tiko
tiko
Mambo
magumu yameibuka katika suala la kujadili uanzishwaji wa Mahakama ya
Kadhi, baada ya kutokea malumbano makali na vurugu huku idadi kubwa ya
wabunge wakiitaka serikali kuuondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi
usiwasilishwe bungeni.
Wabunge wengi walisema kufanya hivyo kunaweza kusababisha mpasuko na kuvunjika kwa amani nchini.
Aidha,
wamesema suala la Mahakama ya Kadhi linataka kufanywa kama mtaji wa
kisiasa kwa baadhi ya viongozi wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi
mkuu mwaka huu ili kutafuta kura za Waislamu.
Mvutano
huo uliibuka jana wakati wa semina ya wabunge kujadili Muswada wa
Sheria mbalimbali wa mwaka 2014 ambao ndani yake kuna Muswada wa
Mahakama ya Kadhi ambao umepangwa kuwasilishwa Aprili Mosi mwaka huu
siku ya kuahirisha mkutano wa 19 wa Bunge.
Mbunge wa Ngara (CCM), Deogratias Ntukamazina,
alisema Kamati ya Katiba Sheria na Utawala ilipowaita viongozi
mbalimbali wa dini kuzungumzia suala hilo Waislamu walitofautiana katika
suala la uteuzi wa Kadhi kufanywa na Mufti Mkuu wa Tanzania na wakataka
waelewane kwanza kabla ya suala hilo kupelekwa bungeni.
Alisema
katika mkutano huo makundi 11 ambayo hayakubaliana na Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (Bakwata), walisema Muswada wa Mahakama ya Kadhi
uletwe bungeni baada ya kuridhiana kwa sababu hawakubaliani na Bakwata
ambalo kiongozi wake ni Mufti Mkuu wa Tanzania.
Walisema
maaskofu walisema hawana tatizo na suala la Mahakama ya Kadhi, lakini
isiwe na muundo kama wa mahakama nyingine na kwamba mawazo ya waasisi wa
Taifa, hawakutaka serikali iwe na dini na ndiyo maana hawakuruhusu
mahakama hiyo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Rukia Kassimu,
alihoji ni kwanini Mahakama ya Kadhi inataka kuundwa na kupewa jukumu
Mufti ambaye anatoka Bakwata ambayo ni taasisi binafsi na imesajiliwa na
Mamlaka ya Rita.
“Bakwata ni taasisi kama zilivyo taasisi nyingine, haikubaliki, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi suala la Mahakama ya Kadhi ili Waislamu wampigie kura kwa sababu anataka kugombea urais mwaka huu,”alisema.
Rukia
alisema ni marufuku serikali kuwalazimisha Waislamu kuwa chini ya
Bakwata na kwamba Waziri Mkuu, Pinda anafahamu kwa kina suluhisho na
mvutano huo wa Mahakama ya Kadhi.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR), Moses Machali,
alisema suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na kuingizwa katika
mfumo wa mahakama za kawaida inajichanganya na ibara ya 19 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema
mwaka 2011 Rais Jakaya Kikwete wakati anazindua msikiti wa Gadaf
alisema suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi lisihusishwe na
serikali kwa sababu wapo watu wengine ambao kila mmoja ana imani yake.
Alisema
hatua ya serikali kutaka kuuleta muswada huo wakati bado Waislamu
wenyewe hawaelewani ni kuwakosea Waislamu na kwamba inawezekana Waziri
alilizungumzia suala hili sababu ya malengo yake ya urais.
Machali
alisema kama muswada huu utapelekwa Bungeni itatoa fursa kwa madhehebu
mbalimbali kila moja kuanzisha mahakama yake hali itakayoleta machafuko
nchini kwa kuwa nchi itakuwa katika mfumo wa mahakama za dini.
Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu,
alisema muswada unapendekeza kutambua kitu ambacho mfumo wa sheria za
nchi hauna na kwamba uongo unaotumiwa na serikali ndiyo unafanya watu
wawe na hofu.
Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Ally Kessy, alisema: “Katika
nguzo tano za Kiislamu Mahakama ya Kadhi haipo, nguzo sita za imani pia
haipo, sasa inakuwaje wanadai kitu ambacho hakitambuliki katika nguzo
za kiislamu.”
Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa, alisema
muswada wa Mahakama ya Kadhi urudishwe ukaboreshwe badala ya
kuharakisha kuupeleka bungeni wakati bado una utata hata kwa waislamu
wenyewe.
Mbunge wa Tarime (CCM), Nyambali Nyangwine, alisema
Muswada wa Mahakama ya Kadhi usimamishwe ukafanyiwe utafiti kwanza
kwa sababu ndani ya Waislamu wenyewe hawaelewani.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema Wabunge wasipokuwa makini na suala la Mahakama ya Kadhi, Bunge litaingia katika historia kuvunjika kwa amani.
Selasini
alisema serikali iachane na kutoa ‘jini’ lililofungiwa na waasisi
Mwalimu Nyerere na Karume na kwamba tukifanya mchezo nchi itabaki katika
vipande vipande.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Dk. Mary Mwanjelwa, alisema jambo hili litaligawa Taifa na kwamba waasisi hawakuwa wajinga walipokataa serikali isiwe na dini.
Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa,
alisema nchi inaelekea kubaya kwani msingi wa kuleta Mahakama ya Kadhi
ni kutaka kuwachota Waislamu kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
“Serikali
kama imedhamiria kuleta Mahakama ya Kadhi ilete katika utaratibu mzuri,
lakini kwa huu utaratibu ni unafiki na mwenyezi Mungu hapendi unafiki,
tusiwahadae Waislamu,” alisema.
Khalifa alisema kwa hali ilivyo muswada huo haujaiva na kwamba usiletwe bungeni hadi hapo serikali itakapojipanga vizuri.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde, alisema
suala la imani siyo la chama cha kisiasa kwani suala la Mahakama ya
Kadhi litaipeleka nchi kubaya na inawezekana ikawa ndio mwisho wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
“Mnataka
kutuvurugia nchi sababu ya kutafuta kura za Waislamu, kwa hili Waziri
Mkuu umechemka sana, nalisema hili kwa sababu wewe Waziri Mkuu ndiye
uliyeahidi kuleta bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi,”alisema.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo, alisema yasifanyike masikhala mswaada huyo uwasilishwe bungeni.
Mbunge wa Mbeya Vijijini (CCM), Mchungaji Lackison Mwanjale,
alisema serikali ikajipange upya katika suala la Mahakama ya Kadhi
kabla ya kuuleta bungeni muswada kwani bado suala hilo halieleweki kwa
jamii.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Martaza Mangungu, alisema
hakubaliani na suala la Mufti kupewa jukumu la kuchagua Kadhi Mkuu
wakati Waislamu wengi hawakubaliani na Bakwata ambayo inaongozwa na
Mufti.
Mbunge wa Lupa (CCM), Victor Mwambalaswa, alisema
muswada wa Mahakama ya Kadhi wapelekewe wahusika kabla ya kuletwa
bungeni ili wajadiliane na kukubaliana mambo ya msingi wanayoona
yatawafaa katika uanzishwaji wa mahakama hayo.
Mbunge wa Igunga (CCM), Dk. Peter Kafumu, alisema
serikali imeshindwa kusimamia vizuri suala la uanzishwaji wa Mahakama
ya Kadhi kwa kushindwa kuwaelimisha wananchi jambo hilo.
Mbunge wa Chwaka (CCM), Yahaya Kassim Issa, alisema Waislamu wanataka Mahakama hiyo kwa kuwa wanakosa haki hivyo serikali iruhusu kuanzishwa kwake.
Pinda: Tutatafakari Upya
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, akihitimisha mjadala huo alisema kulingana na
maoni yaliyotolewa na Wabunge ameelewa kwamba bado hakuna maelewano
miongoni mwa Waislamu wenyewe na pia hakuna uelewa wa jamii kuhusu suala
hilo.
Alisema
mambo yaliyowasilishwa kuhusiana na muswada huo ni maamuzi ya Bunge
Maalum la Katiba na siyo yake, bali anabebeshwa msalaba tu kwa sababu
alikuwa anaiwakilisha serikali.
Pinda
alisema kutokana na hali hiyo, serikali itakaa kushauriana tena na
Spika pamoja na Rais waone wafanye nini katika jambo hilo.
Vijembe na Matusi
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Ismail Aden Rage,
wakati akichangia hoja hiyo alishindwa kuvumulia baada ya baadhi ya
wabunge kuingilia mchango wake kwa kumzomea na kusema maneno
yaliyomuudhi na kuamua kuwatolewa maneno ya kuudhi (matusi).
Mbunge wa Fuoni (CCM), Said Mussa Zubeir, aliwaita baadhi ya wabunge walikuwa wakimzomea wakati akizungumza kuwa ni ‘wapumbavu’.
Wakati wa majadiliano hayo ilipofika saa 8:17 wakati Mbunge wa Kisarawe, Jafo akiendelea kuchangia kulitokea vurugu ambazo nusura wabunge wapigane huku baadhi yao wakiamua kutoka ukumbini.
Kutokana
na kutokuwapo hali ya utulivu ukumbini, baadhi ya askari pamoja na
maofisa usalama waliokuwapo nje, walilazimika kuingia ndani kuhakikisha
amani haivunjiki.
Spika wa Bunge, Anna Makinda, alituliza vurugu ukumbini kwa kuwataka wabunge wawe wavumilivu wakati wenzao wakichangia.
Katika
majadiliano wabunge zaidi 30 walichangia na zaidi ya 20 walikataa
muswada wa Mahakama ya Kadhi usiwasilishwe Bungeni siku ya Jumatano
wiki hii.
Kabla ya kuanza majadiliano, Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia,
alitoa hoja kwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Katiba, Sheria na
Utawala, William Ngeleja, kwamba wakati wa majadiliano waandishi wa
habari wasiwepo ukumbini kwa kile alichoeleza ni unyeti wa jambo hilo.
Hata hivyo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Kessy,
alisema kama waandishi wataondolewa ukumbini naye atalazimika kuondoka
huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akisema hakuna sababu
ya kuwaondoa waandishi kwa sababu jambo linalojadiliwa wananchi wanataka
kulifahamu kupitia vyombo vya habari.
tiko
tiko
Post a Comment