tiko
tiko
Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Wakazi
wa mkoa wa Lindi wametakiwa kushikamana kwa pamoja, kufanya kazi kwa
bidii na kuzitumia rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo.
Rai
hiyo imetolewa jana Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete
wakati akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mitwero Stendi
Kata ya Rasibura wilayani humo.
Mama
Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema mkoa
wa Lindi umejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwa ni pamoja na zao la
korosho, ardhi yenye rutuba, bahari na gesi lakini bado kuna
changamoto zinazowakabili wananchi na hivyo kukwamisha maendeleo yao.
Alizitaja
changamoto hizo kuwa ni pamoja na elimu kwani baadhi ya wanafunzi
wafikapo darasa la tano wanaacha shule kwa ajili ya utoro, mimba za
utotoni na vijana kutokufanya kazi kwa bidii.
“Kuna
baadhi ya watoto wakifika darasa la tano wanaanza tabia ya utoro
hakikisheni wanakwenda shule kusoma kwani elimu itawasaidia katika
maisha yao, msikubali waache shule. Kutokana na umri wao mdogo wanaona
raha kuacha shule na kwenda kucheza lakini wakifika umri wa utu uzima
ndiyo watakapoona umuhimu wa elimu”.
Maisha
bora kwa kila mtanzania yanawezekana ikiwa kila mtu atapata elimu
itakayomsaidia katika maisha yake, wakati shule za Sekondari za Kata
zinajengwa kuna baadhi ya watu walitubeza na kuziita majina ya ajabu
ikiwa ni pamoja na shule za Yeboyebo lakini shule hizi zimewasaidia
watoto wengi kutoka familia maskini ambao wameweza kupata elimu”,
alisema Mama Kikwete.
Kuhusu
tazizo la mimba za utotoni alisema ni hatari kwa maisha ya Mama na
mtoto lakini kama kijana atasoma mimba zitaepukika, jukumu la wananchi
ni kuhakikisha watoto wao wanasoma kwa bidii na kutokubali kupewa
mimba ambazo zitawakatisha masomo.
Kwa
upande wa vijana MNEC huyo aliwahimiza kuangalia mstakabali wa maisha
yao na kutumia muda wao kufanya kazi kwa bidii kwa kufanya hivyo
watapata maendeleo kwani hizi sasa kuna baadhi ya vijana wakati wa
asubuhi wanaacha kwenda shamba kulima na kucheza Pool kwa kufanya hivyo
ni vigumu kupata maendeleo.
“Vijana
wengine wanatumia madawa ya kulevya na kuvuta sigara wanajua kwa
kufanya hivyo ndiyo ujanja kitendo ambacho siyo ukweli, bali unaharibu
afya yako na kujirudisha nyuma kimaendeleo. Kama wewe kijana unahitaji
kuwa na maisha bora ni lazima uachane na vitendo hivyo na kufanya kazi”,
alisisitiza.
Licha
ya kufanya mkutano huo wa hadhara Mama Kikwete pia alifanya vikao na
wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM matawi ya Mbanja, Mabano na Mitwero
Stendi na kuwataka wajumbe hao kuwapa vijana nafasi za uongozi pale
watakapojitokeza kugombea nafasi hizo.
Pia
aliwahimiza wajumbe hao wakiwemo vijana, wanawake na wanaume kujitokeza
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika hapo mwakani ili kuwe na ushindani wa kutosha ndani ya chama.
Mama
Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kichama na katika
mkutano wa hadhara aligawa kadi kwa wanachama wapya 23 walijiunga na
Chama Cha Mapinduzi.
tiko
tiko
Post a Comment