tiko
tiko
SIKU moja baada ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kutangaza kujiuzulu kutokana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akaunti ya Tegeta Escrow, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema suala hilo bado ni bichi.
Pamoja na hali hiyo, PAC imesema hadi sasa Serikali imetekeleza maazimio manane ya Bunge kwa asilimia 35.
Akizungumza
na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), Zitto Kabwe, alisema kati ya maazimio manane yaliyopitishwa na
Bunge hadi sasa ni matatu pekee yaliyotekelezwa.
Alisema
suala la Akaunti ya Tegeta Escrow ni kubwa kuliko Profesa Muhongo,
hivyo watu waliodhani kuondoka kwake litakuwa mwisho wanajidanganya.
“PAC
itaendelea kupaza sauti ili maazimio yatekelezwe. Watu waliodhani kuwa
akitoka (Profesa) Muhongo basi suala hili limekwisha wanajidanganya.
Suala hili ni kubwa zaidi ya Muhongo,” alisema Zitto.
Maazimio nane ya Bunge
Akifafanua
maazimio yaliyopitishwa na Bunge, Zitto alisema la kwanza lilikuwa
linamuhusu Singh Seth (Mmiliki wa Kampuni ya Kufua umeme ya Pan African
Power Limited (PAP) na watu wengine waliotajwa na taarifa ya PAC.
Azimio
hilo lilitaka watu hao kuchukuliwa hatua na vyombo vya sheria kuhusika
na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na Miamala ya Akaunti ya Escrow
na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi unaoendelea kuhusika
katika vitendo vya jinai. Zitto alisema mpaka sasa ni vidagaa tu
wamefikishwa mahakamani kuhusiana na suala hilo.
“Waliofikishwa mahakamani ni wapokeaji tu na sio watoaji, waliopewa fedha kupitia Stanbic hatujawaona mahakamani."
Alisema
kuwa, ofisa mmoja wa PAP (jina tunalihifadhi kwa sasa) alitoa fedha
nyingi sana kutoka Benki ya Stanbic hivyo anapaswa kuchunguzwa ili
ijulikane ni wapi alipeleka fedha hizo.
Kuhusu
umiliki wa mitambo ya IPTL ambayo Bunge liliazimia kuwa Serikali
iangalie uwezekano wa kuichukua na kuimilikisha kwa Tanesco kwa mujibu
wa sheria za nchi bado pia halijaguswa.
“Suala
la msingi sana la umiliki wa IPTL bado kabisa kushughulikiwa, bado
kabisa. PAC haikumaanisha utaifishaji bali ni kwamba hakuna haja ya IPTL
wakati umeme wao hatutauhitaji kabisa,” alisema Zitto.
Alisema
azimio la tatu ambalo lilihusu mapitio ya mikataba ya umeme kama
ilivyoagizwa kwenye kamati teule ya Bunge iliyoshughulikia suala la
Richmond, mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya utekelezaji wake.
Kuhusu
azimio la nne lililohusu kuundwa kwa chombo maalumu cha kushughulikia
rushwa kubwa kubwa na lile la tano la kuundwa kwa tume ya kuchunguza
majaji waliohusishwa na kashfa hiyo, alisema utekelezaji wake ni bado
ingawa kuna muda wa kulishughulikia.
Alisema
azimio la sita lililohusu kuzitaja benki za Stanbic na nyingine
zilizohusishwa na sakata hilo kuwa ni vyombo vya utakatishaji fedha,
bado kabisa halijafanyiwa kazi.
Maazimio
ya Bunge yaliyofanyiwa kazi mpaka sasa ni lile la saba ambapo Profesa
Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema, wameachia nafasi zao huku Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na
Madini, Eliachim Maswi, akiwa amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.
Pia
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco waliotakiwa kuwajibishwa,
tayari muda wao ulishaisha na tayari bodi mpya imeteuliwa.
Pamoja
na hilo azimio la nane lililokuwa likiwahusu wenyeviti wa kamati za
kudumu za Bunge, William Ngeleja, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala, Andrew Chenge aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati
ya Bajeti na Victor Mwambalaswa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Nishati na Madini, tayari Spika Anne Makinda alishatangaza nafasi zao
kuwa ziko wazi.
Hata
hivyo, azimio la kwanza limeanza kutekelezwa kwa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwafikisha mahakamani watu waliohusika
na kashfa hiyo, ingawa Zitto anasema bado ni vidagaa vinavyofikishwa
mahakamani.
Juzi
akitangaza mbele ya waandishi wa habari kuhusu uamuzi wake wa
kujiuzulu, Profesa Muhongo alisema kutamaliza mjadala wa Escrow ambao
ulisababisha shughuli za maendeleo kusimama.
Kutokana
na mabadiliko ya Baraza la Mawaziri, wadau mbalimbali wakiwemo wasomi
na wanasiasa wametoa maoni yao kuhusiana na baraza hilo.
DK. LWAITAMA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azavel Lwaitama, alisema
mabadiliko hayo yanaashiria kuwapo kwa upungufu katika Katiba ya mwaka
1977 na Katiba inayopendekezwa.
“Rais anateua mawaziri na kuwaapisha bila majina yao kuthibitishwa na bunge, hali hii haisaidii kuwa makini katika utendaji.
“Angekubali
mfumo uliopendekezwa kwenye rasimu ya Jaji Joseph Warioba ingemsaidia
kupunguza uwezekano wa kuteua watendaji ambao si waadilifu,” alisema Dk.
Lwaitama.
Hata
hivyo, Dk. Lwaitama alishangazwa na kitendo cha kuachwa kwa mawaziri
aliodai kuwa ni mizigo kwani hata Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kilishapendekeza waondolewe.
Pia
alitilia shaka uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene, kwa kusema kuwa hawezi kuleta jipya kwani hata utaalamu wa
madini hana.
PROFESA MPANGALA
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema
mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri hayawezi kuleta maajabu kwa sababu
muda uliobaki ni mfupi.
“Mimi
nilitarajia angeziba mapengo mawili ya waziri wa ardhi na waziri wa
nishati na madini kwa sababu muda umebaki mfupi kuliko kupangua sehemu
kubwa ya baraza,” alisema Profesa Mpangala.
Kuhusu
kujiuzulu kwa Profesa Muhongo, alisema waziri huyo angejijengea heshima
kama angejiuzulu mapema wakati bunge lilipopitisha maazimio manane.
“Alipaswa
kujiuzulu mapema kwa sababu ilikuwa ni wazi kwa nafasi yake kashfa
kubwa kama ile imetokea kwenye wizara yake alitakiwa kuwajibika…sasa
anajiuzulu dakika za mwisho baada ya presha kubwa amechelewa
sana,” alisema.
Dk. BANA
Mhadhiri
wa UDSM, Dk. Benson Bana, alisema mabadiliko hayo hayawezi kuleta tija
katika utendaji serikalini kwa sababu muda uliobaki ni mfupi.
“Imebaki
miezi tisa tu ya kufanya kazi sasa utaleta mabadiliko gani katika
wizara, wengine watatumia miezi mitatu hadi sita kujifunza kazi za
uwaziri na kuielewa wizara,” alisema Dk. Bana.
Dk. Bana pia alikosoa uteuzi huo kwa kuhamishwa kwa baadhi ya mawaziri katika wizara nyeti.
“Mwakyembe
alikuwa anafanya vizuri lakini kule alikopelekwa (Wizara ya Ushirikiano
wa Afrika Mashariki) ni kama amekwenda kupumzika tu. Kuna wizara nzito
ambazo zinahitaji watu wazoefu siyo matamshi mengi kuliko
matendo,” alisema.
Kuhusu
kujiuzulu kwa Profesa Muhongo, alisema waziri huyo amejiuzulu baada ya
kuwapo shinikizo kubwa hivyo haesabiki kama amejiuzulu kwa matakwa yake.
JUKWAA LA KATIBA
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba (JUKATA), Deus Kibamba, alisema baraza hilo halina
mwelekeo na limedhihirisha kuwa Rais ana washauri wabovu wa masuala ya
kisiasa.
“Taifa
letu linapitia wakati mgumu, nilitegemea Rais alete watu watakaomsaidia
kupambana kwenye hali ngumu kama hii lakini sijaona.
“Kazi
kubwa ya Rais ni kupanga timu nzuri ya watendaji lakini kwa mabadiliko
haya hakuna mwelekeo, bunge linavunjwa Julai angefukuza walioshindwa
kazi na kuleta wapya,” alisema Kibamba.
TUCTA
Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicholas Mgaya,
alisema mabadiliko hayo ni mazuri lakini baadhi ya mawaziri walipaswa
kupumzishwa kwa sababu tayari wamechoka.
“Kuna watu wamechoka, wamezeeka wangepaswa kupumzishwa, wanawaacha wakati kuna vijana wengi makini wako nje,” alisema Mgaya.
MTATIRO
Naibu
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro,
alisema: “Mawaziri ni walewale, hakuna jipya, tutegemee mambo yaleyale”.
Kuhusu
kujiuzulu kwa Profesa Muhongo, alisema lazima waziri huyo asaidie
kwenye upelelezi nani kasababisha taifa liibiwe mabilioni ya fedha za
umma.
“Mimi
binafsi nampongeza kwa kukubali kuwa cheo ni dhamana. Lakini najua
hakujiuzulu kwa kutaka amelazimishwa ili mkuu wa nchi apate ahueni.
“Lakini
lazima atusaidie kwenye upelelezi, nani kasababisha taifa liibiwe
mabilioni ya fedha za umma, hivi sasa hatuangalii ikiwa anaamini fedha
zile ni za umma au la,” alisema.
Credit: Mtanzania
Credit: Mtanzania
tiko
tiko
Post a Comment