tiko
tiko
Ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutangaza kung’atuka katika nafasi yake ya ubunge, Bunge limeeleza kuwa mbunge huyo atapata mafao yake yote kama wabunge wengine.
Zitto
ambaye alitangaza juzi bungeni kuwa anaondoka baada ya kuvuliwa
unanachama wa Chadema aliahidi kuwa ‘Mungu akipenda’ atakuwa tena ndani
ya chombo hicho cha kutunga sheria Novemba mwaka huu baada ya uchaguzi
mkuu.
Kuondoka
kwa mbunge huyo pia kunaifanya nafasi ya uenyekiti wa Kamati ya Hesabu
za Serikali(PAC) kuwa wazi kwa kuwa ndiye aliyekuwa akiishikilia hadi
alipotangaza rasmi juzi kuachia ubunge.
Akizungumzia
uamuzi wa Zitto na juu ya mafao yake baada ya kuamua kuondoka mwenyewe,
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema kuwa mbunge huyo
atalipwa mafao yake yote.
“Unajua
Chadema wametangaza kumvua uanachama Zitto lakini hawajampa barua, sasa
yeye ameona kuwa kuliko kuendelea na ubunge wake ni vyema akakaa kando.
Kutokana na suala hilo atalipwa tu mafao yake yote,”alisema Joel.
Katika
hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa PAC wamesikitishwa na kuondoka kwa
Zitto kabla ya muda wa Bunge la 10 kumalizika huku wakimwelezea ni
kiongozi aliyeweza kuwaunganisha katika kamati bila kujali itikadi za
vyama.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti jana, wajumbe hao walisema aliwafanya wajumbe wa
kamati hiyo kuwa familia na aliwaamini na kuwaheshimu wote.
“Ni mtu aliyekuwa na ushirikiano na aliweza kutuunganisha bila kujali itikadi.
"Alitufanya kama familia na alituamini na kutuheshimu. Tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ijayo,”alisema Ismail Aden Rage (Tabora Mjini).
Mbunge
wa Mkwamtipura, Kheir Ali Khamis alisema kujiuzulu kwa Zitto ni suala
la Kikatiba asingeweza kuendelea kushika nafasi hiyo.
“Hili ni suala la Kikatiba haki ya kuwa mbunge inaondolewa ukishakuwa si mwanachama wa chama cha siasa,”alisema.
Alisema kutojiondoa mwenyewe kungeleta mgogoro kati yake na chama chake kwa kuwa tayari walishamvua uanachama.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy alisema kuondoka
kwa Zitto kunalenga katika kujipanga upya katika chama chake kipya cha
siasa.
“Yeye
ni mwanasiasa atakaa hivi hivi? Na kwenye chama chake ameshafukuzwa
anaenda kukijenga chama chake cha ACT ili katika uchaguzi ujao apate
madiwani na wabunge,”alisema Keissy.
Mbunge wa Ludewa ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Deo Filikunjombe alisema, “Zitto alikuwa kama baba ndani ya kamati na kuondoka kwake kutaifanya kamati kuyumba.”
Filikunjombe
ambaye ni rafiki wa karibu wa Zitto alisema kamati hiyo itayaenzi
mazuri yake na kwamba kazi alizozifanya ndani ya Bunge zitaendelea
kukumbukwa.
Hata hivyo, Filikunjombe alisema,“Zitto
bado hajafukuzwa kwa sababu hajapewa barua rasmi ila yeye mwenyewe
ameamua kukaa pembeni kutokana na maneno yanayoendelea kusemwa pamoja na
ukimya wa chama chake.”
tiko
tiko
Post a Comment