tiko
tiko
Zari hivi sasa limekuwa jina maarufu
katika masikio ya Watanzania, Afrika Mashariki na kwingineko hasa baada
ya mwanadada huyo mfanyabiashara na mwanamuziki wa Uganda kuwa na
urafiki na Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nassib Abdul maarufu kwa jina la
usanii Diamond Platnum.
Kwenye mitandao ya kijamii kama Tweeter,
Facebook, Instagram na hata Whatsapp lazima utakutana na jina Zari
akiunganishwa na Diamond na wengine wataunganisha na Wema Sepetu
aliyewahi kuwa mpenzi wa Diamond.
Uhusiano kati ya Zari na Diamond umezua
gumzo kila eneo Tanzania na Afrika Mashariki huku wakifananishwa na
mastaa wa nje kama vile Kanye West na Kim Kardashian kwa namna
wanavyofuatana wakati wote huku Diamond akionesha kila aina ya mbwembwe
za kumjali mrembo huyo kutoka Kampala, Uganda.
Uhusiano wa Zari na Diamond umewafanya
kuandamana kila sehemu hivi sasa. Wawili hao walianza kuonekana kuwa na
ukaribu wa mahusiano tangu Diamond alipokwenda Afrika Kusini kwenye Tuzo
za Channel O ambapo Diamond aliibuka na ushindi wa Tuzo tatu.
Baada ya Tuzo hizo, Zari alimualika
Diamond kushiriki katika ‘pati’ maarufu ambayo mwanadada huyo huandaa
kila mwaka nchini Uganda ambapo mwaka huu ilijulikana kama All White
Ciroc Party.
Wawili hao baada ya sherehe hiyo,
walifuatana ambapo Zari alimsindikiza Diamond nchini Rwanda na Burundi
alipokwenda kutoa burudani nchini humo, na picha kusambazwa katika
mitandao ya kijamii na kuwafanya wawili hao kuwa gumzo hivi sasa katika
mitandao Tanzania na Afrika Mashariki. Je, Zari ni nani hasa? Zarina
Hassan Tlale.
Maarufu kama Zari ni Mganda anayeishi
Afrika Kusini. Mrembo huyo ni mwanamuziki na mfanyabiashara. Ni mwanamke
aliyefanikiwa na anayependa kuishi maisha ya kifahari. Anamiliki magari
ya kifahari na yenye gharama kubwa kama Lamborghini Gallardo, BMW-
2006, Chrysler-2008, Audi Q7-2010 na Ranger Rover Sports .
Mwanadada huyo ni binti wa Halima Sultan
Hassan na Nasur Hassan akiwa na asili ya damu mchanganyiko ikiwa ni
pamoja na ya Kihindi , Toro, Somalia na Burundi kutoka mji wa Jinja,
Uganda. Babu mzaa mama yake anatoka India na bibi yake ni kutoka Uganda.
Babu yake mzaa baba ni kutoka Somalia na bibi yake mzaa baba anatoka
Burundi.
Zari maarufu kama The Bosslady aliwahi
kuolewa na mwanamume anayejulikana kwa jina la Ivan na kubarikiwa watoto
watatu wa kiume Pinto, Didy na Quincy na anamiliki kampuni tatu.
Mwanadada huyu alizaliwa Septemba 23, 1980. Zari amekulia katika mji wa
Jinja katika nchi ya Afrika Mashariki inayojulikana kama Uganda.
Zari alisoma shule ya msingi, kisha
kwenda Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jinja ambapo alisoma kwa bidii
kutimiza ndoto zake. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, mwanadada
huyo alihamia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kampala ambapo alikuwa
akitoa burudani ya muziki katika maeneo ya starehe kabla ya kuhamia
mjini London, Uingereza na kusomea Stashahada ya masuala ya urembo
(cosmetology).
Historia yake kimuziki inaonesha Zari
alianza kuimba akiwa na umri mdogo wakati akisoma shule ya msingi ambapo
alikuwa akitoa burudani katika matamasha ya muziki yaliyokuwa
yanaandaliwa na wafanyakazi wa shule, wakati wa hafla za mwishoni mwa
mwaka na katika mashindano mengine ya jumuiya akiwakilisha shule yake.
Ingawa amekulia katika familia ya
Kiislamu yenye wasichana sita na wavulana wawili, Zari hakuacha mapenzi
yake kwenye muziki. Alianza muziki akiwa na umri mdogo na albamu yake
ina nyimbo kali kama ‘Toloba’ na ‘Hotter Than Them’. Watu waliomvutia
katika muziki ni Wasanii wa Marekani Arethal Franklin na Whitney Houston
wakati akiwa sekondari.
Afrika waliomvutia akapenda muziki ni
wanamuziki wa Afrika Kusini Brenda Fassie, Miriam Makeba, Lucky Dube na
Malkia wa Muziki Afrika Kusini, Yvone Chaka Chaka. Alipojiunga na
sekondari alijiunga na makundi ya dansi, drama na muziki jambo ambalo
lilimsaidia kuchaguliwa kwa miaka miwili mfululizo la Muigizaji Bora.
Baada ya miaka miwili ya kufanya vizuri
katika majukwaa na matamasha ya shule, alipumzika na kuhama kutoka
Uganda kwenda London, Uingereza na kuendelea na masomo yake lakini bado
mapenzi yake kwa muziki yakiwa mawazoni mwake. Zari kwa msaada wa
familia, mashabiki na marafiki wa- naopenda mtindo wa muziki wake na
kuamini anaweza aliamua kuchukua hatua mwaka 2007 wa kurekodi singo yake
ya kwanza inayoitwa Oliwange (ikiwa na maana wewe ni wangu) .
Mwaka 2008 Zari alishinda Tuzo ya
Channel O ya Video Bora ya Muziki ya Msanii Bora Afrika Mshariki. Hafla
ya tuzo hizo ilifanyika Johannesburg, Afrika Kusini. Tangu hapo Zari
ameendelea kutoa nyimbo zaidi za kuvutia, huku akitiwa moyo na mashabiki
wake wakati huo.
Mwaka 2009 alipata Tuzo inayojulikana
kama Diva ya mwaka katika kipengele cha Diaspora tangu hapo aliendelea
kutengeneza muziki. Zari hivi sasa anaishi Afrika Kusini ambapo
anamiliki maduka makubwa ya vipodozi na shule ya elimu ya juu mjini
Pretoria wakati akiendelea kujijenga kimuziki.
Inaelezwa kuwa Zari na aliyekuwa mumewe
Ivan wanamiliki Shule ya Brooklyn City ambayo ina kampasi sita Afrika
Kusini, huku kila moja ikiwa na wanafunzi kati ya 800 hadi 2,100.
Wanafunzi hao hupewa vyeti vya taifa wanapomaliza mwaka. Vile vile Zari
amejenga hosteli iliyopo barabara ya Sir Apollo Kaggwa, Kampala na
anamiliki nyumba kadhaa katika mji huo hasa eneo la Munyonyo, pamoja na
duka kubwa la nguo Afrika Kusini.
Ingawa muziki wake haujafanya vizuri
kama wanamuziki wengine wa Uganda akiwemo Jose Chameleone, Bebe Cool,
Bobi Wine na Ragga Dee, Zari amekuwa akifurahia kwa mafanikio zaidi
kwenye biashara na kutokana na hilo anasema lazima arudishe kwa jamii na
hivyo kuamua kusaidia vituo na taasisi kadhaa zinazohitaji misaada kama
Katalemwa Cheshire Home, Sanyu Babies’ Home pamoja na Gereza la Luzira.
Mfano mwaka 2013 kutokana na moyo wake
wa kusaidia, kwa kutimiza hilo baada ya sherehe zake anazozifanya kila
mwisho wa mwaka aliamua kutembelea Kituo cha Watoto Yatima cha M-Lisada
kilichopo Nsambya siku moja kabla ya Sikukuu ya Krismasi, akifuatana na
watoto wake Pinto, Didy na Quincy.
Alitoa zawadi maalum kwa watoto hao,
ambapo Zari alishiriki kuandaa chakula cha Krismasi na kisha baadaye
kutoa msaada wa vitu vyenye kama vile taulo za wanawake, sukari,
biskuti, mchele na matoke. Mbali na masuala mengine yote, kwa mujibu wa
tafiti mbalimbali, watu wengi nchini Uganda wanakubaliana kuwa Zari ndio
Mwanamke Mrembo zaidi nchini humo.
“Sitafuti umaarufu, wenyewe umaarufu
ndio hunifuata,” aliwahi Zari kusema kupitia mtandao wa Red Pepper
akikanusha habari za baadhi ya watu wanaodai kuwa anatafuta umaarufu kwa
nguvu.
Habari zake kuandikwa katika mitandao ya
kijamii pamoja na shughuli zake za uhisani zimesababisha wengi kudai
kuwa anataka tu umaarufu, kujulikana na kuzungumziwa kila wakati.Hata
hivyo akijibu madai hayo, Zari alisema umaarufu unamtafuta yeye na sio
kwamba yeye anautafuta.
>>>bofya hapa habari zaidi<<<
tiko
tiko
Post a Comment