tiko
tiko
Wapo wastaafu wengi wa Serikali ambao wanafuatilia kwa karibu nyenendo za siasa nchini, mmoja wapo ni Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa (68) ambaye amekitahadharisha chama cha CCM kwamba kijiandae kwa Serikali ya mseto.
“Na
endapo Rais atatoka CCM na wabunge wengi ndani ya Bunge wakawa ni wa
upinzani, basi lazima Rais huyo akubali kufanya kazi na upinzani.
“Itabidi
akubali kuunda Serikali ya mseto, japo sitarajii kufika huko. CCM ni
imara, lakini tuwe na fikra hizo pia kwa nia nzuri ya kuiweka nchi
katika amani,” ni kauli ya Kanali Mjengwa ambaye pia ni mkuu wa wilaya mstaafu.
Akizungumza na Mwananchi nyumbani
kwake Mbarali, Kanali Mjengwa alisema licha ya upinzani kuwepo na
kujipambanua kwa wananchi, lakini bado siyo tishio kwa CCM na itaendelea
kushika dola tu kwani inaaminika na Watanzania wengi.
“Upinzani
kuingia Ikulu bado sana, ila kwenye nafasi ya ubunge na udiwani ndiko
kutakuwa na changamoto kubwa. Kuna uwezekano mkubwa wa wabunge wengi
wakatoka upinzani lakini siyo Rais.
“Lakini
niseme tu kwamba pamoja na CCM kuendelea kuaminiwa na wananchi wengi,
isibwete wala kupuuza upinzani. Hawa jamaa wanazidi kujitanua kweli
kweli, hivyo wanaweza kuiyumbisha,” alisema Kanali Mjengwa.
Kanali
Mjengwa alisema CCM bado inaaminiwa na Watanzania wengi, lakini tatizo
linalomkera na ambalo kwa maoni yake linaharibu adabu na sifa ya CCM ni
kitendo cha wana-CCM kuchafuana majukwaani.
Alisema
CCM imetoka mbali na inatakiwa kuongoza kwa vitendo na siyo kupiga
kelele za kuchafuana majukwaani kama ambavyo ilivyo hivi sasa.
Kwa
mujibu wa Kanali Mjengwa anachukia kuona mwana-CCM anatumia jukwaa
kumchafua mwenzake kisa tu wote wametangaza nia ya kugombea nafasi
fulani ya uongozi.
“Kama
unona mwana CCM fulani amekwenda ndivyo sivyo kuna taratibu za vikao
ndani ya chama, wakazungumzie na kumaliza tofauti hizo ndani ya Chama
ili kulinda heshima ya Chama na si vinginevyo.
“Na
kitendo hicho ndicho kinachowapa nguvu wapinzani kwa kusemea na
kutunanga kwa Wananchi hatimaye CCM inaonekana kutokuwa na watu makini,” alisema.
Kanali
Mjengwa alisema katika kuelekea uchaguzi mkuu hali ya kisiasa inazidi
kupamba moto na kila chama kinazidi kujipambanua kivyake kwa wananchi
kikitaka kuungwa mkono.
Alisema
tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi kumekuwa na upinzani mkubwa, japo
CCM kimekuwa kikiibuka na ushindi kwa nafasi ya urais na majimbo mengi
ya ubunge.
Kanali
Mjengwa alisema bado anaamini kwamba uchaguzi wa mwaka huu utakuwa
salama na amani, kama Watanzania hususan wanasiasa wataamua uwe hivyo.
Kuhusu mgombea urais, alisema mgombea atakayeteuliwa na CCM ndiye atakayekuwa rais. “Na
kuhusu karata yangu naitupa kwa nani… kundi la wana-CCM wanaoonekana
kutangaza nia hiyo atatoka kwenye kundi hilo na mimi namfahamu ila
siwezi kukutajia kwa sasa ila ujue hivyo,” alisema.
Akizungumzia
umuhimu wa amani, kuwa wanasiasa wengi wanahubiri mfarakano bila
kutambua kwamba na wao ni Watanzania, na amani ikivurugika na wao
watasambaratika.
“Kiongozi
wa siasa anapopanda jukwaani na kuhubiri eti nchi haitatawalika, damu
itamwagika huwa najiuliza hivi huyo siyo Mtanzania? Na hajui kama hayo
yakitokea na yeye damu yake na ya ndugu zake itamwagika?," alisema.
Hivi
karibuni Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki alinukuliwa
akitabiri kuwa CCM ina “kazi kubwa”, katika uchaguzi mkuu ujao.
Balozi
Kagasheki pia alikitahadharisha chama hicho dhidi ya kuzidi kukua kwa
nguvu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akisema iwapo umoja huo
utamchagua mgombea makini, CCM itakuwa na kazi ngumu.
Kauli
yake iliungana na za vigogo wengine wa CCM waliotahadharisha mwenendo
wa chama hicho dhidi ya ongezeko la nguvu ya upinzani, akiwamo Waziri
Mkuu wa zamani, Fredrick Sumaye, ambaye alisema rushwa inakimaliza chama
hicho, na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba,
ambaye alisema kuwa chama hicho kisitegemee ushindi wa kishindo.
Mwananchi
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment