Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

MTWARA: UBOVU WA MIUNDOMBINU CHANZO CHA MAFURIKO

tiko tiko
Mtwara Mjini ni miongoni mwa wilaya tano zinazounda Mkoa wa Mtwara uliopo Kusini Mashariki mwa nchi ya Tanzania. Upande wa Kaskazini, Mtwara Mjini inapakana na Mkoa wa Lindi, Mashariki kuna Bahari ya Hindi na Kusini na Magharibi kuna Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Mheshimiwa Hasnain Mohamed Murji.
Pia Mtwara Mjini ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Hasnain Mohamed Murji kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Wiki iliyopita, Uwazi lilichanja mbuga mpaka kwenye jimbo hilo na kuzungumza na wananchi mbalimbali ambao walieleza matatizo yanayowakabili kisha mbunge wao akayatolea ufafanuzi.
MATATIZO YA WANANCHI NA MAJIBU YA MBUNGE
Wakati gazeti hili likiwa ziarani Mtwara, lilishuhudia maeneo mengi ya Manispaa ya Mtwara yakiwa yamekumbwa na mafuriko makubwa yanayosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Maeneo ya Kisutu, Nabwada na Kiangu, ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa sana na mafuriko huyo kwa maji kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu mkubwa.“Yaani hali ni mbaya kama unavyoona, maji ya mafuriko yameingia ndani na kuharibu kila kitu ndani. Mpaka mazao ya chakula yaliyokuwa ndani yameharibika hata sijui tutaishije. Tunaiomba serikali itusaidie,” alisema Juma Hafidhi, mkazi wa Nabwada.
“Uzembe ni wa serikali, yaani mvua kidogo tu mafuriko yanatokea. Kwa nini wasijenge mitaro mikubwa ya kupitisha maji? Tunateseka sana kiukweli, tunaomba tusaidiwe ili hii kero ya mafuriko iishe,” alisema Ismail Nangwanda, mkazi wa Kiangu ndani ya jimbo hilo.
Jibu: Ni kweli mafuriko ni tatizo kubwa Mtwara, tumechukua hatua za makusudi za kuchimba bwawa kubwa na mabomba yanayopeleka maji baharini lakini tatizo ni kwamba Mtwara ipo kwenye usawa wa bahari kwa hiyo zinahitajika fedha nyingi zaidi. Tatizo linashughulikiwa kikamilifu na muda si mrefu tutalipatia ufumbuzi wa kudumu. Wahanga wa mafuriko tunawasaidia kwa hali na mali na tayari nimeshaiarifu kamati ya maafa ije kutusaidia.
Soko la Mbae, Mtwara.
Tatizo lingine ambalo Gazeti la Uwazi limelishuhudia jimboni humo, ni uhaba mkubwa wa dawa katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula ambapo wananchi wanahangaika kwenda kununua madawa katika maduka yaliyopo jirani na hospitali.
“Huu ni uzembe wa serikali, yaani kama huna fedha unaweza kufa huku unajiona. Mi najiuliza, kama wenye maduka dawa wanazipata inakuwaje hospitali ya serikali, tena kubwa kama hii ya Ligula ikose dawa? Ni uzembe mkubwa na inawezekana madaktari wanakula njama na wenye maduka ya dawa,” Christopher Mwasikili, mfanyabiashara mjini Mtwara aliliambia Uwazi.
Jibu: Tatizo kubwa ni kwamba hii hospitali ya Ligula ipo chini ya mkuu wa mkoa kwa sababu ina hadhi ya rufaa. Sasa inakuwa vigumu kuhoji fedha zinazotolewa na serikali zinafanya kazi gani kama hata dawa zinakuwa ni tatizo kubwa kiasi hiki. Kwa zahanati na vituo vya afya ambavyo vipo chini yetu, tatizo siyo kubwa kama Ligula. Naendelea kuhangaika usiku na mchana ili kulipatia ufumbuzi tatizo hili.
“Kwa hapa Mtwara tunashukuru matatizo ya maji na umeme siyo makubwa lakini bado kuna matatizo mengine mengi. Hakuna ajira hasa kwa sisi vijana, tutaishije sasa?” alisema Yusuf Matiku, mkazi wa Kisutu jimboni humo.
Jibu: Tumeshazungumza mpaka na mheshimiwa rais kwamba makampuni yote yanayokuja kuwekeza Mtwara ni lazima yaajiri wazawa lakini tatizo ni kwamba watu wanatoka Dar es Salaam au nje ya nchi kuja kufanya kazi Mtwara wakati wazawa wanahangaika. Naendelea kupigania hilo.
Matatizo mengine yaliyobainishwa na wananchi wa jimbo hilo, ni uvuvi haramu ambapo nyavu zilizokatazwa (kokoro) na baruti vinatumika kwenye uvuvi na kusababisha madhara kwa viumbe vya baharini na walaji wa samaki.
Jibu: Uvuvi haramu upo lakini kuwakamata wanaovulia kokoro au baruti na kuwapokonya zana zao pekee hakutoshi kwa sababu wakazi wengi wa huku wanategemea uvuvi. Ninachokifanya ni kuzungumza na wizara ili wavuvi wapewe elimu kisha wapewe vifaa vya kisasa vya uvuvi wakiwa katika makundi. Hiyo ndiyo dawa ya uvuvi haramu.
tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top