Realtime blog statistics Realtime blog statistics
Scanning..

MAUAJI YA MTEJA WA GARI. NDUGU WASIMULIA

tiko tiko
Ndugu na majirani pamoja na watu waliohudhuria mazishi wakiwa katika Ibada kabla ya kwenda makaburini , Malamba mawili jijini Dar es Salaam jana kwa ajili ya mazishi.
Mapya yameibuka katika mauaji ya Farahan Maluli (30), anayedaiwa kuuawa na rafiki yake ambaye ni mtoto wa bosi wake baada ya ndugu wa marehemu kuzungumzia jinsi marehemu alivyokuwa akitoa fedha kwa mtuhumiwa wa mauaji hayo.
 
Ndugu wa marehemu walifichua siri hiyo wakati wakizungumza na paparazi  kwenye mazishi ya kijana huyo yaliyofanyika jana eneo la Malamba Mawili Mbezi Mwisho, jijini Dar es Salaam.
 
Kaka wa marehemu, Abdallah Yusuf, alisema Farahani (marehemu), kabla ya mauti hayo kumkuta, alikuwa akitoa fedha kwa awamu kwa ajili ya kununulia gari la kusombea mchanga ‘tiper’ kwa bei ya Sh. milioni 35.
 
Alisema katika makubaliano hayo, Farahani alianza kutoa Sh. milioni 17, mara ya pili milioni 10, mara ya tatu Sh. 500,000 na baadaye akamalizia kwa kutoa Sh. 2,500,000 ambazo alimkabidhi rafiki yake na mtuhumiwa siku moja kabla ya mauti kumkuta. 
 
Alisema mdogo wake alipotea Juni 11, mwaka jana na taarifa zilitolewa katika Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuf.
 
Abdallah alisema baada ya uchunguzi kufanyika, polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambaye ni Hemed Hamis na kumuweka kituoni kwa muda wa wiki mbili kabla ya kutolewa nje kwa dhamana kwa madai alikuwa mgonjwa.
 
“Mdogo wangu alivyopotea nilikuwa natumiwa meseji kupitia simu yake ambazo zilikuwa zinasema `mdogo wako huwezi kumpata hadi pale utakapokuja kunikabidhi fedha zangu Shilingi milioni 75 ,” alisema.
 
Alisema simu hiyo iliendelea kutumiwa kwa mwezi mmoja na baada ya hapo haikupatikana tena, kitendo kilichowafanya ndugu kukutana kujadili suala hilo na baadaye walikata tamaa.
 
“Tulikata tamaa kumtafuta baada ya kumtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio na pia simu tulizokuwa tunapigiwa zilikuwa hazipatikani tena,” alisema na kuongeza:
 
“Pia simu za vitisho zilitupa wasiwasi na kudhani mdogo wetu alishiriki vitendo viovu ambavyo vilitufanya tuamini kuwa mdogo wetu ametoroka kwenda nje.”
 
Naye dada wa marehemu ambaye hakutaka jina lake liandikwe mtandaoni, alisema Jumatatu wiki hii, walipigiwa simu na polisi wa Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuf  na kuwataka waende Kituo cha Polisi Msimbazi.
 
Alisema baadaye kaka yao ambaye ni Abdallah, aliporudi kutoka Kituo cha Polisi Msimbazi, aliwaeleza kuwa Faharani (marehemu), aliuawa na rafiki yake Hemed na alimfukia kwenye nyumba aliyokuwa anaishi.
 
Aliongeza kuwa polisi waliwachukua ndugu zao wa kiume na kwenda nao katika nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa (Hemed) iliyopo eneo la Ilala Sharif Shamba, jijini Dar es Salaam.
 
Alisema walipofika katika nyumba hiyo, walionyeshwa eneo ambako Farahani alikuwa amezikwa na kuanza kuufukua mwili wake na kuuchukua kwenda nao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi.
 
Hata hivyo, zoezi la kufukua mwili huo lilikuwa na changamoto kutokana na mtuhumiwa kuonyesha eneo la uani ambalo halikuwa lenyewe.
 
Jirani mmoja ambaye alikuwapo eneo la tukio, aliwaonyesha polisi eneo ambalo alikuwa na shaka nalo na ndipo polisi walipoanza kufukua mwili huo.
 
Taarifa zinaeleza kuwa kazi ya kufukua mwili wa marehemu huo ulianza saa 4:00 asuhubi na kumalizika saa 8:00 kutokana na shimo alilokuwa amezikwa kuwa na urefu wa mita 10.
 
Naye Mustapha Mwalongo, aliyekuwa akifanya kazi na marehemu, alisema alimfahamu Farahani kuwa mfanyakazi wa mabasi ya kampuni ya Noraz na Waheed.
 
Alisema alimuamini Hemed kwani alikuwa ni mtoto wa bosi wake na aliyekuwa karibu naye.
 
Mwalongo ambaye pia ni Mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), alisema kufuatia marehemu kumdai sana mtuhumiwa, ilifikia hatua akamweleza baba yake na mtuhumiwa, hali iliyosababisha urafiki wao kuvunjika.
 
Kwa upande wake, rafiki wa karibu wa marehemu, Somji Nawanda, alisema Hemed (mtuhumiwa), alimpigia simu marehemu Juni 9, mwaka jana na kumtaka aende Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kulipia ushuru wa gari alilomwagiza.
 
Alisema alipofika TRA, walimtafuta Hemed ambaye alidai kuwa muda huo alikuwa Kariakoo na baadaye alimpigia simu na kumwambia aonane na mtu mmoja aitwaye Said amkabidhi Sh. milioni 2.5.
 
“Marehemu alisita, lakini Hemed alimwambia ni pesa ngapi umenipa unashindwa kuniamini kwa fedha hizo? Ndipo marehemu alipomkabidhi fedha hizo Said na kumwambia asubiri aingie TRA amchukulie stakabadhi, aliporudi Said alisema mtandao unasumbua hivyo hawezi kupata stakabadhi waonane naye tena Juni 11, mwaka jana kwa ajili ya kuchukua gari,” alisema Nawanda.
 
Mmoja wa majirani aliyejitambulisha kuwa ni Mama Salum, alisema hawakuwa na taarifa kama jirani yao alifariki dunia kutokana na kazi zake za uwakala ila walidhani amesafiri.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alipotafutwa juzi kwa njia ya simu, alisema alikuwa barabarani akiendesha gari na kuahidi kuwa akishuka atapiga simu.
 
Hata hivyo, baada ya kuendelea kupigiwa simu, alituma ujumbe mfupi (sms) akisema kuwa angepiga muda mfupi, ingawa hakupiga. 
Hata alipopigiwa na kutumiwa sms, hakupokea hadi tunakwenda mitamboni.
 
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alipopigiwa awali, alielekeza apigiwe Nzuki, akisema kuwa ndiye mwenye taarifa hizo.
 
Jumatatu wiki hii, polisi, ndugu na wakazi wa Ilala Sharif Shamba, jijini Dar es Salaam, walifichua kuuawa kwa Farahani aliyeuawa na rafiki yake kisha kumfukia kwenye shimo alilochimba na kulifukia pamoja na kulisakafia uani kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa.
 
Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa Julai, mwaka jana, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kushindwa kumlipa rafiki yake huyo Sh. milioni 35.

TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII

tiko tiko

Post a Comment

CodeNirvana
© Haki Zote Zimeifadhiwa Kalamu 1 | designed by tabasamu na ∂αиιєℓι
Code Nirvana
Back To Top