tiko
tiko
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki
Mkazi wa Ilala
Sharifu Shamba, jijini Dar es Salaam, anatuhumiwa kumuua rafiki yake
kisha kumfukia kwenye shimo alilochimba na kulisakafia uani kwenye
nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa.
Mauaji hayo yanadaiwa kufanywa Julai, mwaka jana, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kushindwa kumlipa rafiki yake huyo Sh. milioni 35.
Inadaiwa kuwa
marehemu alimpa mtuhumiwa huyo fedha hizo ili akamnunulie gari na
kwamba, baada ya kudaiwa muda mrefu, ndipo alipoamua kufanya ukatili
huo.
Habari
zilizotufikia zinaeleza kuwa kabla ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa
alimpigia simu rafiki yake huyo na kumtaka aende bandarini kuchukua gari
hilo kwa madai kwamba, lilikuwa limewasili.
Kwa mujibu wa
habari hizo, wakati huo mtuhumiwa alikuwa bandarini akimsubiri rafiki
yake huyo. Inadaiwa rafiki yake huyo alikwenda hadi bandarini na
kuonana na mtuhumiwa huyo.
Hata hivyo, kilichotokea ni mtuhumiwa kumzungusha rafiki yake huyo bila kupata gari alilomuahidi.
Hali hiyo
ilimfanya rafiki yake huyo kulazimika kuondoka baada ya kushindwa
kuhimili mzunguko waliokuwa wakifanyiwa na mtuhumiwa. Baada ya kushindwa
kupata gari alilolitarajia, mtuhumiwa aliamua kurudi na rafiki yake
huyo nyumbani kwake (mtuhumiwa), Ilala ambako alitekeleza mauaji hayo na
kumzika.
Akizungumza
jana, mmoja wa mpangaji wa nyumba hiyo, ambaye ni kaka wa Sheikh
Sharifu, Abubakar Matonga, alisema walihamia kwenye nyumba hiyo Novemba
17, mwaka jana na kwamba, wamekuwa wakiitumia kwa shughuli za maombezi.
“Jana (juzi)
walikuja watu wanne waliojitambulisha kuwa ni polisi. Walituhoji na
kutuomba mkataba wa nyumba tulioingia na mwenye nyumba. Baada ya kuwapa
mkataba huo, walituomba namba ya simu ya mwenye nyumba. Walipompigia
simu, walimtaka aje kwenye nyumba yake,” alisema Abubakar.
Aliongeza:
“Alipofika, polisi walisema kuwa nyumba hii ilitumika kwa mauaji
yaliyofanywa na mpangaji aliyekuwa akiishi humu kipindi cha nyuma.
Alihama mwezi wa saba, mwaka jana baada ya kufanya mauaji.”
Abubakar alisema
polisi walisema mpangaji aliyekuwa akiishi katika nyumba hiyo alikuwa
anadaiwa na marehemu zaidi ya Sh. milioni 30 alizopewa kwa ajili ya
kumuagizia gari, lakini akakaa na fedha hizo zaidi ya mwaka bila
kuonyesha hilo gari wala kurejesha fedha hizo.
“Fedha hiyo
ilikaa kwa muda mrefu, takribani mwaka. Kutokana na kero za kumdai, siku
moja mdaiwa akampigia simu mdeni wake na kumwambia gari limekuja
bandarini, aende akamkabidhi pamoja na nyaraka muhimu,” alisema
Abubakar. Alisema polisi waliwaeleza kuwa, alipopigiwa simu, alimwambia
rafiki yake waende wote ili akamsaidie kuendesha gari hilo.
Abubakar alisema
alipofika bandarini, alizungushwa bila mafanikio yoyote. Alisema
rafiki ya marehemu alipoona mizunguko imezidi, alimuaga akamwambia
akishapokea gari amjulishe ili amfuate.
Mmoja wa
majirani, ambaye hakutaka jina liandikwe gazetini, alisema polisi
walifika jana (juzi) eneo la tukio na kuwakusanya wananchi, wakiwamo
wajumbe wa nyumba kumi, viongozi wa serikali za mitaa na kuwapa taarifa
za mtu kuuawa na kufukiwa kwenye nyumba hiyo.
“Baada ya
kutueleza, walianza kuchimba mlangoni ambako mwili huo ulifukiwa na
kuutoa. Lakini mwili huo ulionekana ukiwa umefungwa fungwa na mito ya
godoro ambapo ilionekana miguu, mikono na fuvu,” alisema.
Mjumbe wa nyumba
kumi na Serikali za Mtaa Tawi la Amana, Kitongoji cha Sharifu Shamba,
Christina Msala, aliwashauri wenye nyumba kwamba, wanapopangisha nyumba
watoe taarifa kwa wajumbe wa eneo husika ili likitokea tatizo mtu
afahamike hata kwa jina.
Juzi polisi Mkoa
wa Ilala walifukua mwili huo baada ya kumkamata mtuhumiwa ambaye jina
lake halijafahamika na kumhoji muda mrefu na baadaye waliuchukua mwili
kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi.
Kamanda wa
Polisi Mkoa huo, Mary Nzuki, alipopigiwa simu jana, ilipokelewa na mtu
alijitambulisha kuwa msaidizi wake, ambaye alisema bosi wake yuko kwenye
mazishi ya watu sita walioteketea kwa moto wiki iliyopita katika maeneo
ya Kipunguni.
Hadi tunakwenda mitamboni tuliendelea kumtafuta Kamanda Nzuki, lakini simu yake haikupatikana.
TOA MAONI YAKO HAPO CHINI KUHUSU HABARI HII
tiko
tiko
Post a Comment