tiko
tiko
Waziri
wa Fedha, Saada Mkuya akimsikiliza mbunge wa viti maalumu, Ester Bulaya
aliyetaka waziri huyo afukuzwe kazi kwa sababu amevunja katiba.
Bunge
limeendelea kuwa moto kwa viongozi wakati wabunge wakiwalipua mawaziri,
huku wakimtaka Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kufukuzwa kutokana na
kukiuka Katiba na kumrushia bomu Lazaro Nyalandu kuwa anazunguka nje ya
nchi na msichana kwa madai ya kutangaza utalii.
Mbunge
wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, pia alikumbana na kadhia hiyo
wakati alipodaiwa kuwa anahusika kwenye kila mikataba mibomu, jambo
lililosababisha mwanasheria huyo mkuu wa zamani kuingilia kati akitaka
“kuheshimiana”.
Wabunge
walifanya hivyo jana bungeni mjini Dodoma wakati wakichangia taarifa za
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (LAAC) ya mwaka ulioishia Juni 30 mwaka 2014.
Mkuya
alijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Serikali kuonyesha kuwa Serikali ilitumia fedha zilizotengwa
kwa ajili ya matumizi mengine, kitendo kinachomaanisha kuwa alivunja
Katiba.
Akichangia
mjadala huo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Ester Bulaya alisema Bunge
limekuwa likitunga sheria na wao kama viongozi lazima waonyeshe mfano wa
kufuata sheria.
“Fedha
ambazo ziko kwenye ring fence (mfuko maalumu), hazitakiwi kutumika kwa
matumizi mengine kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa Katiba, Waziri
umevunja Katiba kwa mujibu wa ibara ya 135 na ibara ya 136 ni Tanzania
peke yake (Waziri Mkuya) unabaki salama. Hupaswi hata kupewa heshima ya
kujiuzulu, unafukuzwa kazi,” alisema Bulaya.
Bulaya,
ambaye amekuwa mmoja wa wabunge wachache kutoka chama tawala wanaoihoji
Serikali, alisema wizara hiyo imeshindwa kukata fedha kwa ajili ya
chai, suti na sambusa na badala yake inakata fedha zilizokuwa ziende
kupeleka umeme vijijini.
Alisema fedha hizo zimetengwa ili kuwezesha Watanzania ambao ni masikini kutumia vibatari.
Bulaya
alikuwa akizungumzia Sh180.7 bilioni zilizokusanywa kulipia gharama za
mradi kutokana na mauzo ya mafuta ili ziweze kupeleka umeme vijijini.
Ripoti
inaonyesha kuwa, kati ya fedha hizo, Sh144.2 bilioni ndizo
zilizopelekwa kwenye mfuko wa umeme vijijini ikiwa ni pungufu ya Sh36.5
bilioni.
Wakati
wa kuhitimisha mjadala wa ripoti hizo, Naibu Waziri wa Fedha (Sera),
Mwigulu Nchemba alikiri kuwa wizara iliyumba katika eneo hilo kutokana
na hali ya kifedha ya Serikali.
“Mwaka
huu ni hapa tu ambako tuliyumba, (katika) eneo hili la matumizi ya
fedha za miradi,” alisema Mwigulu na kuongeza kuwa wizara yake inaandaa
utaratibu utakaowezesha makosa hayo kutojirudia.
Hata
hivyo, alisema mwaka jana wizara ilitoa Sh500 bilioni katika mwezi wa
kwanza tangu kupitishwa kwa bajeti, jambo ambalo alisema lilishangaza
wengi.
“Kuna
baadhi ya watu wamesema miradi mingine ilipata sifuri. Ukweli ni kwamba
ile ambayo ilipata sifuri ni kutokana na fedha hizo kutegemewa kutoka
kwa nchi wafadhili,” alisema. “Lakini miradi mingi ilipata fedha kwa
kuwa tulilipa Sh500 bilioni mwezi wa kwanza baada ya bajeti.”
Alishauri
wabunge kumpongeza Waziri Mkuu kwa maeleo kuwa amefanya mengi, ikiwa ni
pamoja na kuanzisha utaratibu wa kutaka fedha za miradi zisitolewe hadi
wahusika watakapotoa maelezo ya matumizi ya fedha na kwamba
amejiondolea hata mamlaka ya kusamehe kodi ili kuwezesha fedha
zinazopatikana ziende kwenye miradi ya maendeleo.
Awali,
katika mjadala huo, wabunge wengi waliilaumu Wizara ya Fedha kwa
kutumia fedha za miradi kwa ajili ya shughuli nyingine na kukopa fedha
kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii na kutorudiusha.
Walisema
vitendo hivyo vinaifanya taasisi hizo kushindwa kujiendesha wakati
miradi ya maendeleo ikishindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa fedha.
Pamoja
na Waziri Nchemba kutoa maelezo ya jinsi miradi hiyo ilivyokwama,
Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema kuwa siyo kweli kwamba Serikali
imechukua hatua na kwamba ahadi ya Waziri Mkuya kuwa ataunda kikosi kazi
kwa ajili ya kushughulia matatizo hayo, haitoi matumaini kwa kuwa hiyo
itakuwa ya kumi.
“Serikali
haina nidhamu ya kulipa,” alisema Zitto na kutoa mfano wa fedha
zilizochukuliwa kutoka Bima ya Afya kwa ajili ya kununua magari ya
polisi ambazo hazijalipwa hadi leo.
“Magari
ya polisi na Bima ya Afya vina uhusiano gani?” alihoji na kuongeza kuwa
tabia hiyo inadhoofisha mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo inatoa fedha
ambazo ni malipo ya pensheni.
“Hii
inafanyika kwa mifuko yote ya NSSF, PSPF na PPF. Deni sasa ni Sh1.8
trilioni na fedha hizi ni za kuwalipa wastaafu… Kuna mfuko mmoja ambao
technically (kitaalamu) ni bankrupt ( umefilisika).”
Pia,
alisema wakati wa kuidhinisha fedha za mradi wa vitambulisho, Bunge
liliidhinisha Sh52 bilioni. Lakini Bunge lilipomaliza vikao, Serikali
ikaenda kuzikopa.
Utoro wa mawaziri
Mapema jana asubuhi wakati Bulaya akiongea hayo, kulikuwa na mawaziri wasiozidi tisa, kati yao wanne wakiwa manaibu.
Waliokuwapo
bungeni ni Mhagama, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais
(Muungano), Samia Suluhu, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais
(Mazingira), Binilith Mahenge, Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji,
Christopher Chiza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Mawaziri
wengine ni Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk
Asha-Rose Migiro, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Dk Mary Nagu na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia.
Manaibu
alikuwa ni Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, Naibu Waziri wa Kazi na
Ajira, Dk Makongoro Mahanga, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Ummy
Mwalimu na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi.
Hali
akijua hayo, Bulaya alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama kugeuka na kuangalia idadi ya
mawaziri ambao wapo bungeni.
Baadaye
aliendelea kusema kuwa wabunge wamekuwa wakiongea mambo mazuri kama
hayo, lakini mawaziri hawako bungeni na badala wanakuwapo wachache.
Mbunge
wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema inasikitisha kwamba
hata wanamitindo sasa wanaanza kufikiria kuwa marais.
Alisema
hali hiyo inasababishwa na wanavyokaa katika Baraza la Mawaziri,
akieleza kuwa mawazo yao mawaziri hayaonyeshi ubunifu wa kubadilisha
nchi.
Lema alisema ndiyo maana Serikali imeshindwa kuwekeza katika miradi ya maji ambayo ingeweza kuleta fedha nchini.
Alisema
Serikali imeshindwa pia kupata Sh20 bilioni kwa ajili ya kufufua
kiwanda cha kutengeneza matairi cha General Tyre kilichopo mjini Arusha.
“Mara
nyingi hii husababishwa na tabia ya mawaziri ambao mnapokutana kwenye
vikao vyenu, mara nyingi mnakwenda kutafuta group picture (picha za
pamoja) badala ya kushauri namna gani ya kupeleka nchi hii mbele,”
alisema mbunge huyo machachari.
“Ndiyo
maana mnashinda kwenye (mitandao wa kijamii ya) instagram, facebook na
Jamii Forums… mnapiga picha za kung’aa kwa sababu katika vikao vyenu vya
kufanya uamuzi, mnajadili mambo ambayo hayana kina cha mawazo. Ndiyo
maana nchi hii inakufa.”
Alisema viongozi wengi wanakosa ubunifu wa kuiendeza nchi hii.
“Angalia
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikwenda kutangaza
utalii nje ya nchi akiwa ameongozana na (mwigizaji maarufu wa filamu wa
Tanzania) Anti Ezekiel,” alisema na kuongeza kuwa waziri huyo hashindi
ofisini kwa kisingizio cha kutangaza utalii.
Alisema
mbuga za wanyama zipo nchini, lakini waziri huyo amekuwa akishinda
Ulaya na kuongeza kuwa sekta ya utalii ingetengenezewa mikakati,
ingeweza kuendesha nchi.
Chagonja atuhumiwa
Lema
alisema hata juzi wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe
anashambuliwa na wabunge kuhusu kilichodaiwa unyanyasaji wa polisi,
alimfuata, akamweleza kuwa tatizo siyo yeye bali ni nchi imekuwa kama
gheto.
“Leo
Jeshi la Polisi, leo (Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la
Polisi, Paul) Chagonja haamini kama Rais ameshafanya Uteuzi wa IGP.
Jeshi la Polisi limepasuka ma-RPC (makamanda wa polisi wa mikoa)
wanalalamika. Chagonja haamini kama Rais ameshafanya uteuzi,” alisema.
“Kwa
hiyo anafanya sabotage (hujuma). Hata hizi bunduki zinazoibwa inaweza
kuwa ni mkakati wa Chagonja kumhujumu IGP. Chikawe anajua, watu wote
wanajua lakini kila mtu anasema polepole hii nchi kama gheto (neno
linalotumika kumaanisha nyumba ya mabachela) hujui Serikali ipo wapi.”
Mvutano wa Lissu na Mwanasheria Mkuu
Katika
sakata jingine bungeni jana asubuhi, Mbunge wa Singida Mashariki
(Chadema), Tundu Lissu alisema katika sakata la uchotwaji fedha kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow watu walioshtakiwa hadi sasa ni wale wenye
nyadhifa ndogo.
Alisema
kuwa watu wamechukua mabilioni ya fedha, lakini waliochukuliwa hatua
katika sakata hilo ni wale waliopatiwa Sh80 milioni.
Alisema
Bunge lilipendekeza majaji waliotajwa katika sakata hilo wachukuliwe
hatua, lakini hadi leo bado hawajachukuliwa hatua. Alisema Rais Jakaya
Kikwete anasema hatua za kuwachukulia majaji hao zianzie mahakamani.
“Huyu
Rais anashauriwa na nani? Katiba yetu inasema wazi kabisa ibara 113 na
120A2 kuwa Rais atakuwa na mamlaka ya nidhamu kwa majaji, huyu anayesema
mamlaka ya nidhamu hayaanzii kwake ni nani?”alihoji.
Hata
hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alimkatisha kwa
kumpa taarifa kuwa suala hilo lilitolewa mwongozo na Spika kuwa hoja
ikitolewa bungeni haiwezi kurejea tena bungeni hadi baada ya miezi 12.
Hata
hivyo, suala hilo linaweza kurejea tena bungeni kama hoja mahususi.
“Lakini pia Serikali ilete taarifa ya utekelezaji kabla ya Bunge la
bajeti ambalo halijafika,” alisema.
Alisema kanuni haziruhusu kumhusisha Rais na ujengaji wa hoja kwa namna ya kejeli.
Akiendelea
na hoja zake, Lissu aliendelea kusema amepata taarifa ya ‘mrithi’ wa
Jaji Fredrick Werema. Hali iliyomfanya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu,
kuingilia kati na kumtaka Lissu kutotaja mambo ya urithi.
Hata hivyo, Lissu alisema hoja yake ya msingi Taifa linaharibiwa na ukosefu wa uwajibikaji.
Alisema wanaotakiwa kuadhibiwa na Rais hawaadhibu na kwamba hoja yake siyo kumkejeli Rais.
Alisema
imeonekana katika kamati kuwa majaji wamechukua rushwa, lakini Rais
amekuwa akikimbia na kushindwa kutimiza wajibu wake kikatiba.
Hali hiyo, ilimfanya Masaju kuomba tena taarifa na kusema:
“Ibara
ya 112 inaunda Tume ya Utumishi wa Mahakama 113 inaeleza majukumu ya
Tume ya Utumishi wa Mahakama… Moja wapo majukumu ni kumshauri Rais
kuhusu nidhamu ya majaji, hivyo Rais hawezi kuchukua hatua bila kupata
ushauri huo,” alisema.
Alisema
Rais hawezi kuchukua hatua bila tume ya utumishi kulifanyia kazi na
kisha kumpelekea Rais mapendekezo ambayo ndiyo yatafanyiwa uamuzi.
Mgawo wa Zanzibar waingizwa
Habibu Mnyaa (Mkanyageni-CUF), alilamikia tatizo la fedha za mafuta wanazokatwa pande zote kushindwa kwenda upande wa Zanzibar.
“Nahitaji
majibu ya waziri ni kwanini mpaka sasa hata shilingi moja haijapelekwa
huko…Tukilalamika mnasema Wazanzibari ni wakorofi. Hii ndiyo hali
inayotufanya tuone uonevu wa misingi ya serikali tatu na kutoona umuhimu
wa muungano,”alisema.
Kamati ya Uongozi
Kamati ya Uongozi ya Bunge imeamua kuwa kuanzia sasa halitajadili jambo lolote lililo mahakamani kama ilivyokuwa awali.
Msimamo
huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu baada ya
kikao cha Kamati ya Uongozi kilichokaa kujadili jambo hilo.
Zungu
alitoa tamko hilo baada ya jana asubuhi mbunge wa viti maalumu, Suzan
Lyimo kuomba mwongozo wa kwa nini suala la Uda linakatazwa kujadiliwa
wakati lipo kwenye ripoti za kamati.
Juzi,
Spika Anne Makinda pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George
Masaju kuzuia kujadiliwa suala la Uda kutokana na kuwapo kwa kesi mbili
mahakamani.
Jana
baada ya kikao cha Kamati ya Uongozi, Zungu alisema: “Tumekubaliana
kwamba suala lolote ambalo lipo mahakamani halitajadiliwa hapa bungeni
kipindi hiki,” alisema Zungu na kuongeza: “Tusiingilie kabisa jambo hilo
na huo ndiyo mwongozo kuhusu ombi la Suzan Lyimo.”
tiko
tiko
Post a Comment