiyo maana wanyama wanapatikana na utalii
unakuwepo.
Aidha alisema mabadiliko ya hali ya hewa yanafanya mazingira yao kuwa
magumu , wanakuwa na njaa huku wakiwa wamekatazwa kulima hata eneo dogo.
“Tuna changamoto nyingi…hatuna ajira, ushiriki wetu katika bodi ni mdogo
na baraza la wafugaji linapewa hela kidogo katika mazingira ya kuwa na
miradi mingi,” alisema Olonyokei.
Alisema Baraza hilo kupewa sh bilioni moja tu haitoshi wakati utalii ukiingiza mabilioni ya fedha.
Pamoja na kuelezea changamoto hizo na kuitaka serikali kuzuia kuongezeka
kwa shughuli zaidi katika eneo hilo, aliwataka watanzania kujua
mazingira ya jamii ya wafugaji na adha wanazokutana nazo.
Hata hivyo Mhifadhi wa mamlaka ya Ngorongoro Dk. Freddy Manongi amesema
kwamba pamoja na malalamiko hayo, mamlaka hiyo iliyoanzishwa mwaka 1959
kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii, utalii na kuhifadhi mazingira mwaka
jana pekee ilitumia sh bilioni 60.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kuhifadhi, kuendeleza jamii na utalii.
Alisema msaada mkubwa wanaoufanya ni katika sekta ya elimu ambapo
imejenga shule 21 na kila mwanafunzi anayekwenda sekondari kutoka katika
eneo hilo hupatiwa udhamini wa masomo.
Aidha alisema kutokana na wananchi kuzuiwa kulima, huwapatia mahindi kwa
ajili ya chakula na ingawa kunatakiwa kuangaliwa namna bora zaidi
endelevu ya wananchi kupata chakula lakini kwa sasa hilo ndilo
wanalofanya.
Mhifadhi
wa mamlaka ya Ngorongoro, Dk. Freddy Manongi katika mahojiano maalum na
Meneja uendeshaji wa mtandao wa habari wamodewjiblog, Zainul Mzige
(hayupo pichani).
“Mahindi ya bure yanapokosekana anagalau yawepo ya kununua kwa bei ya chini, na tunauza kwa shilingi 5000 kwa debe” alisema.
Dk. Manongi alisema pia kwamba fedha nyingine zinatumika katika sekta ya
afya na pia kuboresha hali ya mifugo kwa kuwezesha uharamishaji mifugo
na kujenga majosho.
Alisema ongezeko kubwa la watu katika eneo ambalo haliongezeki ni
dhahiri linaleta migongano lakini mamlaka hiyo inafanya shughuli zake
kwa kushirikiana na Baraza la wafugaji ili kupunguza migongano.
Wakati mamlaka inaanzishwa 1959 eneo hilo lilikuwa na wakazi 8,000 baada
ya wengine 4000 kuhamishiwa hapo kutoka Serengeti. Kwa sasa eneo hilo
lina watu takaribani 90,000 katika eneo lilelile la kilomita za mraba
8,262.
Alisema baraza hupewa sh bilioni 2 kwa mwaka wakati shughuli nyingine za
maendeleo zinazofanywa na Mamlaka hugharimu sh bilioni 11.
Kuhusu changamoto za elimu amesema kwa mwaka jana hali haikuwa njema kwa
ufaulu lakini sasa wametafuta sababu na kuanza kuhakikisha kwamba
walimu wanapewa motisha na pia wanafunzi wanapata mlo wa mchana ili
kuwafanya wasitoroke.
Kuhusu suala la ajira Dk. Manongi amesema ni tatizo la tafsiri tu lakini
kila nafasi zinazpopatikana hujitahidi kuajiri watu kutoka katika eneo
hilo.
Alisema kuna mambo mengi yanayofanywa kuimarisha eneo hilo kuendeleza
jamii na kuendeleza hifadhi ili kuwezesha utalii ambao ndio unatoa fedha
kwa ajili ya mambo yote.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment