tiko
tiko
Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Ziwa Magharibi,
kimeanzisha operesheni maalumu kwa ajili ya kusaka ubunge katika majimbo
yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ambayo yanashikiliwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Operesheni hiyo inayojulikana kama
‘tigitigi’, ilianza juzi kwa kutumia usafiri wa helikopta katika majimbo
kadhaa, ikiwamo Jimbo la Sengerema linaloshikiliwa na mbunge wa sasa,
William Ngeleja.
Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita
Alphonce Mawazo ni miongoni mwa makada wa chama hicho waliofika katika
jimbo la Sengerema juzi, wakiambatana na kada wa chama hicho anayetaka
kutangaza nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo, Hamis Tabasamu.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara
iliyofanyika katika vijiji tofauti kwa muda wa dakika 30 katika kila
kijiji, Mawazo alisema wameanzisha operesheni hiyo kwa lengo la kushinda
ubunge kwenye majimbo yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ili kuleta
ukombozi wa kweli kwa wananchi.
“Wananchi naomba niwambie tumeanza na
Jimbo la Sengerema, tutapambana hadi hatua ya mwisho ili kulikomboa
jimbo hili. Tunataka Kanda ya Ziwa iwe ya mfano, tutazunguka kata zote
na vijiji vyote katika mikoa ya Geita, Simiyu, Mwanza, Tabora, Shinyanga
na Mara kuelimisha wananchi,” alisema Mawazo na kuongeza’
“Pia naomba wananchi mjitokeze
kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili tuweze kupata
nafasi ya kufanya mabadiliko ya kweli mwezi Oktoba. Ndugu zangu
mapambano yameanza hakuna kulala, huu ni wakati wetu Chadema,” alisema.
Naye mtangaza nia wa jimbo hilo, Hamis
Tabasamu ambaye aliwahi kuwa diwani wa Sengerema, alisema kuwa
watafungua ofisi 78 za Chadema kwenye jimbo hilo ili wananchi waweze
kuwa na sehemu za kutoa malalamiko yao kwa viongozi na kuhudumiwa.
Alisema muda uliopo sasa ni wa kufanya
mabadiliko na kwamba kazi ya kutafuta ukombozi Sengerema imeanza, hivyo
ni jukumu la wananchi wa eneo kuunga mkono jitihada za chama hicho za
kuwaletea maendeleo endelevu.
“Mimi ni mtangaza nia wa jimbo hili nipo
tayari kushirikiana na nyie kuleta mabadiliko ya kweli Sengerema.
Tutafungua ofisi 78 hapa na kazi zitafanyika kila kona ya jimbo hili ili
tuweze kuing’oa CCM hapa. Nia na sababu ya kuing’oa CCM tunazo kwa kuwa
ni ukweli kwamba haijafanya kitu chochote katika uongozi wake eneo
hilo,”alisema Tabasamu.
tiko
tiko
Post a Comment