tiko
tiko
Sakata
la kupigwa na kudhalilishwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Prof. Ibrahim Lipumba na wafuasi wengine wa chama hicho, limeibua
mapya, baada wabunge wa upinzani kuja juu wakitaka Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe wawajibike au
Bunge liwawajibishe.
Wengine,
ambao wabunge wanataka wawajibike ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali (IGP), Ernest Mangu, naibu wake (DIGP), Abdukrahman Kaniki,
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa jeshi hilo, Paul Chagonja pamoja na
wote waliohusika na kadhia hiyo.
Pia
wametaka viongozi wengine wa polisi waliohusika ama kutoa amri au
kutekeleza unyama huo wachukuliwe hatua za kisheria na jeshi hilo
lifumuliwe na kuundwa upya.
Walisema
hayo kwa nyakati tofauti wakati wakichangia bungeni mjadala kuhusu hoja
iliyohusu jambo la dharura, iliyotolewa na Mbunge wa Kuteuliwa
(NCCR-Mageuzi), James Mbatia na kauli ya serikali, kuhusiana na
yaliyotokea Januari 27, mwaka huu, Mbagala, jijini Dar es Salaam.
Katika
mjadala huo, Waziri Chikawe pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), George Masaju, walipatwa na wakati mgumu wakijaribu ama kutoa hoja
za kuzuia mjadala kuhusu suala hilo kufanyika bungeni au kuwatetea
polisi na kumkandamiza Prof. Lipumba.
Kila
viongozi hao walipozungumzia mambo hayo, wabunge wa upinzani walikuwa
wakipaza sauti zinazoashiria kuwapinga, kuwakejeli na kuzomea.
LISSU
Wa
kwanza kuchangia mjadala huo ulioruhusiwa na Spika wa Bunge, Anne
Makinda, kwa sharti la kutokutoa kauli zinazoingilia mhimili mwingine wa
dola, alikuwa ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Lissu
kwanza alikosoa kauli ya Masaju ya kulishauri Bunge liache kujadili
kadhia hiyo kwa kuwa kuna kesi iko mahakamani, akisema yeye siyo mshauri
wa Bunge na kwamba, kama linahitaji kushauriwa kisheria litashauriwa na
katibu wa Bunge na wanasheria wake na siyo AG.
Alisema
kauli ya serikali kuhusiana na madhila yaliyotendwa na askari wa Jeshi
la Polisi dhidi ya Prof. Lipumba na wafuasi wengine wa CUF, iliyotolewa
bungeni jana na Waziri Chikawe imejaa uwongo
Alisema
kauli ya Waziri Chikawe imewapa ufahamu kuwa ile kauli iliyowahi
kutolewa bungeni na Waziri Mkuu, Pinda ya kuamuru kila anayekaidi amri
ya polisi kupigwa, ni ya serikali nzima, haikuwa ya bahati mbaya na pia
ni ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Na
kwa sababu ni kauli ya serikali, mtu mwingine, mbaye hapaswi kuendelea
kubaki katika nafasi yake kwa dakika moja zaidi, ni Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda,” alisema Lissu.
Alisema
Jeshi la polisi limetekwa nyara na viashiria vya ufashisti, ambazo
zinaungwa mkono na kubebwa na viashiria vya aina hiyo ndani ya CCM na
serikali.
“Kumbe
tunapigwa siyo kwa sababu tuna makosa, tunapigwa kwa sababu kuna
mafashisti ndani ya polisi, kuna mafashisti ndani ya serikali, hawa
ambao wamesema tupigwe tu,” alisema Lissu.
Alisema katiba ya nchi imetamka wazi kuwa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Pia
alisema sheria ya vyama vya siasa imeeleza wazi kwamba, moja ya haki za
vyama hivyo ni pamoja na kufanya maandamano na mikutano ya hadhara.
"Na
sheria ya Jeshi la Polisi mheshimiwa Spika anayoizungumzia huyu waziri
(anamuonyesha Chikawe) asiyepaswa kuwapo hapo tena, imewapa polisi
mamlaka ya ku-regulate (kudhibiti) mikutano ya hadhara na maandamano,
siyo kuyapiga marufuku," alisema Lissu.
Aliongeza:
"(sheria hiyo) inawaruhusu kukwambia usifanye leo (maandamano), fanya
kesho, usitumie njia hii, tumia njia ile. Haiwapi mamlaka ya kukataza
maandamano na mikutano ya hadhara.”
Alisema
viongozi wote wa vyama vya siasa hakuna asiyekuwa na majeraha, makovu,
ambaye hajakamatwa na kunyanyaswa na Jeshi la Polisi.
Lissu
alisema wengi wa wanasiasa wana kesi nyingi za uwongo zilizotungwa na
Jeshi la Polisi na kwamba, Watanzania wengi wameuawa na jeshi hilo.
Alisema
pia aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel ten,
mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, aliuawa na jeshi hilo kwa amri ya
aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, ambaye
amepandishwa cheo na hivi sasa yuko makao makuu ya jeshi hilo, jijini
Dar es Salaam.
“Watu
wetu wameuawa Arusha 2011, wakauwa Arusha 2012 na 2013, wameuawa
Morogoro, wameuawa Nzega na Jeshi la Polisi. Serikali hii na jeshi lake
imetekwa nyara na fashistic elements (viashiria vya ufashisti),” alisema
Lissu.
Aliongeza:
"Prof. Lipumba amepigwa siyo kwa sababu alikataa (kutii) amri (ya
polisi), alitamka, imeonekana dunia nzima kwenye televisheni. Waziri
mzima unakuja kudanganya umma hapa."
Hivyo,
akasema katika mazingira, ambayo Jeshi la Polisi limetekwa nyara na
viashiria vya kifashisti, serikali inasema “wapigwe tu” na jeshi hilo
limebadilisha hata namba za magari yake kutoka STK kuwa PT “Piga Tu”,
Bunge lazima lichukue hatua.
Pia IGP Mangu, DIGP Kaniki, Chagonja na wote wanaohusika, wawajibike.
Alisema
pia yanahitajika mabadiliko makubwa ya kimfumo wa jeshi hilo na kwamba
ili yapatikane, inahitajika sera na sheria za nchi zilizopo kuhusu
ulinzi na usalama wa raia zitamke wazi wazi kuwa Jeshi Polisi halina
mamlaka ya kuzuia maandamano wala mikutano ya hadhara.
Kutokana
na hali hiyo, alisema umefika wakati wa kuwafukuza kazi wakuu wa wilaya
na wakuu wa mikoa kwenye kamati za ulinzi na usalama akisema hao ndiyo
wamekuwa chanzo cha wapinzani na raia wengine kupigwa.
"(Hao)
ni makada wa CCM, ni wajumbe wa vikao vyote vya CCM kwenye ngazi za
wilaya, kwenye ngazi za mikoa ndiyo wanaowaamuru ma-OCD (wakuu wa polisi
wilaya) watupige, ndiyo wanaowaamuru ma-RPC (makamanda wa polisi mkoa)
watupige," alisema Lissu.
Alisema
Tanzania haiwezi kujiita nchi ya mfumo wa vyama vingi halafu
ikaendekeza mambo ya kikatili, ya kifashisti yaliyofanyika Januari 27,
mwaka huu.
Alisema
Watanzania hivi sasa wanaelekea kwenye uchaguzi mkuu, lakini kwa
ushahidi uliokwishaonekana kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa Jeshi
la Polisi kupiga watu bure, kama kelele hazitapigwa sasa, basi maafa
makubwa yanawasubiri Aprili wakati wa kura ya maoni na Oktoba wakati wa
uchaguzi huo.
MNYAA
Mbunge
wa Mkanyageni (CUF), Mohammed Habib Mnyaa, alisema CUF ilitoa taarifa
kwa Jeshi la Polisi kuhusu maandamano hayo tarehe 22 na siyo 26 kama
ilivyoelezwa na Chikawe, bungeni.
Hata
hivyo, alisema jeshi hilo halikujibu lolote hadi tarehe 27 asubuhi
siku, ambayo maandamano yalipangwa kufanyika, ndiyo waliipelekea CUF
barua ya kuwaarifu kuzuia mkutano wa hadhara na maandamano hayo.
Alisema
polisi walifanya hivyo wakati CUF wakiwa wamekwishafanya maandalizi
makubwa gharama nyingi zikiwa zimetumika, ikiwamo kukodi redio na
televisheni kwa ajili ya kurusha matangazo ya shughuli hizo.
Hata
hivyo, alisema Prof. Lipumba kwa kutii amri ya polisi alikwenda Temeke
Mwisho na kuanza kutoa matangazo ya kuzuia maandamano kufanyika na
kuwatawanya wananchi.
Alisema
kitendo cha Waziri Chikawe kwenda bungeni kueleza kitu tofauti ni jambo
linalosikitisha na kutia aibu kwa Bunge, ambalo linadanganywa, huku
wabunge wakipiga kimya.
Aliungana
na Lissu kutaka Pinda ajiuzulu kutokana na kauli yake “wapigwe tu”
vinginevyo, arudi bungeni kwenda kuifuta na pia jeshi la polisi
livunjwe.
MKOSAMALI
Mbunge
wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali, alisema hashangazwi na
Jeshi la Polisi kuwatendea hayo raia, kwani ripoti ya Jumuiya ya Madola
imeeleza bayana kuwa bado lina mifumo ya wakoloni ya kuhakikisha
wanabaki madarakani.
NASARI
Mbunge
wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nasari, alisema Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora ilipendekeza polisi wachukuliwe hatua, lakini
hadi leo hakuna aliyechukuliwa hatua.
MASUDI
Mbunge
wa Tumbe (CUF), Masudi, alisema Prof. Lipumba ni sawa na Rais Jakaya
Kikwete, kwa kuwa wote ni wenyeviti wa vyama vya siasa, hivyo
anawashangaa polisi kushindwa kumpa heshima inayostahili na kuwa Waziri
Chikawe hafai kuongoza Jeshi la Polisi, hivyo akae pembeni.
SALIM
Mbunge
wa Mtambile (CUF), Masudi Abdallah Salim, aliitaka serikali kueleza
amri ya kumshughulikia Prof. Lipumba na wananchi inayoelezwa kuwa
ilitoka juu, ni sehemu gani?
MBOWE
Mbunge
wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, kwa kuwa Rais na waziri mkuu
wameshindwa kuchukua dhidi ya polisi wanaowafanyia madhila wananchi,
iundwe kamati teule ya Bunge kushughulikia tatizo hilo.
SHEKIFU
Mbunge
wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu, alisema vurugu zote zinazotokea chanzo
chake ni watu kuvunja sheria na kwamba, amebaini kuwapo na njama za
kutaka kulitumia Bunge kama chombo cha kubadilisha mambo, hivyo akasema
kamwe hawawezi kukubali kuona amani inavunjika, badala yake watapambana.
Hata hivyo, alisema kama kuna polisi waliotumia nguvu kubwa, basi wachukuliwe hatua.
NKUMBA
Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba, alishauri wahusika wote kuchukuliwa hatua kwani hakuna mbunge anayeweza kutetea maovu.
KASSIM
Mbunge
wa Chwaka (CCM), Yahya Kassim Issa, aliwalaumu CUF kutaka kufanya
maandamano hayo kukumbuka watu waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi
visiwani Zanzibar, Januari 27, 2001, huku wakishindwa kufanya hivyo kwa
askari polisi aliyechinjwa katika tukio nilo.
SADIFA
Mbunge
wa Donge (CCM), Sadifa Juma Khamisi, alisema haki ya kuandamana ipo
kwenye katiba, lakini haipaswi kutumiwa vibaya, kwani katiba hiyo hiyo
inaeleza kuwa hakuna haki isiyokuwa na mipaka.
Kauli
hiyo nusura ichafue hali ya hewa bungeni baada ya wabunge wa CUF kumjia
juu kutaka kumshughulikia kabla ya Spika Makinda kuingilia kati na
kumtaka afute kauli yake hiyo.
LUSINDE
Mbunge
wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, alipinga hoja ya kutaka viongozj
nao kujiuzulu kwa madai kwamba, kitendo cha polisi kimeonyesha uimara
ilionao serikali ya CCM, ambayo mara kwa mara wapinzani wamekuwa wakiita
dhaifu.
Awali,
akisoma kauli ya serikali, Waziri Chikawe alisema yaliyomkuta Prof.
Lipumba, yametokana na kukaidi amri ya polisi iliyozuia kuandamana.
Wakati Chikawe akisoma kauli hiyo ya serikali, wabunge wa upinzani walikuwa wakizomea na kumwita mwongo.
Hata hivyo, alisema katika Jeshi la Polisi kuna kitengo cha malalamiko, hivyo kama kuna mtu ana malalamiko, ayawasilishe huko.
Hali
ya kuzomea na kutoa maneno ya kumpinga, ilijitokeza wakati Masaju
aliposimama bungeni na kulishauri Bunge kwamba, halipaswi kujadili suala
hilo kwa kuwa liko mahakamani na kwamba, kufanya hivyo, ni kukiuka
katiba ya nchi.
Hata
hivyo, Spika Makinda aliamua mjadala huo uendelee, lakini wachangiaji
wajiepushe kutoa kauli zinazoingilia mihimili mingine ya dola.
WAFUASI 29 WA CUF KORTINI
Katika
hatua nyingi, Shabani Ngurangwa na wenzake 29, ambao ni wafuasi wa CUF,
jana walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na
mashitaka matatu likiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko na kukaidi amri
halali ya Jeshi la Polisi nchini.
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Emmilius Mchauru.
Upande
wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Joseph Maugo, akisaidiana
na Hellen Moshi, ulidai kuwa Januari 27, mwaka huu eneo la Temeke jijini
Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la jinai.
Katika
shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza katika ofisi ya
CUF, iliyopo karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke, jijini, washtakiwa
walifanya mkusanyiko usio halali kwa nia ya kufanya maandamano kwenda
Mbagala.
Maugo
alisema katika shitaka la tatu kuwa, siku ya tukio la pili washtakiwa
bila kujali tangazo lililotolewa na jeshi hilo la kuzuia wasifanye
maandamano hayo, lakini walikaidi na kufanya maandamano kwenda Zakhem
Mbagala.
Mbali
na Ngurangwa, washtakiwa wengine ni, Shabani Tano maarufu kama kasakwa
(29), shabani Polomo (40), Juma Matar (54), Mohamed Kirungi (40),
Athuman Ngumwai (40), Shaweji Mohamed (39), Abdul Juma (40), Hassan Said
(37), Hemed John (49), Mohamed Ibrahim (31), Issa Hassan (53) na Allan
Ally (53).
Wengine
ni, Kaisi Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Alawi Msenga (53), Mohamed
Matutuma (33), Salehe Ally (43), Abdul Hatibu (34), Bakari Maliya
(43)Abdallah Ally (32), Said Mohamed (40), Salima Mwafisi, Salehe Rashid
(25), Abdallah Said (45), Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42),
Athumani Said (39), Dickson Lesson (37) na Nurdin Msati (37).
Washtakiwa
wote walikana mashitaka hayo. Hakimu Mchauru alisema washtakiwa
watakuwa nje kwa dhamana kwa kusaini hati ya dhamana ya Sh. 100,000 kila
mmoja na mdhamini mmoja atakayesaini kiasi hicho cha fedha.
Washtakiwa wamepelekwa mahabusu hadi leo kesi hiyo itakaposikilizwa dhamana yao.
CUF WALAANI
Wakati
huo huo, CUF kimelaani vikali Jeshi la Polisi nchini kumkamata,
kumdhalilisha na kumpiga Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba,
pamoja na wafuasi wake katika vurugu zilizotokea Januari 27 baina ya
jeshi la polisi na wafuasi wa chama hicho.
Pia kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha viongozi wote ambao kwa namna moja ama nyingine walihusika katika tukio hilo.
Makamu
Mwenyekiti CUF Taifa, Juma Duni Haji, alisema Jeshi la Polisi
linatekeleza vitendo hivyo kutokana na mashinikizo ya kisiasa.
Haji
alisema ni jambo la kushangaza kuona jeshi hilo linashindwa kutumia
nguvu kulinda usalama katika maandamano, lakini linatumia nguvu kubwa
kupambana na kupiga raia wasio na silaha.
Alisema
ni vema rais akaliangalia na kulishughulikia suala hilo ikiwa ni pamoja
na kuweka mazingira sawa ya ushindani wa kisiasa, katika kipindi hiki
cha kuelekea uchaguzi Mkuu ili kuepuka kuiingiza nchi katika mapigano ya
wenyewe kwa wenyewe.
Kadhalika,
aliongeza kuwa CUF kitaendelea na msimamo wake wa kufanya maandamano na
mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya
kuwaenzi na kuwakumbuka wenzao waliojitoa mhanga kwa ukombozi wa
kidemokrasia nchini.
tiko
tiko
Post a Comment