tiko
tiko
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama.
Jeshi
la Polisi mkoani Kilimanjaro, limelazimika kutumia mabomu ya machozi na
silaha za moto, kuzima maandamano ya wafugaji wa jamii ya Kimasai
kutoka mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, waliokuwa wamejipanga
kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi Sanya Juu, Wilaya ya Siha mkoani hapa.
Wafugaji
hao wanadaiwa walikuwa wakishinikiza kiongozi wao anayeshikiliwa (jina
halijafahamika), kuachiwa na Polisi Wilaya ya Siha.
Askari
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutoka Mjini Moshi waliokuwa na
magari manne, walilazimika kutumia nguvu walipokutana na wafugaji hao
wakiwa wamefika eneo la mwisho wa lami njia panda ya Karansi na
Magadini, Wilaya ya Siha wakielekea kilipo kituo hicho umbali wa
kilomita tano.
Habari
zilizopatikana jana na baadaye kuthibitishwa kwa njia ya simu na
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Geofrey Kamwela, zilisema makundi ya
wafugaji hao yaliingia Wilaya ya Siha kwa nyakati tofauti yakitumia
malori, pikipiki aina ya bajaj, bodaboda na magari ya kukodi.
“Kwa
sasa niko Siha kwenye operesheni maalum baada ya kuwatawanya wafugaji
kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Bahati nzuri tumefanikiwa kuzima
maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la kuvamia Kituo cha Polisi, na hivi
sasa tunakusanya taarifa za kiuchunguzi kwa hiyo kesho au baadaye
nitatoa taarifa ya kilichotokea,” alisema Kamanda Kamwela.
Kwa
mujibu wa Kamanda Kamwela, wafugaji hao ambao idadi yao hadi sasa
haijajulikana, licha ya kuingia mkoani hapa wakitokea mikoa hiyo ya
jirani kwa ajili ya kuunganisha nguvu na wenzao wa Wilaya ya Siha
kutafuta malisho ya mifugo yao, walikuwa wakitumia mbinu mbalimbali
kuwakwepa Polisi.
Novemba
14, mwaka jana, vurugu kama hizo zilizuka kati ya wafugaji wa jamii ya
Kimasai wa Wilaya za Siha mkoani Kilimanjaro na mikoa ya Arusha na
Manyara baada ya kuvamia na kuteketeza kwa moto hoteli ya kitalii ya
Ndarakwai na kambi sita zinazolaza watalii.
Uvamizi
huo ulisababisha zaidi ya vyumba 300, mali mbalimbali za mwekezaji wa
Kampuni ya Tanganyika Films & Safari inayomilikiwa na Peter Jones,
raia wa Uingereza ambaye anajishughulisha na utalii wa picha na uhifadhi
wa mazingira, kuteketezwa kwa moto.
Kambi
zilizotekezwa na wafugaji waliodaiwa kuvamia eneo la mwekezaji huyo
Novemba mwaka jana, ni Ndarakuwai, Kiseriani, Kambi ya Kati, Karakana,
Casablanca na Rafiki.
Kambi hizo zilikuwa na uwezo wa kupokea wageni kati ya 2,500 hadi 3,000 kwa mwaka kutoka mataifa mbalimbali.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, akizungumza jana kwa njia ya
simu alisema kama wafugaji hao walikuwa wanataka kiongozi wao aachiwe na
Polisi, walipaswa kufuata utaratibu wa kumwekea dhamana na si kufanya
maandamano ambayo yanaweza kuvunja amani.
“Mimi
niko kwenye maandalizi ya kumpokea Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, na
sijapata taarifa ila hao wafugaji walipaswa kufuata sheria kwa kumwekea
dhamana huyo anayeshikiliwa na Polisi, si kuandamana kwa sababu huko ni
kuvunja amani…nakuomba jaribu kumtafuta
RPC (Kamanda wa Polisi) yeye atakupa taarifa za uhakika,” alisema Gama.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Siha, Dk.
Charles Mlingwa, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, alipotafutwa
kuzungumzia tukio hilo alisema:
“Wilaya yangu iko vizuri, naamini hizo ni operesheni za Polisi na itapendeza zaidi ukiwasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa.”
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment