tiko
tiko
MJADALA juu ya ukwapuaji wa zaidi ya Sh. 321 bilioni, kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow ndani ya Benki Kuu (BoT), ungali mbichi.
Aliyetegemewa
kufunga mjadala huu, kwa kushughulikia wezi halisi wa fedha hizo,
ameishia kutetea uhalifu, kuhalalisha wizi, kubeba watuhumiwa na
kupotosha umma juu ya waliohusika na kilichotendeka.
Akihutubia
taifa juzi Jumatatu kupitia kilichoitwa, “mkutano wa rais na wazee wa
mkoa wa Dar es Salaam,” Rais Dk. Jakaya Kikwete, alikiri kuwapo
udanganyifu katika kufikia utoaji wa fedha hizo.
Alikiri
baadhi ya nyaraka kughushiwa. Akakiri kuwa kampuni ya Pan African Power
Solution (PAP), imekwepa kodi ya serikali baada ya kulipwa fedha kutoka
kwenye akaunti ya Escrow.
Akajitetea
kuwa serikali inaitafuta kampuni ya MECHMAR iliyodaiwa kuuza asimimia
70 ya hisa zake katika kampuni ya Independent Power Tanzania Limited
(IPTL) kwa PAP ili iweze kulipa kodi hiyo.
Kampuni
ya IPTL ni muungano wa kampuni mbili – VIP ya Rugemalira iliyokuwa
inamiliki asilimia 30 ya hisa na MECHMAR ya Malaysia iliyokuwa na
asilimia 70 za hisa.
Rais
alikiri kuwa aliyepewa fedha na serikali – PAP –hakuwa na sifa za
kuvuna alichopata. Akakiri kuwa mmoja wa wanahisa wa IPTL, James
Rugemalira, alicholipwa kilikuwa halali kwa mujibu wa sheria.
Akakiri fedha zake zililipiwa kodi ya serikali, tena kama ilivyoainishwa na mahakama.
Rais
alikiri kuwa serikali yake haikufanya uchunguzi yakinifu, kuhusu
historia, uhalali, sifa na uwezo wa kampuni ya PAP, katika uwekezaji wa
umeme, ununuzi wa mitambo na mtaji.
Hata
hivyo, pamoja na kukiri yote hayo hadharani, alishindwa kuchukua hatua
dhidi ya wazembe na waliovunjaji sheria walioko serikalini.
Rais
aliishia kumfuta kazi, Prof. Anna Tibaijuka, waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, ambaye kwa namna yoyote ile, hakuhusika na wizi
uliotokea.
Haikutarajiwa
kiongozi mkuu wa nchi kama hii, ambaye ana mamlaka makubwa ya kidola –
awezaye kuvunja Bunge, kumtia mtu kizuizini, kuridhia mtu kunyongwa na
kutangaza nchi kuingia vitani – kutishwa na wasiokuwa na dola.
Kitendo
cha rais kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wizi huu, kimethibitisha
madai ya wananchi, baadhi ya vyama vya siasa makini vya upinzani na
taasisi za kiraia (NG’OS), kuwa rais “amekusudia kutenda uhalifu kwa
kulinda wezi.”
Kuhusu
kitendo cha ukwepaji kodi kilichofanywa na PAP, rais alikiri kuwa
mamlaka ya mapato (TRA), walidai kodi kwa barua kwenda BoT.
Bali,
kama PAP aliambiwa asilimlipe Rugemalira mpaka atakapolipa kodi, kwa
nini hakuambiwa asimlipe MECHMAR mpaka atakapolipa kodi?Rais Kikwete
amesema, Prof. Tibaijuka amepokea fedha kutoka kwa Rugamalira.
Amethibitisha kuwa fedha hizo zilikuwa mchango kwa ajili ya shule ya
Johanssen ya jijini Dar es Salaam.
Rais
hakusema Prof. Tibaijuka hana shule. Hakusema fedha hazipelekwa shule.
Hakusema fedha zilikuwa chafu. Amekiri fedha za Rugemalira zililipiwa
kodi; Katibu Mkuu Kiongozi wa zamani, Balozi Paulo Rupia, amethibitisha
kupokelewa kwa fedha hizo katika shule ambayo yeye ni mlezi wake.
Rais
Kikwete amesema, mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow
yalilipwa kwa PAP baada ya Mahakama Kuu kutoa “amri” tarehe 5 Septemba
2013. Hii siyo kweli.
Hakuna
amri ya mahakama inayoelekeza fedha kutolewa. Kinachoitwa amri ya
mahakama, kilikuwa ni kumaliza ugomvi wa wanahisa wa IPTL. Siyo mgogoro
wa Escrow uliotokana na tozo halali ya uwekezaji na mtaji katika
uwekezaji. Hiyo ndiyo amri ya mahakama.
Hakujawahi
kutolewa amri nyingine yoyote ya kuruhusu fedha kutolewa katika Akaunti
ya Escrow kulipwa PAP au IPTL. Wala mahakama haikuamuru kutolewa fedha
hizo na serikali kama “mali iliyotekwa kwenye vita.”
Mahakama
haikusema serikali ilipe fedha kutoka Akaunti ya Escrow, bila
kujiridhisha na uhalali wa ununuzi wa hisa za kampuni ya IPTL, kwenda
kwa PAP.
Haikuzuia
serikali kuhoji kufanyika kwa malipo hayo, wakati bado kuna mgogoro
kati ya serikali na Benki ya Standard Chartered (SCB) Hong Kong (BSC
–HK).
Mahakama
haikuagiza, wala haijaagiza serikali kutohoji, kwa nini malipo hayo
yafanyike, wakati benki ya Standand Chartered, bado inaendelea
kung’ang’ana mahakamani.
Benki
inadai kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na fedha zilizopo kwenye
akaunti ya Escrow, zinastahili kuwa zake. Mpaka sasa, benki hii bado
inaendelea kuhangaika mahakamani kudai haki yake.
Aidha,
rais anajua kuwa mahakama haikuamuru fedha hizo kutolewa kwa PAP kwa
kuwa hilo halikuwa miongoni mwa hoja zilizokuwa kwenye meza mahakamani.
Hata
yeye amekiri katika hotuba yake pale aliposema, “…serikali haikuona
umuhimu wa kurudi mahakamani kufanya marejeo juu ya uamuzi iliotoa.”
Hakuna
shaka kama mahakama ingeelezwa vizuri kuhusu kuwapo kwa mgogoro kati ya
IPTL na benki ya Standard Chartered na Tanesco na benki hiyo,
isingeruhusu PAP kununua hisa za IPTL.
Amri ya mahakama iliyopo na ambayo rais amekwepa kuzungumzia, ni ile ya 17 Januari 2014.
Katika
amri hii, mahakama iliamuru kampuni ya PAP kuilipa VIP Engineering
Limited. Hii ni baada ya Rugemalira kushitaki karibu serikali yote
mahakamani.
Rugemalira
aliiambia mahakama katika hati yake ya kiapo kuwa yote yaliyofanyika,
ikiwamo kutolewa kwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, ulikuwa ni
“utapeli mtupu.”
Alisema, utapeli huu ulifanywa na serikali ya rais Kikwete, BoT, Benki ya Stanbic na PAP.
Kutokana na uzito wa madai ya Rugemalira, PAP na serikali zilinywea. Zikakubali kuingia katika usuluhishi wa mahakama.
Habari
zinasema, suluhisho hilo halikuwafurahisha baadhi ya watu ndani ya
serikali. Zikaandaliwa kampeni chafu dhidi ya Rugemalira na kampuni
yake. Akaitwa mwizi.
Kazi
ya kusakama wote waliopewa fedha na Rugemalira ikafanyika nchi mzima.
Waliopewa mgawo, wakageuzwa wezi. Walioshiriki katika wizi, waliokwapua
mabilioni ya shilingi kutoka benki ya Stanbic na waliobeba fedha kwa
magunia, mifuko ya plasitiki na vikapu, wakatakatishwa.
Rais
Kikwete amerejea kauli ya serikali yake bungeni, mwezi uliopita, kwamba
fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow hazikuwa mali ya
serikali. Amedai kuwa zilikuwa mali ya IPTL.
Amesema,
ziliwekwa kwenye Akaunti ya Escrow na Tanesco badala ya kulipwa moja
kwa moja kwa kampuni IPTL, kutokana na kuibuka mgogoro wa tarifu na
malipo ya gharama za kuweka mtambo – Capacity Charge. Hili nalo siyo
kweli. Sababu ni mbili.
Kwanza,
fedha hii zilizokuwa zikisubiri kumalizika mgogoro kati ya Tanesco na
IPTL, haziwezi kuwa mali ya IPTL, kabla ya mgogoro kumalizika.
Katika
hotuba yake hiyo, rais amekiri kuwa mpaka fedha zinatolewa, mgogoro huo
ulikuwa haujamalizika. Tanesco bado inaendelea kudhulumiwa kwa kutozwa
kiwango kikubwa cha malipo ya Capacity Charge.
Hakika, hotuba ya Rais Kikwete haina jipya. Imeishia kuchochea mgogoro na kuibua yale ambayo hayakufahamika.
Mathalani,
Rais Kikwete amesema azimio la Bunge lililotaka serikali kutaifisha
mitambo ya IPTL, halitekelezeki. Amedai kulitekeleza azimio hilo,
kutasababisha kukimbiza wawekezaji nchini.
Lakini
imefahamika kuwa yule ambaye rais na serikali wanaita “muwekezaji mpya
katika IPTL,” hana sifa ya kuitwa mwekezaji. Huyu aweza kuitwa,
“mchuuzi.”
Ripoti
ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeeleza
Harbinder Singh Sethi, alighushi nyaraka. Siyo mwadilifu. Ni laghai na
mdanganyifu.
Harbinder
Singh amelipwa fedha asizostahili. Hadi anamaliza kuchota mabilioni
hayo ya shilingi na akaunti ya Escrow inaamuriwa kufungwa, alikuwa
hajanunua asilimia 30 ya hisa za VIP Engineering katika IPTL.
Wakati analipwa fedha hizo alikuwa hajawa mmiliki halali wa hisa katika MECHMAR.
Hii maana yake ni kwamba, wakati PAP inachotewa mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Escrow, hakuwa mmiliki halali wa IPTL.
Hadi
fedha zinatolewa, alikuwa hajasajili asilimia 70 ya hisa alizodai
amenunua kutoka kampuni hiyo ya Malaysia kwa Wakala wa Serikali na
Kampuni (BRELA).
Kwa hali hiyo, uamuzi wa serikali wa kutaifisha mitambo ya IPTL, hauwezi kufukuza wawekezaji nchini.
Badala
yake, kitendo hicho kitaongeza wawekezaji, kitarejesha heshima ya nchi
na kingerudisha matumaini mapya kwa wananchi kwa serikali na chama
kilichoko Ikulu.
Lakini
kitendo cha kulea wezi na matapeli wengine wanaokuja kwa kofia ya
“uwekezaji,” kitalifanya taifa hili kuendelea kudharauliwa.
Kuhusu
azimio la Bunge lilitoka mamlaka ya uteuzi kuchukua hatua dhidi ya
Katibu Mkuu wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Rais Kikwete
amesema suala hilo ameliacha kwa mamlaka ya nidhamu.
Mamlaka ya nidhamu ambayo rais amesema amekabidhi jukumu hilo, ni Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue.
Lakini
uteuzi wa makatibu wakuu, haufanywi na katibu mkuu kiongozi. Unafanywa
na rais. Kitendo cha rais kulikabidhi suala la Maswi kwa katibu mkuu
kiongozi, ni kukwepa wajibu wake.
Naye
Prof. Sospeter Muhongo, aliyetuhumiwa na Bunge kuwa dalali wa
kufanikisha wizi huo, rais amedai, uchunguzi bado unaendelea. Ameeleza
anayefanya kazi ya uchunguzi dhidi ya Prof. Muhongo, yuko nje ya nchi
kikazi.
Ni muhimu Rais Kikwete akafahamu kuwa hakuna sabuni ambayo itaweza kumsafisha Prof. Muhongo katika tuhuma hizi.
Jitihada zozote za kumtetea zitaishia kudhoofisha serikali na rais binafsi.
Si
hivyo tu. Sakata la wizi katika akaunti ya Escrow haliwezi kumalizika
bila rais kueleza hatua ambazo zitachukuliwa dhidi ya maofisa wa ikulu
“waliopata mgawo” kutoka kwa Rugemalira.
Sababu
zilezile na makosa yaleyale ambayo rais amemtwisha Prof. Tibaijuka,
anapaswa kuwatwisha pia maofisa wake wa ikulu waliolipwa na Rugemalira.
Wala
sakata hili haliwezi kufungwa bila kutaja majina ya waliopokea kitita
cha kati ya Sh. 800 milioni na Sh. 5 bilioni, kutoka benki ya Stanbic.
Yawezekana wakafichwa leo. Lakini hakuna mwenye ubavu wa kuficha milele na milele.
Ikiwa
mkataba wa IPTL uliofungwa miaka 20 iliyopita, wakati Rais Kikwete
akiwa waziri wa nishati na baadaye waziri wa fedha – bado unamtafuna
mpaka sasa – hakuna awezaye kuzuai kufahamika kwa waliochota fedha
Stanbic.
Watajulikana tu – kama si leo, kesho.
tiko
tiko
Post a Comment