Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

SIMULIZI YA NATASHA - 5

tiko tiko
WIKI iliyopita tuliishia pale tulipofika rasmi nchini Angola. Tulikuwa tukiifikiria tofauti nchi hiyo tukiamini kwamba ni nchi isiyokuwa na amani.
SASA  ENDELEA…
Sasa nakupa mtazamo wangu nilipofika Luanda, ambao ni mji mkuu wa Angola.  Kwanza ni amani tupu wala huwezi jua kama kuna mtu anatumia risasi mahali fulani ili aishi.Rais ni Eduardo dos Santos, ni nchi nzuri iliyotawaliwa na majengo mengi ya ghorofa na nimejitahidi kila nilipopita nione kama kuna nyumba ya udongo, sikuwahi kuiona zaidi ya nyumba za chini chache.
Ujenzi wa nyumba zao wanatumia milango mingi kama kiunganishi cha chumba na chumba, unaweza kukuta sehemu inayotakiwa kuwa na mlango mmoja wao wamejenga mitatu. Marumaru za ukutani ni jambo la kawaida katika kuta za nyumba zao.
Luanda iko pembezoni mwa Bahari ya Atlantiki inayosifika kwa samaki wengi na watamu, huko niliwaona  samaki wanaoitwa kashushu ni samaki watamu zaidi ya sato maana kwangu sato ni samaki pendwa, kuna sardina na karapau, achilia mbali kamba na kambakochi.
Kwa wiki tulikuwa tukinunua kiroba cha samaki na kama hujamaliza wiki inayofuata unaletewa kiroba kingine mpaka nikawa napika sambusa za samaki kila mwishoni mwa wiki, pia kuna samaki maalum kwa ajili ya kuchoma tu upo hapo?
Kwenye hiyo pwani kuna sehemu ambayo ardhi imeingia baharini wenyewe wanaita ilha (tamka ilya) panapendeza sana na hiyo sehemu haina kazi nyingine zaidi ya watu kwenda kushuhudia jua linavyozama tu (sun set).
Kwa upande mwingine wa bahari kuna hoteli nzuri iitwayo Panorama, ukiiangalia kwa woga unaweza kudhani iko ndani ya bahari na pia upande mwingine kuna matanki makubwa ya mafuta.Usafiri wa mabasi na teksi zipo kama kawaida ingawa sikuwahi kutumia hata mara moja hivyo siwezi kuelezea adha wanazozipata kama za madaladala hapa kwetu.
Cha ajabu hakukuwa na maduka yanayouza nguo wala vifaa muhimu vya matumizi ya kawaida, bado ile hali kama ya Bongo tulipoondoka ya kufunga mikanda ilikuwa inafanana kwa vile wao walikuwa vitani, kwa sisi wageni wafanyakazi wanaofanya katika balozi mbalimbali au mashirika ya kimataifa tulipangiwa na duka la wageni liliitwa Angodiplo (Angola Diplomats).
Huko ndiyo tulinunua mahitaji ya vyakula na vifaa vya nyumbani vidogovidogo. Kwa upande wa nguo, viatu na mafuta ya kupaka inabidi uagize Uingereza au Marekani kwa kupitia kwenye catalogue (vitabu maalum vinavyouza vitu kwa kuagizia) unachagua, unaagiza, unatuma hela kisha wanakuletea.
Gharama unazotakiwa ulipe ikiwemo na usafiri unatuma pesa kupitia benki, baada ya wiki tatu wanakuletea, unaenda kuchukua airport ambako kuna urasimu mkubwa ukizubaa mzigo wako unaweza kukaa hata miezi lakini nilijilazimisha wanijue hivyo ikawa nikipata tu invoice ya mzigo, asubuhi nasema zege halilali nitaneng’eneka mtoto wa Kizaramo hadi jioni narudi na mzigo.
Chezea Natasha wewe! Domo mali yangu silipii vat!
Kitu kingine kilichonishangaza ni kuona wanawake wengi wanavaa nguo nyeusi kila ukitembea mtaani, nikauliza kulikoni?

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII

tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top