tiko
tiko
Wakati mwingine kuna maswali magumu sana
kuweza kuyajibu. Kwa mfano kwanini watu muhimu na wazuri hufa mapema?
Kwanini watu wenye umuhimu mkubwa katika jamii huondoka ghafla tena
katika wakati ambapo wapo kwenye kilele cha mafanikio yao?
Chukulia mfano Aaliyah, Tupac, Notorious
BIG au Stephen Kanumba! Hili ni swali gumu sana kulijibu na hivyo mambo
mengine ni ya kumwachia Mungu.
Leo ni April 7, miaka mitatu tangu kifo cha muigizaji mahiri, aliyependwa, aliyekuwa na kipaji cha hali ya juu, Kanumba.
Kifo chake kilikuwa cha kushtusha na cha
ghafla. Alifariki kwa kuanguka chini alipokuwa kwenye ugomvi wa kawaida
na mpenzi wake Elizabeth ‘Lulu’ Michael. Kifo chake kilifichua siri
ambayo wengi tulikuwa hatufahamu – kwamba Lulu na Kanumba walikuwa na
uhusiano wa kimapenzi kwa muda mrefu.
Lulu akaingia hatiani na kukabiliwa na
kesi ya kuua bila kukusudia. Amekaa mahabusu kwa miezi mingi kabla ya
kutoka kwa dhamana na sasa ikiwa wazi kuwa kesi hiyo ni kama imeshafutwa
kimya kimya.
Kanumba alifariki kipindi ambacho
alikuwa kwenye kilele cha mafanikio yake. Alikuwa ametoka kuigiza filamu
ya kimataifa iitwayo Devil’s Kingdom akiwa na Ramsey Noah wa Nigeria.
Jina lake lilikuwa halivumi Afrika Mashariki peke yake, bali Ghana na Nigeria walikuwa wameanza kumsikia na kukubali uwezo wake.
Kanumba alikuwa na ujasiri, mbishi na
hakuogopa kujaribu. Kupitia miradi yake ya kuwashirikisha wasanii wa
Nollywood, wadau wengi wa filamu barani Afrika walianza kushawishika na
umahiri wa filamu za Kitanzania.
Laiti kama Mungu angemwepushia mauti,
leo Kanumba angekuwa mbali sana. Hakuna shaka kuwa kwa speed aliyokuwa
nayo, Hollywood ilikuwa ni kituo chake ambacho kingefuata.
Kanumba aliwapa changamoto waigizaji
wenzake wa filamu nchini kwa kufanya filamu zenye story za kuvutia.
Ameondoka na kuacha pengo kubwa.
Miaka mitatu baada ya kifo chake,
kiwanda cha filamu nchini kimeyumba sana. Bongo movies hazipo tena
midomoni mwa watu. Filamu za kibongo hazitengenezi tena mijadala
vijiweni. Waigizaji wa filamu hawatengenezwi tena mada vibarazani.
Kiwanda hicho hakina tena msisimko.
Kiwanda kimegeuka kuwa sehemu ya vita
vya maneno, makundi na miparaganyiko. Waigizaji wazuri wameanza kukata
tamaa na hali ilivyo sasa na kuamua kutafuta njia mbadala za kuendesha
maisha yao.
Pamoja na kuwepo filamu nyingi sokoni, bado hazitengenezi hamu ya kuangaliwa ama kushawishi watu kuzinunua.
Tatizo kubwa ambalo kiwanda cha filamu
Tanzania kinalo ni kutokuwepo na njia nzuri ya kuzifanyia promotion.
Filamu nyingi zinatoka kimya kimya.
Hebu chukulia mfano huu kwamba
wasambazaji wa filamu za Hollywood nchini Marekani, hutumia zaidi ya
dola bilioni 4 kwa mwaka kutangaza filamu mpya kwenye TV, redioni,
kwenye matangazo ya barabarani na mtandaoni.
Biashara ni matangazo, hata kama iwe
biashara yenye wateja wengi kiasi gani. Kwahiyo msisimko kwenye soko la
filamu za Tanzania ni mdogo sana kwakuwa wasambazaji hawatengi bajeti ya
kuzitangaza filamu zao.
Kadri miaka inavyozidi kwenda, filamu za
Tanzania zinaendelea kuwa za kawaida sana. Hali hii ikiendelea hivi
hivi, kuna wasiwasi kuwa kiwanda hiki kitakufa kabisa!
RIP Kanumba.
By: Fred Bundala on Bongo5
tiko
tiko
Post a Comment