tiko
tiko
EMMANUEL Mbasha
ana jina kubwa katika muziki wa Injili hapa nchini. Lakini hata hivyo,
ukubwa wa jina lake hautokani na uwezo wake wa kuifanya kazi hiyo, bali
kitendo chake cha kufunga ndoa na mmoja kati ya waimbaji bora zaidi wa
kike, Flora Mbasha.
Simfahamu sana kikazi Emmanuel, lakini nimewahi kusikiliza nyimbo zake
kadhaa na kugundua kuwa anacho kipaji kinachohitaji kuendelezwa.
Anafanya kazi nzuri ya utumishi wa Mungu kwa kuwaelekeza watu njia ya
kupita ili kuepuka matendo mabaya, kama waimba Injili kote duniani
wanavyowafundisha mafuasi wao.
Katika miezi ya karibuni, uhusiano wake na mkewe uliingia dosari kiasi
cha kujikuta mambo yao ya chumbani yakiibuka hadi sebuleni kabla ya
kuingia mtaani na kuwa habari kubwa ya mjini. Ndoa yao ipo katika
msukusuko mkubwa unaohatarisha ustawi wake.
Katika nafasi yangu ya uandishi, nimesikia kauli zao mara kadhaa, kila
mmoja akiitoa kwa namna ya kumshangaa na hata kumshambulia mwenzake. Kwa
watu walio katika maisha ya ndoa kama mimi, habari zao zinahuzunisha
sana kwa sababu zinajaribu kukuweka katika nafasi ambayo haungependa
ikukute siku moja.
Kuzungumza mambo ya ndani ya mke au mume wako siyo jambo linalopendeza
hata kidogo, kwa sababu ni watu wanaofahamiana kwa mambo yao mengi ndani
ya nyumba yao. Niliwahi kuzungumza suala hili wakati ule Gardner
alipotofautiana na mkewe Jide na kila mmoja kuanza kumzungumzia mwenzake
kwa maneno mabaya katika vyombo vya habari.
Jambo hili limejitokeza tena kwa wanandoa hawa, ambao mzozo kati yao
umewaweka mbali kimaisha, kila mmoja akiishi kivyake. Nimejikuta
nikiumizwa zaidi na Emmanuel katika mzozo huu, kwa sababu yeye ni kijana
wa kiume, ambaye mara nyingi, tunaamini ni wavumilivu na wenye subira
zaidi kuliko akina dada.
Amezungumza maneno mengi kuhusu mkewe, hadi kumtupia baadhi ya tuhuma
ambazo kimaadili, alipaswa kubaki nazo kama siri yake moyoni. Moja kati
ya mambo hayo ni tuhuma kuhusu ujauzito uliosababisha kujifungua mtoto
hivi karibuni.
Wakati ninamsifu Flora kwa kuulea ujauzito wa mtu ambaye anachafuana
naye magazetini na mitandaoni, nimeshangazwa kidogo na Emmanuel kwa
kumkana mtoto aliyezaliwa, akitaka jamii ielewe kuwa mkewe amechepuka.
Lakini maneno ya baba mdogo wa Flora aliyejitambulisha kama Kisekwa,
aliwaambia waandishi wa Global Publishers kwamba maneno ya mkwe wake ni
ya kushangaza sana kwani kila ndugu wa pande zote, wanafahamu kwamba
wakati mzozo kati yao ukianza, mwanamke alikuwa ni mjamzito na wote
wawili walifahamu kuhusu jambo hilo.
Kama ukweli ni huu, kwa nini Emmanuel anajaribu kukifanya kitu cha namna
hii, hasa kwa mtu ambaye anafahamika kama Mtumishi wa Mungu? Anataka
dunia ifahamu kwamba Flora alizini nje ya ndoa yake na asivyo na busara,
akamudu hata kuzaa nje katika kipindi kifupi tu cha mzozo wao?
Lakini kwamba ujauzito siyo wake, yaweza kuwa kweli pia kwani hakuna
lisilowezekana chini ya jua. Kinachonitatiza ni ukosefu wa busara za
kawaida tu za kibinadamu katika kupambanua mambo, hasa ya kifamilia kama
haya.
Leo wapo katika mzozo, vipi kesho wakifikia mahali na kumaliza tofauti
zao? Mbasha hatajisikia vibaya tukimwambia analea mtoto asiye wake?Mtoto
wa kiume siku zote anatakiwa kuwa jasiri na mvumilivu, ndiyo maana
wazee wenye busara zao husema mwanaume ana koromeo, linalomzuia kuongea
baadhi ya mambo. Muache mtoto wa kike apige kelele kwa sababu ndiyo sifa
yao ‘kuchonga’, wanaume wanatafuta hela.
Andiko hili liwahusu pia wanandoa wengine wote wanaokimbilia kuzungumza
habari za wenza wao nje kutokana na mzozo wao. Unaweza kudhani
unamkomesha mwenzako, lakini ukweli ni kwamba unajivua nguo mwenyewe!
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment