tiko
tiko
Mke wa Ruwaichi Wilson, Josephine Singano (anayelia kwa uchungu) aliyetelekezwa na mumewe huyo baada ya kukatwa mguu.
Tukio hilo linadaiwa kuanza mwaka 2013
ambapo Josephine alidai kuwa mumewe alianza kudai kuwa mwanaye wa kwanza
aliyemtaja kwa jina la Goodluck kuwa siyo wa kwake na kusema kuwa
ameonyeshwa hayo na Roho Mtakatifu.
Josephine alidai kuwa alivumilia maneno
hayo ya mumewe kwa muda mrefu ambapo baadaye alianza kuumwa ugonjwa wa
kisukari na kutoka kidonda mguuni mwake ambapo hakikupona na kuwa
kikubwa kiasi cha kukatwa mguu Februari 14 mwaka 2014.
Katika kipindi chote hicho, Josephine
alidai kuwa mumewe ambaye ni daktari wa zahati ijulikanayo kwa jina la
Mafalaso, hakuwa akimsaidia kwa kitu chochote jambo lililomfanya kuhama
nyumba na kwenda kuishi kwa mama yake mdogo aliyemtaja kwa jina la
Neema Juma.
Akizungumza mbele ya Baraza la
Usuluhishi, Kata ya Mburahati, Dar Januari 28 mwaka huu, Josephine
alidai kuwa amezaa na mumewe watoto watatu lakini anamshangaa kumkataa
mtoto wake wa kwanza na kuwakubali wengine wawili huku akidai
kutelekezwa baada ya kuwa mlemavu.
“Nimeishi ndani ya ndoa na huyu mwanaume
miaka kumi na tisa sasa, nilimshangaa mwenzangu baada ya kuanza
kumkataa mwanaye wa kwanza na kutonihudumia mimi kipindi chote
nilichokuwa nikiugua. Mbaya zaidi hadi nakatwa mguu hakuwahi kuja
hospitali wala kunijulia hali. Kwa kuwa sasa ni mlemavu ndiyo hanitaki
kabisa,” alilalama mama huyo huku akimwaga machozi.
Akijibu tuhuma hizo, Dk. Manyanga
alisema kuwa Roho Mtakatifu amemuonesha kuwa mtoto anayedaiwa kuwa ni
mtoto wake wa kwanza, siyo wake. Alipoulizwa kuhusu kumtelekeza mkewe,
alisema kuwa anapenda sana kumsaidia, lakini nafsi yake haimpi msukumo
hivyo anachofanya ni kusikiliza Roho Mtakatifi anasema nini kwa kuwa
yupo tayari kumsikiliza Mungu kuliko mwanadamu na kuongeza kuwa ugonjwa
alionao mkewe ni laana kutoka kwa Mungu kutokana na dhambi alizozifanya.
“Nitamtii Mungu kuliko mwanadamu. Nyinyi
hamjui tu huyu mke wangu nilishamkuta mara kibao na mambo ya
kishirikina halafu aliwahi kuwa kiongozi wa Efatha kanisani. Alipomwacha
Mungu na kwenda hospitali akaishia kukatwa mguu badala ya kudumu kwenye
maombezi ambayo Mungu angemponesha, hilo ndiyo jambo linalonifanya niwe
mzito hata kumtunza.
“Halafu huyo anayemtaja kuwa ni mwanangu
wa kwanza alizaliwa kabla hatujaoana na kila mmoja alikuwa akikaa
kwake, hivyo uhakika kama huyo mtoto ni wa kwangu haupo kabisa,” alisema
Dk. Manyanga.
Baada ya kuwasikiliza wanandoa hao,
wajumbe wa baraza hilo walimtaka Dk. Manyanga na Josephine wafike
Februari 3 mwaka huu (leo) katika baraza hilo kwa ajili ya hukumu huku
Dk. Manyanga akitakiwa kufika na mtoto wake wa mwisho ambaye ana miaka 3
aliyezaa na Josephine ambaye alidaiwa kumpeleka Moshi bila idhini ya
mama yake.
Akizungumza na waandishi wetu, mama
mdogo wa Josephine aliyejitambulisha kwa jina la Neema Juma alisema kuwa
anamshangaa Dk. Manyanga kwa kuhusisha ukatili wake na Roho Mtakatifu
na kuhoji kwa nini asingesema hayo muda wote walioishi katika ndoa yao
mpaka aibue suala hilo hivi karibuni wakati mwenzake ni mgonjwa na
mlemavu anayeshinda akilia na anahitaji msaada wa mume wake?
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Baraza la
Usuluhishi, Kata ya Mburahati, Khadija Magambo alisema kuwa kama suala
hilo halitamalizwa na baraza hilo, basi watalifikisha mahakamani ambapo
pande zote mbili zitaamuliwa kisheria.
tiko
tiko
Post a Comment