tiko
tiko
Aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samweli Sita akisalimiana na rais Jakaya Mrisho Kikwete.
MWAKA huu
unaingia katika historia ya nchi yetu moja kwa moja pasipo maswali.
Tofauti na wakati mwingine, mwaka huu una uwezekano wa kupitisha matukio
makubwa mawili, ambayo kwa namna yoyote, yanaweza kuharibu au
kuimarisha taifa letu lenye umri wa miaka 50 tangu lipate uhuru wake.
Tukio moja tumelizoea kwa sababu
tunalipitia kila baada ya miaka mitano, ambalo linahusu uchaguzi mkuu wa
kutupatia rais, wabunge na madiwani mpya kwa kipindi cha miaka mitano
ijayo. Hii itakuwa ni mara ya tano kwa wananchi kujipanga vituoni
kufanya uchaguzi tangu tuanze mfumo wa vyama vingi, 1992.
Ingawa tangu tuanze kufanya hivyo mara
zote Chama Cha Mapinduzi kimeibuka kidedea katika nafasi ya urais, kama
inavyotarajiwa tena safari hii, lakini uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na
changamoto nyingi, kwani kwa mara ya kwanza, CCM inahisi upinzani wana
nafasi ya kushika dola, kutokana na kuimarika kwa kambi ya upinzani na
migawanyiko ya ndani kwa ndani miongoni mwa makada wake.
Ni uchaguzi unaokuja huku wapinzani
wakitangaza kuungana kwa kusimamisha mgombea mmoja kwa kila nafasi, kwa
kila jimbo na kata, kupitia umoja wao wa Ukawa. Katika nchi ambayo
imeamua kufuata misingi ya demokrasia, ya kuwaachia wananchi kumchagua
kiongozi wanayemtaka, lolote linaweza kutegemewa katika kinyang’anyiro
hiki kinachotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu baada ya Rais Kikwete
kumaliza muda wake.
Lakini ukiachana na tukio hili, lipo
lingine ambalo kinadharia linaonekana ni dogo lakini kiuhalisia ni kubwa
na muhimu kuliko hata Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Hili linahusu kura ya
maoni ya Katiba Inayopendekezwa ambayo katika kalenda, inaonyesha kuwa
wananchi watapaswa kupiga kura ya kuikubali au kuikataa Aprili 30, mwaka
huu.
Wote tunajua kuwa upitishwaji wa Katiba
hii katika Bunge Maalum la Katiba lililokuwa likiongozwa na Mhe. Samuel
Sitta haukuwa mzuri, kwa namna ile tuliyoitarajia baada ya baadhi ya
wajumbe kususia mchakato wake kwa madai ambayo tunayafahamu. Sitaki
kurejea nyuma, juu ya uhalali wake, kwa sababu ninajua kwa mujibu wa
sheria, Katiba Inayopendekezwa ni halali.
Tatizo langu limekuwa juu ya namna
mamlaka zinazohusika zinavyolichukulia jambo hili kirahisi, kiasi kwamba
wanaacha mambo ya msingi bila sababu zenye hoja. Kwa mfano, tunahitaji
kujua idadi ya wananchi watakaokuwa na hadhi ya kuipigia kura katiba
hii, ambao haina namna wanavyoweza kupatikana pasipo uandikishaji upya
kufanywa na Tume ya Uchaguzi yaani NEC.
Hadi ninapoandika makala haya, bado
hakuna hatua zilizo wazi juu ya nini kinafanyika kuhusu uandikishwaji
huu. Lakini achana na hilo, kuna hili la kutoa elimu kwa wananchi juu ya
nini kilichomo ndani ya katiba inayoelezwa kuwa ni yao, ili waijue,
wajiandae kuikataa au kuikubali. Zoezi la kutoa elimu hii, haliwezi
kufanywa kwa kutoa makala magazetini, linatakiwa kufanywa ‘live’ ili
watu wawe na nafasi ya kuuliza na kujibiwa maswali.
Labda mamlaka zinapaswa kutambua kuwa
suala hili siyo la kulifanyia majaribio wala masihara, kwa sababu halina
hati miliki ya chama chochote cha siasa. Kama kuna watu wanadanganyana
kuwa Watanzania wanaburuzika, ni sawa, lakini muhimu kwao kutambua kuwa
wataburuzika leo, siyo kila siku.
Elimu ni lazima itolewe ili wananchi
wapige kura itakayosukumwa na dhamira ya mioyo yao, tusiwafanye wapige
kura kwa laghai, kwa sababu watakapogundua kuwa watawala waliwalaghai,
inaweza kutuletea matatizo kuliko kama tungeweza kuzuia jambo hili leo,
tena pasipo gharama yoyote.
Kama tunadhani tuna mambo mawili makubwa
na muhimu, basi moja lisubiri. Hili la Katiba Inayopendekezwa lisubiri,
tufanye uchaguzi, tuwapate viongozi wetu wapya, wakae na kuanza
mchakato wa kura ya maoni, kwa sababu tutakuwa na muda wa kutosha,
tofauti na hili la zimamoto linaloonekana kutayarishwa kufanywa na
watawala wetu. Kinga ni bora kuliko tiba!
tiko
tiko
Post a Comment