tiko
tiko
MTOTO Jacqueline
Lepenza, aliyenusurika katika ajali mbaya ya basi lililogongana na lori
huko Mafinga mkoani Iringa wiki mbili zilizopita, ameripotiwa kuwa na
maajabu baada ya baba yake mzazi kujitokeza na kusimulia, Uwazi
linakutaarifu.
Willy Lupenza, baba mzazi wa mtoto huyo
mwenye umri wa miaka mitatu na nusu, alisema marehemu mke wake, Anjela
Osward (35) (pichani) alikuwa amekwenda nyumbani kwao Ilembula mkoani
Njombe kwa ajili ya ubatizo wa binti yao huyo.
Alisema katika hali ya kushangaza, siku
ya ubatizo huo, Jacqueline alibatizwa peke yake pasipo watoto wenzake
kupewa baraka hizo kwa sababu ambazo hazikueleweka.“Ndugu mwandishi,
hili ni tukio ambalo sitalisahau katika maisha yangu, kwa sababu
haiwezekani mtoto abatizwe peke yake halafu kwenye ajali, idadi kubwa ya
watu wapoteze maisha lakini yeye anusurike.”
Alisema baada ya ajali, mtoto wake huyo
alikutwa na watu waliojitokeza kuwasaidia majeruhi akiwa amelala juu ya
bati la kuzuia matope kwenye tairi ya lori lililokuwa limebeba kontena
huku akilia na matairi yakiendelea kuzunguka.
Alisema haelewi mtoto huyo alitokaje
ndani ya basi hadi kwenye bati hilo la lori, kwani licha ya kukutwa
mzima, lakini eneo hilo pia lilikuwa hatarishi kwa mwanaye ambaye
alimpoteza mama yake aliyekuwa mmoja kati ya watu zaidi ya 50
waliofariki dunia.
Willy alisema Machi 11, mwaka huu
alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa shemeji yake ambaye yuko
mkoani Iringa kwa shughuli zake za kibiashara juu ya tukio hilo, baada
ya yeye naye kuarifiwa na Jeshi la Polisi Iringa baada ya kuokotwa kwa
simu ya mkewe.
Alisema baada ya kupigiwa na polisi
waliofika katika eneo la tukio mapema, shemeji yake huyo alimpigia na
kumjulisha juu ya mkewe kupata matatizo Mafinga.“Nilianza safari mara
moja kuelekea huko, lakini nilipofika Morogoro nilipata taarifa za
uhakika zilizoniaminisha kuwa mke wangu alikuwa amefariki dunia,”
alisema.
Aliongeza kuwa aliendelea kufanya
mawasiliano na ndugu kujua alipo mtoto, hadi alipoambiwa kuwa kulikuwa
na mtoto mmoja aliyekuwa wodini (Hospitali ya Wilaya Mafinga), hivyo
akaambiwa kama anaweza kuwatumia picha yake kwa njia ya mtandao ili
waweze kumfananisha.
“Niliwatumia picha kwa Mtandao wa
WhatsApp, kumbe siku ya ajali mwanangu alikuwa amevaa gauni ambalo
aliwahi kulivaa siku za nyuma, na ndiyo picha niliyowatumia, walimtambua
kirahisi na alipofanyiwa uchunguzi wa kidaktari ikagundulika kuwa
hakuwa na matatizo yoyote kiafya,” alisema baba huyo.
Kufuatia kufika Mafinga na kuutambua
mwili wa mke wake, aliomba mwili huo kutopelekwa sehemu yoyote ili
urudishwe nyumbani kwao Ilembula kwa mazishi yaliyofanyika katika Kijiji
cha Mwambaga.Kuhusu hali ya mtoto kwa sasa, Willy alisema anaendelea
vizuri na anamshukuru Mungu pamoja na madaktari na polisi walioshiriki
katika tukio hilo ambalo mwanaye huyo alipona kimaajabu.
Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya
Scania namba T 689 APJ mali ya Cipex Company lililokuwa likiendeshwa na
Maka Sebastian (26) na basi aina ya Scania namba T 438 CED mali ya
Majinja lililokuwa likiendeshwa na Baraka Gabriel (38).
tiko
tiko
Post a Comment