tiko
tiko
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) imetangazwa kufilisika, kutokana na kutokuwa na mtaji baada ya mwekezaji, Kampuni ya simu za mkononi ya Bharti Airtel, kushindwa kuwekeza kwa miaka 14.
Kutokana
na hatua hiyo, Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC)
imeamua kupeleka suala hilo bungeni ili kuweka mipango ya kimkakati
kuifufua kampuni hiyo. Kwa kuanzia, Msajili wa Hazina amepewa kazi ya
kufanya tathmini ya kina.
Hayo
yalibainika jana katika kikao cha uongozi wa kampuni hiyo na kamati
hiyo, inayoongozwa na Kabwe Zitto, iliyotaka kufahamu maendeleo ya
kampuni hiyo, ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikikabiliwa na changamoto
kadhaa katika ushindani wa huduma za simu hususani katika siku za
mkononi.
Umekuwepo
pia mvutano mkali baina ya Serikali na Kampuni ya simu za mkononi ya
Bharti Airtel kuhusu hatima ya asilimia 35 ya hisa, ambazo kampuni hiyo
inamiliki ndani ya Kampuni ya TTCL.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Dk Kamugisha Kazaura aliieleza Kamati ya
Bunge kuwa kutokana na hasara kubwa ya kiasi cha Sh bilioni 334.5 mpaka
kufikia mwaka 2013 na kushindwa kukopesheka huku ikibaki na mtaji hasi
wa Sh bilioni 87.9, kwa sasa ni mufilisi.
Alisema
hatua hiyo, inatokana na mbia mwenye hisa kwa asilimia 35, kutofanya
uwekezaji mkubwa tangu waingie ubia mwaka 2001, jambo ambalo
limesababisha pia uchakavu wa miundombinu na kupungua kwa ubora wa
huduma.
Kutokana
na hatua hiyo ya kutokuwekeza, kampuni hiyo ilimtaka mwekezaji huyo
kuondoa umiliki alionao, ambapo Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru
alisema kampuni hiyo ya India, ambayo ni Kampuni mama ya Airtel
Tanzania, inataka ilipwe Sh bilioni 14 licha ya kuwa haijawahi kuwekeza
chochote ndani ya TTCL, kama ilivyo kwa watangulizi wake; Celtel
Tanzania, Celtel International na Zain.
Lakini,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa
Patrick Makungu alisema Baraza la Mawaziri limeunda jopo la majadiliano
na mwekezaji huyo, kuzungumzia gharama za kumlipa ili kuondoka katika
kampuni hiyo ya TTCL na hawana taarifa ya kiwango hicho cha fedha
kilichotajwa.
“Mitambo
mingi ni chakavu, kutokana na kutowekeza katika teknolojia za kisasa
kwani kampuni nyingine za simu za mkononi kila mwaka zimekuwa zikiwekeza
dola milioni 100 kuboresha huduma,” alisema.
Alisisitiza
kuwa kwa mwaka 2012, mapato ya kampuni hiyo yalikuwa Sh bilioni 92.4
lakini mwaka uliofuata yaliongezeka kwa asilimia moja na kufikia Sh
bilioni 93.6 baada ya jitihada mbalimbali katika kukuza teknolojia.
Akizungumzia
hasara ya kampuni hiyo, alisema mwaka 2012 hasara ilikuwa Sh bilioni
20.8 na mwaka 2013 ilikuwa Sh bilioni 16.2, jambo linalosababisha hali
ya fedha kuwa mbaya na kushindwa kukopesheka kutokana na serikali
kushindwa kuwadhamini.
Alisema asilimia 50 ya miundombinu ya kampuni hiyo ni chakavu huku wakitegemea mapato kwa kutumia wateja.
Alitaka
serikali kuwafutia deni la Sh bilioni 76 wanazodaiwa baada ya
kukopeshwa serikali ilipouza hisa zake na kutumia kulipa wafanyakazi
waliostaafu.
Dk
Kazaura alisema uhaba wa fedha, pia unasababishwa na madeni mengi
kampuni hiyo inadai idara na taasisi ya serikali, ambapo hadi kufikia
Septemba 2014 walikuwa wakiidai Sh bilioni 3.2 na dola za Marekani
milioni mbili, hivyo waliomba Hazina kusaidia kwa kukata taasisi na
idara hizo moja kwa moja kwenye mafungu yao.
Alisema
licha ya changamoto hizo, bado wanadaiwa na wazabuni, Mamlaka
Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine za kimataifa, jambo
lililofanya TCRA kuwaagiza kulipa madeni hayo hadi Oktoba 31,mwaka jana,
vinginevyo watafutiwa leseni .
Lakini,
pia alisema wanaiomba serikali kuangalia namna ya kuwaongezea mtaji
kufikia dola milioni 711 ili kufufua shirika, ikiwa ni pamoja na
kuwamilikisha rasmi mkongo wa taifa wa mawasiliano, ambao kwa sasa
wanausimamia baada ya kukamilika kwa awamu mbili.
“Pia
tunahitaji kurekebisha muundo wa kampuni kutokana na kuwa na
wafanyakazi wengi wanaofikia 1,550 na wengi wao ambao ni asilimia 50
wana miaka zaidi ya 50 na elimu isiyozidi kidato cha nne, hivyo lazima
kuchambua watakaoweza kuendana na teknolojia na ikibidi wengine
kuwapisha wenye uwezo,” alisema.
Waliomba
serikali pia kuangalia suala la taratibu na sheria za manunuzi ili
kusaidia ushindani wa kibiashara na kampuni nyingine za simu za
mikononi, ambazo ni binafsi na taratibu zake hazichukui muda mrefu.
Alizungumzia
pia suala la gharama kubwa za intaneti ya TTCL kuwa inatokana na ubora
wake na uhakika kwa huduma zinazotolewa huku akitaka wananchi kuwaunga
mkono katika huduma hiyo.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Kabwe Zitto alisema watapeleka bungeni suala hilo ili
litolewe maamuzi ya pamoja na wabunge na kuweka mikakati ya kunusuru
kampuni hiyo yenye kukabiliwa na madeni, ukosefu wa mtaji pamoja na
kufanya maamuzi ya kuondoka kwa mwekezaji.
Alisema
wamemtaka Msajili wa Hazina kufanya tathmini ya majadiliano na kupeleka
taarifa katika kamati hiyo siku ya Ijumaa ili kutafuta njia ya kunusuru
kampuni hiyo na kuhakikisha inafanya kazi kwa faida na kushindana na
kampuni nyingine.
Zitto
alisema baadhi ya maamuzi yaliyofanywa kwenye kampuni hiyo, ikiwemo
leseni na masafa yake kutumiwa bure na kampuni ya Celtel ambayo sasa ni
Airtel na kufanya TTCL sasa wanatafuta upya.
“Kampuni
kwa sasa imefilisika kutokana na kuwa na mizania ya bilioni 157 ya
ziada lazima maamuzi yafanyike na tathmini kupelekwa bungeni ili
yafanyike maamuzi sahihi,” alisema Zitto.
Februari
21, 2001, TTCL ilisaini mkataba na Kampuni ya SMI/Detecon, ambayo
ilinunua asilimia 35 ya hisa kwa Dola za Marekani 120 milioni (Sh
bilioni 198).
Hata
hivyo, kiasi kilicholipwa ni Dola 65 milioni tu (Sh bilioni 107.3) kwa
ahadi kwamba kiasi kilichosalia, kingelipwa baada ya hesabu za TTCL
kukaguliwa.
Baadaye
MSI/Detecon ambao ulikuwa ushirika wa Kampuni ya Mobile Systems
International ya Uholanzi na Detecon ya Ujerumani, ilitumia leseni ya
biashara ya simu za mkononi iliyokuwa mali ya TTCL, kuanzisha Celtel
Tanzania.
Baada
ya kuundwa kwa Celtel Tanzania, TCCL walipewa umiliki wa asilimia 40 ya
hisa, baada ya muda mfupi, hisa hizo zilihamishiwa Hazina, hivyo
kuiacha TTCL bila hisa wala biashara ya simu za mkononi.
Katika
mchakato huo, Celtel Tanzania iliuzwa kwa Celtel International ambayo
baadaye iliuzwa kwa Zain. Juni 2010, Zain iliuzwa kwa Kampuni ya Bharti
Airtel Limited ambayo ndiye mmiliki Airtel Tanzania
tiko
tiko
Post a Comment