tiko
tiko
Askari wawili wa Jeshi la Polisi katika Kituo cha Ikwiriri wilayani Rufiji mkoani Pwani, wameuawa baada ya kushambuliwa kwa silaha na majambazi, waliovamia kituo hicho na kuiba silaha baada ya kufanikisha mauaji.
Kutokana
na tukio hilo, Jeshi la Polisi liko katika msako mkali, huku Mkuu wa
jeshi hilo, IGP, Ernest Mangu akitangaza donge nono la Sh milioni 20 kwa
watakaofanikisha kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo na silaha.
Akizungumza
na waandishi wa habari kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, Ikwiriri,
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema majambazi hao
walitumia silaha kuwaua askari hao.
Kamanda
Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 8 usiku katika
kituo hicho cha Polisi cha Ikwiriri. Aliwataja askari waliokufa kuwa ni
mwenye namba E 8732 Koplo Edgar Milinga na WP 5558 Konstebo Judith
Timothy.
Alisema
licha ya kufanya mauaji hayo, pia majambazi hayo yalipora silaha tano
za moto aina mbalimbali, zikiwemo SMG 2, SAR 3 na risasi 60. Pia,
walichukua mabomu mawili ya machozi.
Kamanda alisema kuwa pia watu hao, waliharibu kwa kulipiga risasi gari la Polisi la kituo hicho lenye namba za usajili PT 1965.
Msemaji
wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Bulimba alisema tukio hilo la
kusikitisha, halitapita hivi hivi, bali jeshi limeelekeza nguvu zake
huko kuhakikisha wahusika wanakamatwa.
Alisema
tayari Mkuu wa Jeshi ametangaza dau la Sh milioni 20. Pia, alisema
katika kuongeza kasi ya msako, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul
Chagonja akiwa na timu ya makachero, yuko eneo la tukio kuhakikisha
wahusika, kokote waliko, wanasakwa na kutiwa mbaroni.
“Hili
ni sawa na tukio la kigaidi, Jeshi la Polisi litakabiliana na wahusika
kokote waliko, lazima wakamatwe. Kikubwa tunaomba ushirikiano wa
wananchi, tunaamini wengi ni raia wema na watalisaidia jeshi kufanikisha
jukumu hilo la kukomesha uhalifu nchini,” alisema Advera.
Aliwataka
wananchi kuelewa Jeshi la Polisi liko imara, hivyo wasiwe na hofu
yoyote juu ya tukio hilo. Alisisitiza kuwa wahusika wote watadhibitiwa
na kushikishwa adabu.
tiko
tiko
Post a Comment