Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

‘JICHO LA FIKRA’ LITUMIKE BUNGENI TUKIELEKEA UCHAGUZI MKUU

tiko tiko

MUNGU ni mwema na ndiyo maana amenichagua mimi na wewe kuendelea kuishi hadi leo, hivyo tumsifu!
Baada ya kusema hayo nianze makala haya kwa kusema kuwa wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu hapa Tanzania, Oktoba mwaka huu, tayari yapo matukio yanayojitokeza yakiwa na taswira tofauti.
Kimsingi matukio haya yanahitaji mtu atumie zaidi ‘jicho la fikra’, kuliko macho ya kawaida ili kupata tafsiri sahihi ya anayoyaona au hata kuyasikia na ni jukumu la wabunge wanaoanza kikao chao leo mjini Dodoma na wananchi kutafakari hili nitakalolisema leo.
Miongoni mwa mambo ya kuyaangalia ni uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi kutoka katika vyama, mikutano ya kuhusisha vyama husika katika ngazi tofauti, kuanzishwa miradi mbalimbali katika maeneo tofauti ya kupiga kura, zawadi na misaada kwa wapiga kura ktoka kwa wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali.
Niwaambie wabunge na wananchi wote kuwa jicho la fikra lina sifa ya kuona mbali zaidi na linaambatana na maswali mengi ambayo pindi yakijibiwa kwa usahihi, tafsiri halisi ya matukio husika hupatikana.
Kinyume chake macho haya ya kawaida, yana udhaifu mkubwa kiasi cha kutoa taswira au picha ya kitu tofauti na kinavyoonekana. Kwa hiyo wote tuwe makini katika kuujua ukweli huo. Mfano, kwa kutumia macho haya ya kawaida, utamuona mtu anacheka na anazo ishara zote za kucheka, lakini katika hali halisi mtu huyo amekasirika sana na ndani ya moyo wake anatokota kwa chuki, uadui na hasira kali na visasi dhidi ya wengine.
Kulithibitisha hili, wachunguze wanasiasa wa Tanzania wanapokaribishwa katika hafla za kidini. Machoni hucheka sana, lakini hotuba na kile kinachoitwa nasaha zao kwa waumini hubeba picha nyingine kabisa tofauti na wanavyoonekana machoni. Huwakejeli, huwacheka, huwalaumu na hata kuwadhalilisha kisaikolojia, lengo likiwa ni kuwafanya waamini kuwa, wao ni raia wa daraja la pili katika jamii hii.
Kutokana na ukweli huo ndiyo maana, tumeanza kwa anwani kuwa, jicho la fikra litumike ili tupate picha halisi ya mambo yanayojitokeza, lengo likiwa ni kuinusuru jamii na dhuluma katika kipindi kijacho cha uchaguzi. Kimsingi, hiyo ni tafsiri ya kwanza inayopatikana kutokana na macho ya kawaida na kila mmoja anaweza akaridhika nayo.
Hata hivyo, jicho la fikra, lenye sifa ya kuona mbali na vizuri zaidi, picha nyingine tofauti na ya mwanzo inapatikana na hii ni hali halisi zaidi kwa wale wenye kujua hadhi yao stahiki katika jamii hii. Kuiona picha hiyo ni vyema ukajiuliza maswali yafuatayo. Je, viongozi wa dini nao ni wanasiasa? Jibu likiwa ndiyo, swali jingine litakuwa, ni vyama gani vya siasa wanavyoviwakilisha?
Jibu la swali la kwanza likiwa ni hapana, swali lingine litakuwa, kwa nini askari hawawakamati viongozi wa dini wanaohubiri siasa katika nyumba za ibada?Ikumbukwe kuwa, katika nchi yetu majumba ya ibada na viongozi wao hawaruhusiwi kufanya mambo ya kisiasa, kwani kufanya hivyo watakuwa wamechanganya dini na siasa na stahiki yake ni kufunguliwa kesi za uchochezi.
Kwa kuzingatia hali hizo, tunaamini kuwa jicho la fikra litafanya kazi sawasawa na kutoa majibu sahihi.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alikwishatoa wosia kuwa viongozi wetu wana dini lakini serikali haina dini, kama hivyo ndivyo kwa nini viongozi wa dini na wanasiasa wanahubiri siasa kwenye nyumba za ibada?
Kwa kuzingatia mtiririko wa fikra hizo ipo haja kwa Watanzania wenye kulijua lengo la viongozi hao, kutumia zaidi macho ya fikra katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili kuyapa tafsiri matukio yanayojiri na kuitahadharisha jamii isije ikajuta baadaye.
Pia izingatiwe kuwa, hotuba za viongozi zinazotolewa sasa, vitabu na hata magazeti kwa ujumla wake, ni sehemu ya mambo yanayohitaji jicho la fikra la kupata tafsiri halisi.
Kwenye chaguzi za serikali za mitaa tumeona vurugu nyingi, zingine ni za makusudi za kusukwa na watu wenye uroho wa madaraka bila kujali kwamba wanahatarisha usalama na amani ya nchi. Aliyeshindwa anafanywa mshindi na aliyeshinda kwa kura za wananchi anatupwa nje ya uongozi! Hii ni dhuluma ambayo hata Mungu haikubali.
Katika yote haya na yanayofanana na haya, yaliyojiri katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vyombo husika pamoja na mamlaka zilizopo zinatakiwa kusimamia haki.
Dhuluma ni kosa bila ya kujali ni nani anaifanya. Kuiondoa ni kazi ya wanaodhulumiwa kuunganisha nguvu zao na ufahamu wao. Lakini wabunge nao wana wajibu wa kujadili na kuhakikisha haki inatendeka bila kujali itikadi zao. Hatutaki kuona ‘sarakasi’ kama zilizotokea kwenye kikao kilichopita, nina imani kila mmoja atatumia jicho la fikra kuchambua mambo.
Jipu limepasuka siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top