tiko
tiko
Utangulizi
Ndugu zangu;
Watanzania Wenzangu;
Kama ilivyo ada imefikia siku ya kuuaga
mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na
kuukaribisha mwaka mpya wa 2015. Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa
rehema kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa
ndugu na jamaa zetu ambao hawakujaliwa kuiona siku ya leo tuzidi
kuwaombea mapumziko mema. Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehema atujaalie umri mrefu, afya njema na mafanikio tele kwa kila
tuliombalo katika mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ndugu wananchi;
Hizi ni salamu zangu za mwisho
za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi yetu. Mwakani salamu kama hizi
zitatolewa na Rais wetu mpya. Mimi wakati huo nitakuwa raia wa kawaida
kijijini kwangu Msoga nikifuatilia kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa
Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi yetu akitoa salamu zake za kwanza za
mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha na faraja kubwa kwangu.
Hali ya Usalama
Ndugu Wananchi;
Tunaumaliza
mwaka 2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na hakuna
tishio lolote la kiusalama kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano
wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani ni mzuri. Hakuna nchi iliyo
adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha usalama wa
Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na
watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya nchi
yetu kuwa salama.
Uhalifu Unapungua
Ndugu Wananchi;
Taarifa za Polisi zinaonyesha
kuwa, mwaka 2014 vitendo vya uhalifu vimepungua ikilinganishwa na mwaka
2013. Mwaka huu, matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906 katika
mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la
Polisi wakishirikiana na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia wema.
Naomba ushirikiano huu uendelee mwaka ujao na miaka ijayo ili tuweze
kupata mafanikio makubwa zaidi.
Ajali za Barabarani
Ndugu Wananchi;
Nimefarijika kusikia pia kuwa matukio ya ajali za barabarani nchini nayo yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali 14,048 zilizosababisha vifo vya watu 3,534 na wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383zilizosababisha vifo 3,746 na majeruhi 19,433. Hivyo mwaka huu kulikuwa na ajali 8,335,vifo 212 na majeruhi 3,267 pungufu
kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo ingawa bado
ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata unafuu
huu mwaka huu yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ugaidi
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumefanikiwa
kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao wanaotuhumiwa kupanga na
kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu na kumwagia watu
tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wametiwa nguvuni. Tayari watuhumiwa 87 kati
yao wameshafikishwa mahakamani na waliosalia watafikishwa wakati wo
wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua wahusika wengine ambao
hawajakamatwa.
Ndugu wananchi;
Kwa niaba ya Watanzania
wenzangu wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na
usalama kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutambua mtandao wa ugaidi nchini
na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti. Hali kadhalika nawashukuru
raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha haya kufanyika. Hatupaswi
kubweteka wala kudhani kuwa mambo yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua
tahadhari muda wote kwani hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani,
lini na wapi.
Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupata mafanikio
ya kutia moyo katika vita dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za
kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa 935 wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19 zimefunguliwa Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45 za cocaine na kilo 81,318 za
bangi zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum
cha Kukabiliana na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea
kupatikana. Matunda ya kazi yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe
maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali itaendelea kuwaunga mkono.
Ndugu wananchi;
Kama nilivyoahidi mwaka jana, Muswada wa
Sheria ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa
mara ya kwanza katika Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu.
Pamoja na kupendekeza kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa
za kulevya, Muswada huo pia unapendekeza kuanzisha chombo kipya chenye
nguvu cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Muswada huu
ukipitishwa na kuwa Sheria tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi
ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Ujangili wa Wanyamapori
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya
bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa. Kwa ujumla kasi ya
ujangili imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu 114 waliuawa ikilinganishwa na ndovu219 waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473 mwaka 2012. Aidha, majangili 1,354wamekamatwa na pembe za ndovu 542 na silaha mbalimbali 184 nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaani Tanzania Wildlife Agency (TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na mapambano dhidi ya ujangili.
Natoa pongezi nyingi kwa
askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Serikali na
raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na mafanikio
yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana na ujangili na biashara
haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori zitaendelezwa kwa nguvu
zaidi mwaka ujao 2015 na miaka inayofuatia. Napenda kutumia fursa hii
kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu wa maendeleo wanaotuunga mkono kwa
hali na mali katika mapambano haya. Naomba waendelee kutusaidia.
Hali ya Uchumi Jumla
Ndugu wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri kwa
uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta nyingi ulikuwa ni mzuri. Ndiyo
maana tunategemea kuwa tutafikia au hata kuvuka lengo tulilojiwekea la
pato la taifa kukua kwa asilimia 7.4 mwaka huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwaasilimia 7.3. Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014 ukilinganisha na Januari 2014 ulipokuwa asilimia 6.0.
Hali nzuri ya upatikanaji wa chakula nchini imesaidia sana kufanya
mfumuko wa bei kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko wa
bei utaendelea kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.
Mauzo Nje
Ndugu Wananchi;
Mauzo nje yameendelea kuongezeka. Katika
kipindi kilichoishia Oktoba 31, 2014, Tanzania iliuza nje bidhaa na
huduma zenye thamani ya dola za Marekani milioni 8,503.9ukilinganisha na mauzo ya dola milioni 8,332.5 katika
kipindi kama hicho mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa zaidi
kama bei za kahawa, chai, korosho na pamba zisingeanguka au bei ya
dhahabu nayo isingepada.
Akiba ya Fedha za Kigeni
Ndugu Wananchi;
Akiba yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za Marekani milioni 4,251.8 kwa kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014. Kiasi hicho kinatuwezesha kuagiza bidhaa toka nje kwa miezi 4.1. Hii ni chini ya lengo letu la kuwa na akiba ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi minne na nusu. Hata hivyo, sina wasiwasi kabisa kwamba tofauti hii ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.
Mapato ya Serikali
Ndugu Wananchi;
Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati ya Julai hadi Novemba, 2014 yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama hicho mwaka 2013 hadi shilingibilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo yalikuwa asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu mbalimbali zilizosababisha
lengo lisifikiwe katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2014/2015.
Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa kurekebisha mambo hayo ili
katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha makusanyo yafikie lengo na
ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la nusu ya kwanza.
Takwimu Mpya za Pato la Taifa
Ndugu wananchi,
Ni utaratibu wa kawaida wa nchi zote
duniani kuwa na mwaka unaotumika kuwa kizio (base year) cha kukokotoa
takwimu za Pato la Taifa. Ni utaratibu wa kawaida pia kwa kila baada
ya muda fulani mwaka wa kizio hubadilishwa. Lengo ni kuboresha takwimu
husika. Katika marekebisho hayo pia huingizwa thamani ya bidhaa na
huduma mpya katika pato la taifa na kuziondoa zilizotoweka ili kutoa
picha halisi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika miaka ya hivi karibuni nchi za
Ghana (mwaka 2010), Nigeria (mwaka 2013) na Kenya (mwaka 2014)
wamefanya marekebisho ya takwimu zao za pato la taifa. Na sisi Tanzania
tumefanya hivyo mwaka huu (2014). Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu
kurekebisha takwimu za pato la taifa. Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka
1966, 1976, 1992 na 2001.
Ndugu wananchi;
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekamilisha
marekebisho ya takwimu za pato la taifa na kukokotoa takwimu mpya kwa
kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa kizio. Kutokana na marekebisho
yaliyofanyika, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 70 kwa kutumia bei za mwaka 2007. Ukitumia bei za mwaka 2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 53.17. Kuongezeka kwa pato la taifa kumeongeza pia pato la wastani la kila Mtanzania kutoka shilingi 1,186,200 (sawa na US$ 742) kwa bei za mwaka 2001 hadishilingi 1,560,050 (sawa na US$ 977) kwa bei za mwaka 2007.
Kilimo na Chakula
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini. Uzalishaji ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni 14.38 mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu wa mahitaji yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani milioni 3.25. Katika ziada hiyo, mahindi yanachangia tani milioni 1.55,mchele tani 794,000 na kiasi kinachobakia kinachangiwa na mazao mengine ya chakula.
Ndugu wananchi;
Kuna jambo moja muhimu kuhusu ununuzi
wa nafaka ambalo ningependa kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga
wote na mtama wote unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua
sehemu ndogo tu ya nafaka ya ziada iliyozalishwa na hununua kwa ajili
ya kuweka akiba ya taifa ya chakula cha kutumika wakati wa dharura ya
watu kupata tatizo la njaa. Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana
na uwezo wa maghala yake kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni
kuhifadhi tani 246,000 ingawaje tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa kuhifadhi tani 400,000ifikapo 2015. Hivyo basi kwa Wakala kununua tani 292,415.41 mwaka huu ina maana kwamba kiasi cha karibu tani 50,000 zinahifadhiwa
nje ya maghala kwa kutumia maturubai. Huu siyo utaratibu mzuri na
haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka hiyo kuharibika na
kuzua mgogoro mkubwa siku moja.
Ndugu wananchi;
Baada ya NFRA kununua tani 292,415.41 kuna takribani tani milioni 2.96 za
nafaka ya ziada ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo yetu
ni kuwa wafanyabiashara wetu watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya kuuza
mijini na kwingineko inakohitajika. Bahati mbaya mwaka huu kama
ilivyokuwa mwaka wa jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza kununua
nafaka yote ya ziada ambayo Serikali haikuweza kununua kupitia Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Hali hii imezua tatizo ambalo Serikali kwa
kushirikiana na wafanyabiashara nchini hatuna budi kulitafutia
majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine ndani na hata nje ya
nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada. Nimeagiza Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa chini
na kushirikiana na wafanyabiashara kulitafutia ufumbuzi suala hili
lenye maslahi makubwa kwa wakulima na nchi yetu kwa jumla.
Ndugu Wananchi;
Katika mazingira haya, ninapopata
taarifa ya kuwepo watu wanaotaka kuuza mahindi nje ya nchi lakini
wanawekewa vikwazo na maafisa wa Serikali inanishangaza na
kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya hivyo waache mara moja na
badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao kufanikisha azma yao. Hali
kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao wajitokeze kufanya biashara
hiyo. Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba pawepo na
utaratibu mzuri ili biashara hiyo ifanywe kwa kutumia njia halali na
zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki na wala hakuna sababu
ya kufanya hivyo.
Miradi ya Kimkakati
Ndugu wananchi;
Katika mwaka 2014 utekelezaji wa miradi
mikubwa ya kimkakati kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2011/12 – 2015/16) umeendelea vizuri. Tunayo matumaini makubwa kwamba
katika mwaka 2015 miradi mingi itakamilika.
Tuanze na Mradi wa ujenzi wa bomba la
gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam. Mradi huu
unategemewa kukamilika Januari, 2015. Utakapokamilika utatuwezesha
kutimiza lengo letu la kuzalisha MW 2,780 za
umeme ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya ujenzi wa mitambo ya
kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa
kwenda kwenye masoko, inakwenda vizuri.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi mkubwa wa kimkakati
wa kusambaza umeme vijijini umeendelea vizuri na tumepata mafanikio
makubwa yasiyokuwa na mfano wake katika historia ya nchi yetu. Hadi
kufikia Novemba, 2014, jumla ya vijiji 3,836 vimepatiwa umeme na vingine1,500 vinategemewa kupatiwa umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji 5,336 kati ya vijiji12,423 vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na asilimia 43 ya vijiji vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasa wananchi milioni 17.3 nchi nzima sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na watu milioni 8.1sawa na asilimia 18.4 waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme. Kwa upande wa vijijini mwaka 2012 watu milioni 2.3 sawa na asilimia 7 walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015, idadi hiyo itaongezeka na kuwa milioni 7.4 sawa na asilimia 21.
Haya ni mafanikio makubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini kupata
umeme katika kipindi kifupi kiasi hiki. Ni mageuzi ya aina yake
yatokayotoa mchango muhimu katika kuinua hali za maisha ya Watanzania.
Ndugu Wananchi;
Tunaanza kuiona nuru ya matumaini kwamba
siku si nyingi kutoka sasa, makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya
chuma ya Liganga yataweza kutumika kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wa
Ludewa. Maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015
kuanza ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe kule Mchuchuma, mtambo wa kufua
umeme, ujenzi wa mgodi wa chuma kisichoyeyushwa pale Liganga na ujenzi
wa kiwanda cha kuyeyusha chuma.
Natoa pongezi maalum kwa Shirika la
Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya
China kwa hatua iliyofikiwa. Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika
itatoa ajira 33,000 za moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja.
Ndugu Wananchi;
Mradi mwingine mkubwa wa kimkakati ni
ule wa kujenga Eneo Maalumu la Kiuchumi (Special Economic Zone) la
Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa mpango kazi wa wabia wa mradi huo
yaani Mamlaka ya Kuendeleza Maeneo huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni ya China Merchants Holdings International na
Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali za Serikali ya Oman (Oman State
General Reserve Fund), ujenzi wa bandari na miundombinu mingine
itakayowezesha viwanda kujengwa imepangwa kuanza Julai 2015.
Miundombinu ya Usafiri na Uchukuzi
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga
barabara za lami na kuimarisha barabara za udongo ili ziweze kupitika
wakati wote ziliendelea kote nchini. Huu nao ni mradi mkubwa wa
kimkakati. Barabara za lami 19 zenye urefu wa kilometa 1,459 zimekamilika
kujengwa mwaka huu katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Kagera, Dar es
Salaam, Dodoma, Tanga, Morogoro, Arusha, Tabora na Shinyanga. Ujenzi
unaendelea kwa barabara nyingine 24 katika
mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa, Simiyu, Katavi,
Tabora, Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo wakati wo wote
mwaka 2015 zitakamilika. Maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara
nyingine nane yanaendelea vizuri sehemu mbalimbali nchini.
Kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara,
tumeendelea kufanya kazi ya ujenzi na ukarabati wa barabara za udongo
kote nchini. Mwaka huu Mfuko huo umetengewashilingi bilioni 751.7 ukilinganisha na shilingi bilioni 504.4 mwaka
jana. Aidha, mwaka huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la
Mto Kilombero. Matumini yetu ni kuwa ujenzi wa daraja hilo na Daraja la
Kigamboni utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa Daraja la Malagarasi
ulishakamilika mwaka jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya uzinduzi.
Kwa upande wa jiji la Dar es
Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya barabara za
mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio yetu pia kwamba mabasi yataanza
kusafirisha abiria katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2015.
Halikadhalika, tunategemea katika mwaka 2015 ujenzi utaanza wa barabara
zinazozunguka jiji la Dar es Salaam (ring roads), barabara ya Mwenge -
Morocco na ile ipitayo juu ya nyingine (flyovers) eneo la TAZARA. Vile
vile, daraja jipya la Salenda litaanza kujengwa. Aidha, kivuko cha
abiria 300 cha
MV Dar es Salaam kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam
Kaskazini na Ferry mapema mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza
msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Usafiri wa Anga na Reli
Ndugu wananchi;
Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea kwa mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane vya treni vimekarabatiwa, mabehewa mapya 22ya abiria na mabehewa 274 ya
mzigo yamenunuliwa. Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini kati ya
Novemba na Desemba mwaka huu. Kati ya Januari na Mei, 2015 tunatarajia
kupokea vichwa vipya vya treni 13.
Uboreshaji huu wa huduma za treni unakwenda sambamba na ukarabati wa
reli yenyewe, ujenzi wa madaraja na kuimarisha maeneo yaliyo korofi
katika reli hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli iliyo pana zaidi
(standard guage), yenye uwezo wa kubeba mabehewa mengi na kuwezesha
treni kwenda kwa mwendo wa kasi zaidi, juhudi za kutafuta fedha za
ujenzi au wabia wa kushirikiana nasi kujenga zinaendelea. Wakati huo
huo, tunaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya
TAZARA ili mambo yaende vizuri. Tutashirikiana kwa karibu na wabia
wenzetu wa Zambia. Bahati nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga
mkono juhudi zetu za kufufua reli ya TAZARA.
Usafiri wa Anga
Ndugu Wananchi;
Sekta ya usafiri wa anga
imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya abiria wanaowasili na
kutoka katika viwanja vyetu vya ndege nchini imeongezeka kutoka abiriamilioni 2.5 mwaka 2013 hadi abiria milioni 3.5 kufikia Septemba, 2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi za nje zimeongezeka kutoka 274 Januari, 2013 hadi 295 kufikia Septemba, 2014. Hili ni ongezeko la asilimia 8. Safari za ndege ndani ya nchi nazo zimeongezeka kutoka safari 230,458 mwaka 2013 hadi safari 241,922 mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 39. Maongezeko haya ni kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii na biashara nchini zimeendelea kukua.
Ndugu Wananchi;
Ujenzi wa Jengo la 3 (Terminal 3) la
Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea
vizuri. Jengo hilo litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa
kuhudumia wastani wa abiria milioni 8 kwa mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la 2(Terminal 2) utafanyika
ili liweze kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi huo,
Wakala wa Viwanja vya Ndege wameendelea kukarabati na kuboresha viwanja
vya ndege vya KIA, Mwanza, Songwe, Bukoba, Tabora na Kigoma. Tunatarajia ukarabati wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga kuanza mapema mwaka 2015.
Elimu
Ndugu wananchi;
Tumeendelea kupiga hatua za
kuridhisha katika kuboresha elimu nchini. Tumefanikiwa kupunguza tatizo
la upungufu wa maabara, vitabu na walimu wa shule za msingi na
sekondari. Mwaka huu tumeajiri walimu 36,339 kati ya 81,562 wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu 45,223 yaani 26,946 wa shule za msingi na 18,277wa shule za sekondari hususan wa masomo ya sayansi. Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari.
Mwaka huu tumeanza mpango
maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya Ualimu kwa masomo ya sayansi na
hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo jumla ya wanafunzi 5,602 wa
masomo hayo wamedahiliwa. Mpango huu utatuwezesha kupunguza pengo kubwa
tulilonalo la walimu wa sayansi katika muda mfupi zaidi.
Ujenzi wa Maabara
Ndugu wananchi;
Ujenzi wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za Kata 3,463umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe maabara 10,389ilipofika Novemba, 2014. Taarifa kutoka TAMISEMI zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 29, 2014, maabara 4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara5,688 sawa na asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.
Ndugu Wananchi;
Natoa pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa,
Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za
Wilaya na Miji nchini pamoja na wananchi, kwa jitihada kubwa
iliyofanyika. Kwa kutambua jitihada hizo, nimeongeza miezi sita zaidi
kwa wale ambao hawajakamilisha ujenzi wa maabara hizo wafanye hivyo.
Sikusudii kuongeza tena muda baada ya hapo. Naomba watumie kipindi
hicho kitumike kutafuta vifaa vya maabara. Serikali itasaidia
upatikanaji wa watunza maabara (laboratory technicians) ambao tumeanza programu kubwa ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya maabara.
Ununuzi wa Vitabu
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea kupunguza tatizo la
uhaba wa vitabu na vifaa vya kufundishia katika shule za msingi na
sekondari. Tumekuwa tunanunua vitabu kwa kutumia Bajeti ya Serikali na
misaada kutoka kwa marafiki zetu wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali ya
Marekani imetupatia vitabu milioni 2.5 vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule za sekondari. Ongezeko hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wanne na kufikia kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili. Lengo letu ni kila mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo ifikapo mwaka 2016.
Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Ndugu wananchi;
Mafanikio mengine tuliyopata mwaka huu
ni kukamilika kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua
muhimu sana katika maendeleo ya elimu nchini hakuna badala yake. Sera
mpya inalenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na
taratibu zitakazowezesha Watanzania wengi zaidi kupata fursa za elimu
iliyo bora na inayolinga na wakati tulionao. Jambo jipya sana na la
kihistoria katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa
ada katika elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada
kwenye shule za msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu
ya sekondari. Kwa mujibu wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa
maagizo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango kuanza
kutafakari namna jambo hilo litakavyotekelezwa.
Afya
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2014 jitihada za kuboresha
huduma ya afya kwa Watanzania ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na
mlipuko wa homa ya dengue iliyowapata watu 1,039 na kusababisha vifo vya watu 3 kati
yao. Kwa upande wa maradhi ya ebola tumejiandaa vya kutosha kutambua
watu wenye maradhi hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya ndege vya
kimataifa na vituo vyote vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema
kuwahudumia wagonjwa wa maradhi hayo iwapo watatokea.
Mwaka huu pia, Madaktari wetu watano wamekwenda
Liberia kusaidiana na ndugu zetu wa huko katika kukabiliana na ugonjwa
wa ebola. Madaktari wetu hao wako salama na wanaendelea vizuri kutoa
huduma. Madaktari hao watakaporejea nchini watakuwa hazina kubwa ya
taifa katika kupanga mipango ya kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hali
kadhalika, watakuwa viongozi wa wengine katika kutibu wagonjwa wa
maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.
Ndugu Wananchi;
Katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri watumishi wa sekta ya afya 8,345 ambao kati yao kuna madaktari 244, madaktari bingwa 75, wauguzi 2,555na wataalamu wa kada nyingine za afya 5,471. Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 7,956 katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi9,730. Kwa ongezeko hilo, sasa tumefikia asilimia 97 ya lengo letu la kudahili wanafunzi10,000 ifikapo mwaka 2017.
Jitihada zetu za kuongeza fursa za
mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na wataalamu wengine wa afya zina
muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya kufundishia pale Mloganzila
unaendelea vizuri na hospitali ya kufundishia ya Chuo Kikuu cha Dodoma
umekamilika. Ni matarajio yangu kuwa wakati wo wote mwakani ujenzi wa
kampasi mpya ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila utaanza. Ujenzi
huo ukikamilika Chuo kikuu cha Muhimbili kitaweza kudahili wanafunzi 12,000 kutoka wanafunzi 2,500 wa
sasa jambo ambalo litafanya upungufu wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu
wa Afya kupata jawabu la uhakika. Tumeendelea kufanya mambo mengine
ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za ubongo na mishipa ambalo limekamilika
pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata vifaa.
Maji
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kuwapatia
wananchi maji safi na salama mijini na vijijini. Kwa ajili hiyo
miradi 498 ya maji vijijini imekamilika na miradi 740 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Miradi mingine 378ipo katika maandalizi ya ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba katika mwaka ujao wa 2015, miradi mingine 731 itatekelezwa na vituo 25,790 vya kuchota maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza kuwafikia asilimia 71 ya wananchi wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 58 ya sasa. Kwa ajili hiyo, tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la kuwapatia watu maji asilimia 65 ya
Watanzania waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi langu kwa ndugu zetu wa
Hazina waiangalie sekta hii ya maji kwa ukaribu zaidi na wawapatie fedha
kwa wakati.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga – Same – Mkomazi pamoja
na miji na vijiji vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015. Fedha
zimekwishapatikana na Mkandarasi wa Awamu ya Kwanza ameshapatikana.
Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana muda si mrefu kutoka
sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi wa maji wa mji wa
Orkesment.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu miradi ya kuipatia maji miji
kadhaa nchini ilikamilika na tatizo la upungufu wa maji litakuwa
limepatiwa ufumbuzi. Ipo miji kadhaa ambayo miradi imefikia hatua ya
juu na kwamba wakati wowote mwakani itakamilika. Jiji la Dar es Salaam
lipo katika kundi hili. Kazi ya upanuzi wa miradi ya maji ya Ruvu Juu
na Ruvu Chini kwa msaada wa Serikali ya Marekani na mkopo kutoka
Serikali ya India imefikia hatua nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Mwaka ujao pia visima virefu vya
Kimbiji na Kipera vitachimbwa na Bwawa la Kidunda litaanza kujengwa.
Serikali ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola za Marekani milioni 268.2 kwa
ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya Tabora, Nzega na
Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha miji ya Sikonge
na Urambo katika mradi huo utaangaliwa.
Bunge na Mahakama
Ndugu Wananchi;
Katika
mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza vyema
majukumu yao. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza
kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa pamoja na kulazimika kugawana
Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la Katiba. Bunge limefanya
mikutano mitatu, Miswada 17 ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria tano na maazimio saba yalipitishwa. Maswali ya msingi 569 na ya nyongeza 1,541yaliulizwa
na kujibiwa. Aidha, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nalo
lilijadiliwa na kutolewa maazimio. Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu
maazimio hayo na bado tunaendelea.
Napenda kuitumia nafasi hii kutoa
pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa kutekeleza vizuri wajibu wao wa
Kutunga Sheria na kusimamia Serikali. Nawasihi waendelee na msimamo huo
mwema na chanya kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Mahakama napenda
kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa ya kupunguza mrundikano wa
mashauri katika Mahakama za ngazi zote. Wahenga wamesema “mcheza kwao hutunzwa”.
Hatuna budi kutoa pongezi maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed
Chande Othman kwa uongozi wake mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji wa
Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na
Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wamejiwekea malengo ya kusikiliza na
kutoa hukumu kwa mashauri yasiyopungua 200 kwa mwaka kila mmoja wao.
Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea vizuri. Mashauri 870 yalisikilizwa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya Rufani, mashauri 11,334kwenye Mahakama Kuu, mashauri 8,715 kwenye Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683 katika
Mahakama za Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa
Mahakama Kuu kwa wakati mmoja kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama
ilivyofanyika Kigoma, Shinyanga na Tabora umesaidia sana kupunguza
mrundikano wa mashauri ya siku nyingi. Haijawahi kutokea mashauri mengi
kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika historia ya Mahakama nchini.
Ndugu Wananchi;
Mkakati huu mpya umeleta matumaini mapya
kwamba tatizo la kuchelewesha kwa mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni
tatizo sugu sasa limeanza kupatiwa ufumbuzi. Kwa niaba ya Watanzania
wenzangu wote natoa shukrani na pongezi nyingi kwa Jaji Mkuu, Majaji wa
Rufani, Jaji Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa ngazi zote
kwa kazi nzuri waifanyayo.
Hali kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu
wa Mahakama na watendaji wote wa Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya
kuwawezesha Majaji na Mahakimu kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika
utendaji Mahakamani umebadilika na kuwa bora zaidi. Mimi naahidi
kuendelea kusaidia Mahakama kwa kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina kutoa
kwa wakati pesa zilizotengwa katika bajeti.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Mapambano dhidi ya rushwa na
matumizi mabaya ya madaraka yameendelea bila ya ajizi. Katika mwaka
huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237 na wamekamilisha uchunguzi wa mashauri 545. Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni428. Mashauri yaliyomalizika ni 205, kati ya hayo 125 watuhumiwa waliachiliwa na 80walipatikana na hatia na kuhukumiwa. Mwaka huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye thamani ya shilingi bilioni 38.96 zimeokolewa. Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji, maafisa wapya 394 wameajiriwa.
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu wa 2014 tuliadhimisha miaka 50
ya Muungano wa nchi zetu mbili yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na
Jamhuri ya Tanganyika kwa heshima inayostahili. Maadhimisho yalifikia
kilele tarehe 26 Aprili, 2014 na zilifanyika sherehe nchini kote na
sherehe hizo zilifana sana. Ni ukweli usiopingika kuwa kwa Muungano
wetu kuweza kudumu kwa nusu karne ukiwa bado imara na unazidi kustawi ni
mafanikio makubwa. Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri. Naamini
Muungano wetu utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa
kwani yale mambo yenye kuleta matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa
ufumbuzi.
Miaka 50 ya JWTZ
Ndugu Wananchi;
Wakati nchi inasherehekea miaka 50 ya
Muungano, baadhi ya vyombo na taasisi muhimu kitaifa zilifanya hivyo
hivyo. Miongoni mwa walioadhimisha nusu karne ya kuundwa kwake ni Jeshi
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe 1
Septemba, 1964. Jeshi letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi
kubwa la kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli
Mkoani Arusha.
Nilibahatika kushuhudia siku ya mwisho
ya zoezi hilo. Nilifurahishwa sana na kiwango cha utayari kivita cha
Jeshi letu. Wanajeshi wetu walionesha weledi wa hali ya juu, umahiri
mkubwa, ujasiri, ukakamavu na uvumilivu wa aina yake wakati wa
kutekeleza majukumu yao katika mazingira magumu ya uwanja wa medani za
vita. Niliwapongeza siku ile na narudia tena leo kuwapongeza.
Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na Watanzania wote kuwa Jeshi letu la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko imara kulinda mipaka ya nchi yetu na
kuhakikisha usalama wa taifa letu na watu wake. Jeshi letu bado ni lile
tunalolijua sisi sote, lakini limezidi lile lililomng’oa mvamizi
Dikteta Iddi Amin wa Uganda, tena limezidi kwa mbali.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu pia tumeshuhudia kukamilika
kwa zoezi muhimu la kuandika Katiba Inayopendekezwa. Kama tujuavyo sote,
mchakato uliozaa Katiba Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi
ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo
lilikamilisha kazi yake kwa salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba,
2014 ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar,
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein tulikabidhiwa nakala za Katiba
Inayopendekezwa tarehe 8 Oktoba, 2014. Nimeshatimiza wajibu wangu wa
kuchapisha katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya
maoni kuwa tarehe 30 Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya
Uchaguzi kufanya matayarisho husika ya kuwezesha Kura ya Maoni
kufanyika.
Ndugu Wananchi;
Moja ya mambo muhimu ambayo Tume ya
Uchaguzi inafanya kwa sasa ni kuandikisha wapiga kura katika Daftari la
Mpiga Kura. Tume imeamua kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters
Register. Uandikishaji wa majaribio umefanyika katika baadhi ya Kata
katika Majimbo ya Mlele, Kawe na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza
yatasaidia kuboresha mfumo huo kabla ya uandikishaji wa watu wote wenye
sifa stahiki kuanza.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii
kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa mfumo mpya unatengeneza
Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha inayotumika ni uboreshaji wa
Daftari la sasa. Uboreshaji huu wa Daftari la Mpiga Kura ni tofauti na
ule tuliouzoea ambapo walikuwa wanaandikishwa wapiga kura wapya na wale
waliopoteza vitambulisho vyao. Safari hii wanaandikishwa wote wapya na
wa zamani na wote watapata vitambulisho vipya. Hivyo basi, sisi wenye
vitambulisho vya kupiga kura vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze
kujiandikisha wakati ukifika.
Jambo la pili ni kwamba, Daftari la
Mpiga Kura linalotayarishwa siyo kwa ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa peke yake, daftari hilo hilo litatumika pia kwenye
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo basi, kujiandikisha ni jambo
muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu utajinyima fursa ya kushiriki
kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa bali pia utakosa fursa ya kuchagua
Rais wako, Mbunge wako na Diwani wako. Katu usikubali yakukose hayo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo tarehe 14
Desemba, 2014 na 20 Desemba, 2014 ulifanyika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa. Uchaguzi
umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni wajibu wa viongozi
hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha uchaguzi ni wakati mzuri
wa kufanya tathmini ili wapate mafunzo yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa
TAMISEMI na Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri, lengo liwe ni kuona
namna ya kuimarisha mazuri na kusahihisha makosa na matatizo
yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa amani watambue matatizo ya kiusalama
yaliyotokea na kuona namna ya kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya
namna hiyo yasijitokeze tena. Hatma ya yote, shabaha yetu ni kutaka
kufanya vizuri zaidi katika chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na
kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu Tanzania imechaguliwa kuwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni zamu yetu kwa mujibu wa
mzunguko wa uongozi wa Jumuiya yetu kati ya nchi wanachama. Ni dhamana
kubwa na kwamba wenzetu wa Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze
katika kutekeleza malengo na madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa
katika Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika,
tunategemewa kuongoza katika utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya vikao
vya Jumuiya. Hii inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa kabla yetu ambayo
utekelezaji wake unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa katika kipindi
cha uongozi wetu.
Kwa niaba ya Watanzania wote napenda
kuwashukuru ndugu zetu wa Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda kwa
kutuamini. Napenda kuahidi kuwa hatutawaangusha. Sisi Watanzania
tutafanya kila tuwezalo kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
manufaa ya Jumuiya yenyewe, nchi zetu na wananchi wa Afrika Mashariki.
Tutajitahidi kuwa wabunifu kwa nia ya kuona utangamano unakua na kustawi
kwa kasi na kuzaa matunda ya maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda
tuliyoyatarajia tulipoamua kuanzisha Jumuiya hii na matunda tuliyoyapata
tulipoamua kwa hiari yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.
SADC, AU NA UN
Ndugu Wananchi;
Kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, tunaahidi
kuendelea kuwa wanachama waaminifu na kushiriki kwa ukamilifu katika
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mashirika haya ya kikanda na
kimataifa. Kwa upande wa SADC tutaendelea kushiriki katika utekelezaji
wa mikakati na mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na ile ya
kisiasa na kiusalama kama ilivyoainishwa katika RISDP (Regional
Indicative Strategic Development Plan) na SIPO (SADC Strategic
Indicative Plan for the Organ). Kwa ajili hiyo Tanzania, itaendelea
kutoa mchango wake katika kukuza utangamano wa kiuchumi katika SADC na
kusaidia kuimarisha uhusiano mwema na usalama miongoni mwa nchi
wanachama wa SADC. Hii ni pamoja na kusaidia katika kutatua migogoro ya
kisiasa na kusalama kati ya nchi wanachama.
Kwa upande wa Umoja wa Afrika
tutaendelea kutekeleza maamuzi ya vikao na taasisi mbalimbali za Umoja
huo. Daima tutakuwa wanachama waaminifu wa Umoja wa Afrika na kuchangia
katika uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa Mataifa tutaendelea kutimiza
wajibu wetu kama wanachama wa Umoja huo wa kimataifa ulio adhimu na
muhimu kwetu na dunia nzima. Tutaendelea kushiriki katika shughuli za
ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao wanajeshi
wetu katika majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi za
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari wakati
wote kuchangia zaidi iwapo Umoja wa Mataifa watatutaka tufanye hivyo.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Namaliza
hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa kuiunga
mkono Serikali yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu kupata
mafanikio haya makubwa tunayojivunia katika mwaka 2014. Tumeweza kuvuka
mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. Umoja wetu na mshikamano wetu
ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka 2015 kwa matumaini
makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea kuliimarisha zaidi
taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo huenda ukawa na
changamoto na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu. Uelewa wetu,
umoja wetu, mshikamano wetu na moyo wetu wa uzalendo ndivyo
vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma. Mimi nina imani
kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa nzuri
ya nchi yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na
utulivu. Tumeweza mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na
miaka ijayo. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka
mpya.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza
tiko
tiko
Post a Comment